Klabu EPL zataka Manchester City iadhibiwe mapema
Muktasari:
- City bado inakabiliwa na madhara ya uamuzi wa kamati huru ya watu watatu iliyobaini kuwa klabu hiyo ilikiuka mashtaka yote yaliyokuwa ikikabiliwa nayo kuhusu kanuni za kifedha, huku pia ikibainika kuwa ilihusika katika mikataba ya kibiashara na mikataba ya wachezaji iliyodaiwa kuwa ya kughushi, yenye thamani ya karibu pauni bilioni moja.
LONDON, ENGLAND: WAKATI kesho Oktoba 2 ikiwa ni siku ya mwisho waliopewa Manchester City kuwakilisha utetezi wao wapinzani wake klabu za Ligi Kuu England (EPL), zinataka klabu hiyo ipewe adhabu kabla ya kumalizika kwa msimu huu, baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka kanuni za fedha.
City bado inakabiliwa na madhara ya uamuzi wa kamati huru ya watu watatu iliyobaini kuwa klabu hiyo ilikiuka mashtaka yote yaliyokuwa ikikabiliwa nayo kuhusu kanuni za kifedha, huku pia ikibainika kuwa ilihusika katika mikataba ya kibiashara na mikataba ya wachezaji iliyodaiwa kuwa ya kughushi, yenye thamani ya karibu pauni bilioni moja.
Hata hivyo, mabingwa hao wa England wameapa kuendelea na mapambano yao ya kisheria dhidi ya uamuzi huo, huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Ferran Soriano, akieleza Jumatatu kwamba mchakato huo bado unaweza kuchukua muda mrefu zaidi.
Lakini wakati adhabu ambayo haijawahi kutokea katika historia ya EPL, na ambayo inaweza kupelekea City kushushwa daraja, ikisubiriwa, klabu pinzani zimesema haziko tayari kuendelea kusubiri.
Klabu hizo zimeelekeza kwenye kanuni mpya zilizokubaliwa na timu za EPL katika mkutano wao wa Juni, ambazo ziliundwa kwa lengo la kuharakisha mchakato wa kushughulikia kesi za kinidhamu.
City imepewa hadi kesho Ijumaa kuwasilisha rufaa yake, lakini kwa kutumia utaratibu huo mpya wa haraka, mchakato wa rufaa unaweza kukamilika kabla ya Sikukuu ya Pasaka mwakani.
Mmoja wa viongozi wa klabu pinzani alisema: “Kwa upande wetu, kanuni mpya lazima zitumike.
“Tumekuwa tukisubiri kwa muda mrefu sana na sasa ni wakati wa jambo hili kumalizika.
“Mtazamo wa klabu nyingi ni kwamba haikubaliki kabisa, baada ya muda wote huu, mchakato huu kuendelea hadi kuvuka mwisho wa msimu.”
Kwa mujibu wa kanuni hizo mpya, kesi ya rufaa ya City inapaswa kukamilika ndani ya wiki 12, sawa na siku 84, tangu siku ambayo klabu itakapowasilisha rufaa.
Aidha, utaratibu wa kawaida unaelekeza kwamba usikilizwaji wa rufaa haupaswi kuzidi siku tano na unatakiwa kufanyika kwa mfululizo katika kipindi kimoja, badala ya kugawanywa katika vipindi tofauti.
Iwapo ratiba hiyo ingefuatwa kikamilifu, usikilizwaji wa kesi ungepaswa kukamilika ifikapo Desemba 25, huku ukianza Desemba 21.
Hata hivyo, kutokana na tarehe hiyo kuangukia Sikukuu ya Krismasi, tafsiri ya ratiba hiyo inaashiria kuwa usikilizwaji unaweza kuanza Desemba 14.
Baada ya hapo, kamati husika itakuwa na siku 30 kutoa uamuzi wake wa mwisho kuhusu rufaa hiyo.
Bado haijawa wazi iwapo uamuzi wa rufaa utakuwa mwanzo rasmi wa mchakato wa kutoa adhabu kwa City. Hata hivyo, iwapo rufaa yao itakataliwa, mchakato huo unaweza kuwa mfupi kwa sababu hoja za klabu hiyo za kupunguziwa adhabu huenda zisipate uzito mkubwa.
Baadhi ya klabu kubwa zinaamini kuwa mchakato wa kutoa adhabu unapaswa kuanza tayari, kwa kuzingatia uwezekano mkubwa wa City kukata rufaa dhidi ya adhabu yoyote itakayopewa.
Kwa mtazamo wao, kuendesha michakato hiyo miwili kwa wakati mmoja kunaweza kusaidia kuharakisha uamuzi wa mwisho.
Hata hivyo, bado haijathibitishwa iwapo kanuni hizo mpya zinaweza kutumika katika kesi ambayo usikilizwaji wake wa awali ulianza Septemba 2024.
Soriano ameshutumu mchakato huo akidai una kasoro, huku akisema kamati hiyo imekubali “nadharia za njama” za Ligi Kuu England.
Inatarajiwa mawakili wa City watapambana kwa nguvu kupinga hatua zinazofuata na huenda wakajaribu kurefusha zaidi mchakato huo.
Lakini presha kutoka kwa klabu pinzani imeongezeka zaidi, huku uongozi wa EPL, ukiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu Richard Masters, ukiwa hauna sababu kubwa ya kuipa City nafasi ya ziada kutokana na ukubwa wa juhudi ambazo klabu hiyo imekuwa ikifanya kupinga uchunguzi huo rasmi.
SITAKI CITY IUZWE
Meya wa zamani wa Greater Manchester, Andy Burnham amesema angekuwa na wasiwasi endapo wamiliki wa Manchester City wangeamua kuiuza klabu hiyo kufuatia uamuzi wa tume huru iliyobaini ukiukaji wa kanuni za kifedha za Ligi Kuu England.
Burnham alisema suala hilo bado linapingwa na Manchester City, huku akiwapongeza wamiliki wa klabu hiyo kwa uwekezaji walioufanya Manchester tangu walipoichukua mwaka 2008.
Wamiliki hao wanaongozwa na Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan, ambaye pia ni mmoja wa viongozi wakuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na mwanachama wa familia ya kifalme ya Abu Dhabi.
Tume huru iliyoundwa kushughulikia kesi hiyo ilibaini kuwa City ilikiuka sehemu kubwa ya kanuni za kifedha ilizotuhumiwa kuvunja. Klabu hiyo, hata hivyo, imekanusha makosa hayo na inatarajiwa kukata rufaa kabla ya muda wa mwisho wa Oktoba 2.
Wakati huohuo, Mdhibiti Huru wa Soka, taasisi iliyoanzishwa na Serikali ya Uingereza mwaka 2025, imesema kesi hiyo imeibua “masuala mazito”.
Mdhibiti huyo amesema anaweza kuchunguza hatua mbalimbali baada ya mchakato wa kinidhamu kukamilika, ikiwamo uwezekano wa kuangalia iwapo wamiliki wa City wataendelea kuwa na leseni ya kumiliki klabu.
Miongoni mwa mambo yaliyobainishwa na tume hiyo ni madai kwamba City iliingia mikataba iliyodaiwa kuwa ya “kughushi” na baadhi ya washirika wake wa kibiashara katika mpango wa kuficha ufadhili wa zaidi ya pauni milioni 830.
Ligi Kuu ilisema City “ilivunja kwa utaratibu kanuni zake kwa karibu muongo mmoja”.
Hata hivyo, adhabu ambayo klabu hiyo inaweza kupewa bado haijaamuliwa. Tume huru itaitisha kikao cha kuamua adhabu, mchakato ambao unaweza kuchukua miezi kadhaa kuanza.
Akizungumza na mhariri wa siasa wa BBC, Chris Mason, kuhusu uwezekano wa wamiliki wa City kuiuza klabu, Burnham alisema:“Ningekuwa na wasiwasi mkubwa kuwapoteza.
“Wamekuwa mshirika mkubwa katika kujenga Manchester ya kisasa na, bila shaka, katika kuijenga Manchester City kuwa nguvu ya kimataifa ilivyo sasa.”
Burnham, ambaye alikuwa meya wa Greater Manchester hadi Juni, alisema anaishukuru City Football Group na wamiliki wake kwa uwekezaji ambao haukuishia kwenye Uwanja wa Etihad na eneo la mafunzo pekee, bali pia katika jiji la Manchester.
Alisema pia ana imani kwamba mawasiliano na uhusiano aliokuwa nao na wamiliki wa City wakati akiwa meya wa Greater Manchester vinaweza kuchunguzwa bila kumweka katika mazingira ya kujitetea.
Kauli ya Burnham imekuja wakati kukiwa na mjadala mkubwa katika soka England kuhusu ukubwa wa tuhuma na matokeo ya tume huru.
Burnham alitoa kauli hizo akiwa Uwanja wa Hill Dickinson, nyumbani kwa Everton, klabu anayoishabikia.
Everton yenyewe iliwahi kukumbana na matatizo ya kanuni za kifedha za Ligi Kuu, ikitozwa adhabu ya kukatwa pointi 10 Novemba 2023 kutokana na ukiukaji uliotajwa kuwa mdogo zaidi. Adhabu hiyo ilipunguzwa hadi pointi sita baada ya rufaa.
Burnham alisema aliiunga mkono Everton katika kipindi hicho kwa sababu bado anaamini klabu hiyo haikutendewa kwa haki katika mchakato huo.