AKADEMI ZA HISPANIA: Siri iliyomsuka Yamal na wenzake
Muktasari:
- Mapitio makubwa ya kitaifa kuhusu maendeleo ya soka katika nchi fulani kwa kawaida huhusishwa na vipindi virefu vya kutofanya vizuri au vifupi vya kushuka kwa kiasi kikubwa. Kwa nchi zilizokuwa vizuri huko nyuma, mifano miwili ya hivi karibuni ni Ujerumani na England.
MADRID, HISPANIA: HISPANIA imeshinda mashindano makubwa mawili ya kimataifa ya wanaume mfululizo, ambapo mfumo wa kuwatoa wachezaji kutoka akademi hadi timu za wakubwa katika klabu za La Liga umewasaidia.
Mapitio makubwa ya kitaifa kuhusu maendeleo ya soka katika nchi fulani kwa kawaida huhusishwa na vipindi virefu vya kutofanya vizuri au vifupi vya kushuka kwa kiasi kikubwa. Kwa nchi zilizokuwa vizuri huko nyuma, mifano miwili ya hivi karibuni ni Ujerumani na England.
Kwa Ujerumani, kutolewa kwao katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia 1998 na Croatia ulikuwa wakati muhimu wa kutafakari upya na kuongeza uwekezaji katika soka la vijana. Hivyo, wakati kulipotokea hasira na wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina baada ya timu ya taifa kushindwa kuvuka hatua ya makundi ya Euro 2000, hatua za kuboresha mambo zilikuwa tayari zimeanza. Ujerumani iliendelea kuwa mshindi wa pili katika Kombe la Dunia 2002, ikamaliza ya tatu katika Kombe la Dunia 2006 na 2010, kabla ya kushinda 2014.
England, kwa upande mwingine, ilishindwa hata kufuzu Euro 2008, na hilo likafuatiwa na kutolewa na Ujerumani katika hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia 2010. Takribani miezi sita baada ya hilo, Chama cha Soka England (FA) kilizindua mapitio ya maendeleo ya vijana yaliyotoa mapendekezo 25 yaliyolenga kuboresha kiwango cha soka katika kila ngazi, lakini hasa soka la ngazi ya chini.
Mapitio hayo yanakubalika kwa kiasi kikubwa kuwa kichocheo kikubwa cha kuboreka kwa matokeo ya England katika mashindano makubwa ya kimataifa ya wanaume katika miaka ya karibuni, huku Three Lions ikifika nusu fainali mara nne katika Kombe la Dunia na michuano ya Ulaya tangu 2018, idadi sawa na nusu fainali zote walizowahi kufikia katika historia yao kabla ya Kombe la Duni lililopigwa Russia 2018.
HISPANIA IKOJE?
Kwa miaka kadhaa, Hispania ilifanya mapitio yake kuhusu maendeleo ya vijana na kwa sasa iko katika awamu ya pili ya mpango wa miaka 10 hadi 12 unaoongozwa na La Liga kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha akademi za vijana, ambao kimsingi ni mkakati wa kuzifanya ziendeshwe kitaalamu zaidi. Lakini, kama Juan Florit, mkuu wa miradi ya soka wa La Liga anavyoeleza, mageuzi ya akademi nchini Hispania yalikuwa tofauti na mifano iliyotangulia kwa sababu hayakuanzishwa kutokana na mgogoro.
“Kwa kawaida, nchi, taasisi kama La Liga au chama cha soka inapoanza mradi kama huu, huanza ikiwa katika hali ya udhaifu, ikiwa na tatizo au katika hali hasi. Lakini tukifikiri kwamba hili litatosha kwa muongo wa kwanza, mapema au baadaye tutakuwa nyuma ya nchi nyingine tena,” anasema.
Mwaka 2016, klabu kutoka madaraja mawili ya juu zilianza kuandaa uzoefu kupitia akademi za vijana kila mwaka kwa lengo la kubadilishana maarifa, mbinu na zana, zikiwa na matumaini ya kuongeza ushindani. Ni kweli kwamba wakati huo Hispania ilikuwa imetoka kufanya vibaya katika Euro 2016, baada ya pia kushindwa kuvutia katika Kombe la Dunia 2014. Lakini bado, ilikuwa miaka minne tu tangu washinde Euro 2012, ambayo ilikuwa taji lao la tatu mfululizo katika mashindano makubwa ya kimataifa. Soka la Hispania halikuwa katika mgogoro.
Mikutano ya akademi za vijana ilisababisha kuundwa kwa mpango wa kitaifa uliolenga kuinua “soka la ngazi ya chini hadi kiwango kipya” ambao umeibua nyota kubwa kama kina Lamine Yamal.
Baada ya hapo timu ya wakubwa ilifika nusu fainali ya Euro 2020 iliyochezwa mwaka mmoja baadaye kutokana na kuahirishwa, na fainali ya Nations League 2021. Kwa ngazi ya vijana, timu za chini ya miaka 19 na chini ya miaka 17 za Hispania kila moja ilikuwa imefika angalau nusu fainali za Euro zao za mwisho mwaka 2019, huku mashindano ya vijana ya mwaka 2020 na 2021 yakifutwa kutokana na janga la COVID-19.
“Tulifikiri kwamba tulihitaji kufanya jambo. Nchi nyingine kama Ujerumani, Austria na Sweden zilikuwa zinaanzisha miradi mizuri yenye msingi imara na dira ya muda mrefu. “[Kabla] hakukuwa na mpango wa pamoja, dira ya pamoja au mkakati wa pamoja wa kuendesha mfumo wa akademi na kuimarisha maendeleo ya vipaji vijana [nchini Hispania],”anasema Florit.
NAMBA HAZIJIFICHI
Na ingawa huenda hali ilikuwa hivyo, kundi la wachezaji wa ndani katika La Liga tayari lilikuwa imara na bado liko hivyo. Huu ndio msingi wao wa kutisha katika soka la dunia. Katika misimu 10 kabla ya 2026/27, wastani wa idadi ya wachezaji wa Hispania waliocheza zaidi ya dakika 450, sawa na mechi tano kamili katika msimu mmoja ni 236.6, idadi inayozidi kwa mbali ligi nyingine kati ya tano bora Ulaya. Wanaofuata kwa ukaribu ni Waitaliano katika Serie A (152.2), wakifuatiwa na Wafaransa katika Ligue 1 (149.9), Wajerumani kwenye Bundesliga (142.6) na kisha Waingereza katika Ligi Kuu England (117.7). Tofauti ni kubwa sana.
Ingawa wakosoaji wanaweza kujiuliza kama takwimu za La Liga zimeongezwa na mkusanyiko mkubwa wa wachezaji wa ndani wanaocheza dakika za kutosha tu kufikia kiwango cha juu, lakini takwimu zinaonyesha hilo kwa uwazi.
Katika kipindi hicho hicho wachezaji wa Kihispania walichangia wastani wa asilimia 57.2 ya dakika zilizochezwa na wachezaji wote katika La Liga. Hiyo ikiwa juu tena, tofauti na ligi nyingine kubwa ni kubwa. Wachezaji wa England katika Ligi Kuu walichangia wastani wa asilimia 30.5 ya dakika zote kipindi hicho; dakika zilizochezwa na Wajerumani Bundesliga zilifikia asilimia 40.7; Waitaliano katika Serie A 36.8; na Wafaransa katika Ligue 1 asilimia 40.1.
Msimu huu, tofauti hiyo ni kubwa zaidi; wachezaji wa Kihispania wanachangia asilimia 58.9 ya dakika zilizochezwa katika La Liga. Hakuna hata moja kati ya ligi tano kubwa za Ulaya inayofikisha asilimia 40. Umuhimu wa takwimu hizo unaenda mbali zaidi.
“Timu ya taifa inanufaika wakati klabu hazifundishi tu wachezaji vijana, bali pia zinawaamini kwa kuwapa dakika halisi katika kiwango cha juu. Na katika suala hilo, tukizingatia hasa kuwapa dakika wachezaji wenye umri wa miaka 21 au chini, La Liga ina rekodi nzuri.”” anasema Florit.
Katika misimu 10 kabla ya 2026/27, ni Ligue 1 pekee (asilimia 8.2) iliyokuwa na wastani bora kuliko La Liga (asilimia 5.3) kwa uwiano wa dakika zilizochezwa na wachezaji wa ndani wenye umri wa miaka 21 au chini katika ligi tano kubwa za Ulaya. Hata hivyo, inapaswa pia kukumbukwa kwamba isipokuwa klabu moja zingine zote kutoka madaraja mawili ya juu Hispania zina timu za akiba, ambazo kimsingi ni timu za chini ya miaka 23 zinazocheza katika mfumo huo huo wa ligi na zinaweza kupanda hadi daraja la pili; baadhi ya klabu zina zaidi ya moja. Hivyo, hata kama hawachezi katika timu za wakubwa watakuwa wanacheza soka la wakubwa katika kiwango cha chini.
Katika mfumo huo, soka la Hispania siyo la kipekee katika suala hilo, kwani hali kama hiyo inapatikana pia Italia, Ujerumani na Ufaransa. Hata hivyo, Italia na Ujerumani, timu hizo zinaruhusiwa kucheza kuanzia daraja la tatu au chini; Ufaransa, nyingi zinaishia daraja la tano, huku klabu zenye akademi za “wasomi” pekee zikiruhusiwa kuingia daraja la nne.
Florit anaamini mfumo wa timu za “B” wa Hispania ni moja ya faida kubwa zaidi za kimuundo katika soka la Hispania.
“Hispania klabu 41 kati ya 42 za kulipwa zina timu ya akiba au timu inayohusishwa nayo inayoshiriki katika mfumo wa kawaida wa ligi za wakubwa. Hilo linawapa wachezaji vijana wenye umri wa miaka 17, 18, 19 na 20 daraja lenye changamoto kubwa kabla ya kufika katika soka la timu ya kwanza,” anasema Florit.
KWINGINEKO
Katika nchi nyingi za Ulaya ikiwamo England, kwa mfano, vijana wenye vipaji zaidi hutoka katika mfumo wa makundi ya umri mapema. Hata hivyo, wengi hucheza mara kwa mara soka la chini ya miaka 21 hadi wanapofikisha miaka ya mwanzo ya 20, jambo ambalo kwa wengi halionekani kuwa na manufaa.
Kufikia umri huohuo, wachezaji vijana wa Hispania wanaweza kuwa tayari wamecheza misimu kadhaa ya soka la mara kwa mara katika mazingira ya nusu-’profesheno’ au la kulipwa dhidi ya wapinzani wanaoendelea kukua pamoja na wale wenye uzoefu. Kuna dalili pia kwamba wachezaji wanaopanda kutoka timu za akiba wanafanya hivyo wakiwa wadogo zaidi Hispania.
Wastani wa umri wa wachezaji wa ndani waliocheza dakika 450 au zaidi katika La Liga msimu wa 2021/22 ulikuwa miaka 28 na siku 101, karibu mwaka mmoja zaidi ya wastani katika ligi nyingine kubwa. Msimu uliopita, wastani huo ulishuka hadi miaka 27 na siku 60, ukiwa mdogo kuliko Ligi Kuu England (miaka 27, siku 68) na Bundesliga (miaka 27, siku 79).
Takwimu zinaunga mkono kwa kiasi kikubwa hoja kwamba juhudi za Hispania za kukuza vijana ni nzuri na halisi. La Liga imeweka mkazo mkubwa katika uendelevu miaka ya karibuni, huku kuanzishwa kwa ukomo wa mishahara kwa kila klabu mwaka 2013 ukiwa na athari muhimu.
Ukomo wa mshahara wa kila klabu unatokana na tofauti kati ya mapato, matumizi na malipo ya madeni yanayotarajiwa katika kipindi cha msimu. Ingawa kitaalamu timu hujiwekea ukomo zenyewe, lazima uthibitishwe na chombo kinachosimamia kanuni za udhibiti wa uchumi wa La Liga.
Timu lazima ithibitishe kuwa inazingatia masharti kila inapomsajili mchezaji mpya na ikiwa haiwezi kufanya hivyo, mchezaji hawezi kusajiliwa hadi klabu irejee katika hali nzuri kifedha, jambo linalomzuia kucheza.
HATA HUKU UNAWABEBA
Wazo kwamba mfumo huo unahamasisha nidhamu ya kifedha na ushindani ni dhahiri. Ingawa mfumo unahusishwa zaidi na shughuli za usajili, kuna hoja kwamba unazihamasisha klabu kupata thamani zaidi kutoka katika akademi zao wenyewe.
Klabu zilizokumbwa na matatizo ya kifedha zina mahali pa kugeukia. Valencia, kwa mfano, imekuwa ikiwategemea wachezaji wake wa akiba katika miaka michache iliyopita; Sevilla, ambayo sasa imeanza misimu mitatu mfululizo ikiwa na ukomo wa chini zaidi wa mishahara La Liga imelazimika kujaza kikosi chake wachezaji vijana, na kadhaa kati yao wamekuwa muhimu.
Na kati ya Euro 41 milioni walizopata kutokana na mauzo ya wachezaji msimu huu, Euro 21 milioni zilitokana na bidhaa za akademi akiwamo Juanlu Sanchez (Euro 11 milioni kwenda Bournemouth) na Oso (Euro 10 milioni kwenda Strasbourg).
Inaelezwa kuwa kanuni hizo zinasababisha wachezaji kuuzwa kwa bei nafuu, na hilo linawahusu pia vijana wenye vipaji kutoka Hispania wanaoondoka kwenda klabu za nje, kama vipaji hivyo viwili vya Sevilla hapo juu. Ni wazi kwamba hapa kuna mkazo kwa klabu. Na linapokuja suala la kupima mafanikio, La Liga inaiona ngazi mbalimbali za timu za taifa kama kipimo muhimu.
Mwezi uliopita La Liga ilibainisha kwamba Hispania imeshinda mataji 23 katika ngazi za timu za taifa za wakubwa na vijana kwa wanaume na wanawake tangu akademi za vijana zilipoanza kukutana 2016, zaidi ya mara mbili ya nchi nyingine yoyote ya Ulaya, Ujerumani ikiwa na tisa, England saba na Ufaransa sita. Mafanikio makubwa hapa ni ushindi wa timu ya wanaume katika Kombe la Dunia 2026 na Euro 2024, pamoja na ushindi wa Hispania katika Kombe la Dunia la Wanawake 2023.