Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha England alia na ulinzi

TUCHEL Pict

Muktasari:

  • England inatarajiwa kushuka dimbani Jumanne dhidi ya Jamhuri ya Czech katika Ligi ya Mataifa ya Ulaya, ikiwa na presha ya kurejea kwenye njia ya ushindi baada ya kupoteza mabao 3-2 dhidi ya mabingwa wa dunia, Hispania, Jumamosi.

LONDON, ENGLAND: KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, ameonya safu yake ya ulinzi baada ya kukiri kuwa kikosi chake kimekuwa “hatari kwao wenyewe” kutokana na makosa ya kiufundi yanayoigharimu mabao.

England inatarajiwa kushuka dimbani Jumanne dhidi ya Jamhuri ya Czech katika Ligi ya Mataifa ya Ulaya, ikiwa na presha ya kurejea kwenye njia ya ushindi baada ya kupoteza mabao 3-2 dhidi ya mabingwa wa dunia, Hispania, Jumamosi.

Kipigo hicho kimeifanya England kufungwa jumla ya mabao 13 katika michezo sita iliyopita, huku ikiwa imeweka rekodi ya kutoruhusu bao katika mechi nne pekee kati ya 13.

Tuchel amesema tatizo kubwa limekuwa makosa ya wachezaji wenyewe, hasa wakati wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma.

“Tunapaswa kuboresha mambo kwa sababu tulipokuwa na mpira tulikuwa hatari zaidi kwetu wenyewe eneo la boksi. Tulifanya makosa mengi ya mtu mmoja mmoja, hasa wakati wa kuanza kujenga mchezo kutoka nyuma,” amesema Tuchel.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 amesisitiza kuwa England haiwezi kuendelea kufanya makosa ya aina hiyo katika kiwango cha juu.

“Hilo ni jambo ambalo hatuwezi kulirudia katika kiwango hiki. Tunapaswa kuwa makini na sahihi kabisa kiufundi tunapokuwa kwenye presha.”


TUCH 01

GUEHI AENDELEA

Licha ya kosa lake lililozaa bao la mapema la Hispania kupitia Lamine Yamal, beki Marc Guehi anatarajiwa kuendelea kupewa nafasi katika kikosi kitakachokabiliana na Czech mjini Prague.

Tuchel amedhamiria kuendelea na safu ileile ya mabeki, ingawa Ezri Konsa na Nico O’Reilly wana mashaka ya kuwa fiti baada ya kukosa mazoezi kutokana na matatizo madogo ya kiafya.

“Walikosa mazoezi kutokana na matatizo madogo ambayo bado yapo. Wanahitaji kufanyiwa tathmini na tutafanya uamuzi,” amesema.

Pamoja na England kuruhusu mabao matatu dhidi ya Hispania, Tuchel amesema hana wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa timu yake kujilinda.

“Katika ulinzi sina wasiwasi na ninaamini tunaweza kufanya vizuri. Kuna baadhi ya wachezaji ambao hawapo hapa na ambao wangetusaidia katika kupanga mfumo wa ulinzi,” amesema.


Ameongeza: “Ulinzi wetu ulikuwa na nidhamu, mshikamano na mpangilio mzuri zaidi kuliko baadhi ya mechi za Kombe la Dunia. Hatukupoteza mfumo wetu. Matokeo yaliathiriwa zaidi na makosa ya mtu mmoja mmoja, na hilo linaweza kutokea.”


TUCH 02

BELLINGHAM AMVUTIA

Kiungo Jude Bellingham alikuwa miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango kizuri dhidi ya Hispania, akimsaidia Anthony Gordon kufunga bao la kusawazisha.

Bellingham pia amekuwa na mwanzo mzuri akiwa na Real Madrid msimu huu, akifunga mabao matatu na kutoa pasi tatu za mwisho.

Tuchel amesema anafurahishwa na namna kiungo huyo alivyojumuika ndani ya kikosi cha England, ndani na nje ya uwanja.

“Anaonekana kuwa mwanachama halisi wa kikosi, ndani na nje ya uwanja. Nilipenda sana kiwango chake,” amesema.

Tuchel pia amefichua kuwa Bellingham alicheza katika nafasi ambayo inampa uhuru wa kusaidia pande zote mbili za uwanja.

“Ilikuwa nafasi mpya kidogo kwake ambapo anaweza kuongeza nguvu pande zote mbili. Hilo linamfaa sana.”

Baada ya kupoteza dhidi ya Hispania, England inahitaji matokeo chanya dhidi ya Czech ili kuendelea kuwa na matumaini katika kampeni yake ya Ligi ya Mataifa.

Hata hivyo, Tuchel amesisitiza kuwa bado ni mapema kuitaja mechi hiyo kama ya “lazima kushinda”.

“Bado ni mapema kwenye kundi kuitaja kama mechi ya lazima kushinda,” amesema.