Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fainali Kagame Cup... Ngoja tuone 

Muktasari:

  • Kocha wa Gor Mahia FC ya Kenya, Charles Kwablan Akonnor, amesema timu yake imefika hatua hiyo kwa sababu ina uwezo wa kupambana katika mazingira magumu na sasa imebaki hatua moja kutimiza lengo la kutwaa ubingwa.

IKIWA zimesalia saa chache kabla ya mechi ya fainali ya Kombe la CECAFA Kagame 2026 kupigwa hapo kesho, Ijumaa kwenye Uwanja wa Amahoro kati ya Gor Mahia dhidi ya Rayon Sports , vita ya maneno imeibuka  Kigali kwa makocha wa timu hizo wakionyesha kuutolea  macho ubingwa huo.

Kocha wa Gor Mahia FC ya Kenya, Charles Kwablan Akonnor, amesema timu yake imefika hatua hiyo kwa sababu ina uwezo wa kupambana katika mazingira magumu na sasa imebaki hatua moja kutimiza lengo la kutwaa ubingwa.

Kwa upande wake, kocha wa Rayon Sports FC ya Rwanda, Harringingo Francis Christian, amesema hawana mpango wa kuishia kwenye fainali pekee, bali wanataka kuhakikisha kombe linabaki Kigali mbele ya mashabiki wao.

Fainali hiyo ambayo itachezwa saa 1: 00 usiku kwa Afrika ya Kati huku ikiwa saa 2:00 usiku kwa Mashariki itawakutanisha mabingwa wa  zamani wa mashindano haya, Gor Mahia  dhidi ya wenyeji Rayon Sports katika mchezo unaotarajiwa kuvuta hisia za wengi hapa Kigali.

Mechi hiyo itapigwa baada ya Al Hilal ya Sudan kucheza dhidi ya Jamus katika kupigania nafasi ya mshindani wa tatu kwenye uwanja huohuo wa Amahoro.


MKWARA WA GOR MAHIA

Akizungumza na Mwanaspoti hapa Kigali,  kocha wa Gor Mahia, Charles Kwablan Akonnor, alisema wachezaji wake wameonyesha tabia ya mabingwa na sasa wanataka kumaliza kazi.

Gor Mahia ilitinga fainali baada ya mchezo mkali dhidi ya Al Hilal uliomalizika kwa sare ya  bao 1-1 ndani ya dakika 120 kabla ya Wakenya hao kushinda kwa mikwaju ya penalti 8-7 huku wakiwa pungufu.

Akonnor alisema ushindi huo umeonyesha uwezo wa timu yake kuvumilia presha na kupambana hadi dakika ya mwisho.

“Nawashukuru wachezaji wangu kwa kucheza kwa moyo wote na kupata ushindi dhidi ya timu imara kama Al Hilal, walipambana sana na walistahili kufika hatua hii,” alisema Akonnor.

Kocha huyo alisema  pamoja na kuheshimu ubora wa Rayon Sports, hawajaingia fainali kwa bahati bali wamefanya kazi kubwa kufika hapo.

“Tumefanya kazi kubwa kufika hapa, lakini bado hatujamaliza kazi, fainali itakuwa ngumu kwa sababu tunakutana na timu nzuri yenye mashabiki wengi, tunapaswa kuwa tayari kila upande,” alisema.

Akonnor anaamini uzoefu wa Gor Mahia kwenye mashindano ya kikanda unaweza kuwa silaha yao kubwa katika mchezo huo.

“Tunaiheshimu Rayon Sports. Ni timu nzuri na imefanya vizuri hadi kufika fainali, lakini sisi pia tuna malengo yetu. Tutaingia uwanjani kupambana kutafuta ushindi,” aliongeza.


RAYON WANATAKA HISTORIA

Kwa upande mwingine, kocha wa Rayon Sports, Harringingo Francis Christian, amesema kufika fainali mbele ya mashabiki wao ni hatua nzuri, lakini lengo lao kubwa ni kumaliza kazi kwa kutwaa ubingwa.

Rayon Sports imekuwa moja ya timu zilizofanya vizuri zaidi kwenye mashindano haya, ikishinda mechi zake zote nne kabla ya kufika fainali.

Katika nusu fainali, Rayon Sports iliiondoa Jamus SC ya Sudan Kusini kwa ushindi wa mabao 3-1.

Harringingo alisema mafanikio hayo yameongeza kujiamini kwa kikosi chake kuelekea pambano la mwisho.

“Nina furaha kwa sababu tumeshinda mechi zote nne tulizocheza kwenye mashindano haya. Hii pia ni maandalizi mazuri kuelekea msimu mpya,” alisema.

Hata hivyo, kocha huyo alisema hawajaridhika kwa kufika fainali pekee na sasa wanataka hatua kubwa zaidi.

“Baada ya kufika hatua hii tunataka zaidi. Tunataka kushinda kombe. Tunajua fainali itakuwa ngumu, lakini tuko tayari kupambana,” alisema.


NJIA ZAO FAINALI

Gor Mahia ambayo ilikuwa kundi A, ilianza mashindano hayo kwa kishindo kufuatia kuichapa APR ya Rwanda mabao 5-0 kisha ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Vipers.

Baada ya kupoteza dhidi ya mabingwa hao wa Uganda, Gor Mahia ilijibu mapigo kwa kuichapa Garde Republicaine ya Djibouti bao 1-0 na kutinga nusu fainali kabla ya kukutana na Al Hilal.

Gor Mahia ilikuwa na pointi sita  sawa na Vipers lakini ilibebwa na wastani mzuri wa mabao hivyo wakasonga mbele.

Rayon Sports iliyokuwa kundi C yenyewe ilitinga kwa kishindo hatua na nusu fainali kufuatia kushinda mechi zake zote za hatua ya makundi.

Walianza kwa kuichapa KVZ ya Zanzibar kwa mabao 2-0, Tusker na Al Hilal bao 1-0 katika kila mchezo hivyo kumaliza kinara wa kundi hilo ikiwa na pointi tisa kabla ya kuichapa Jamus na kutinga fainali.

Mbali na historia na heshima ya ubingwa, timu hizo mbili ambazo zimetinga fainali ya michuano hiyo  pia zinawania zawadi ya fedha.

Mshindi wa CECAFA Kagame Cup 2026 ataondoka na dola 30,000 za Marekani, huku mshindi wa pili akipata dola 20,000.