Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa jela… Hawa jamaa na soka basi tena

JELA Pict

Muktasari:

  • Hata hivyo, umaarufu mkubwa unakuja na changamoto zake na baadhi yao wamejikuta wakiteleza na kuingia katika matatizo ya kisheria, hali iliyosababisha kwenda jela na maisha yao ya soka kuharibika kabisa.

LONDON, ENGLAND: KATIKA ulimwengu wa michezo, wachezaji huchukuliwa kama kioo cha jamii, watu wa kuigwa na mashujaa kwa wale wanaowashabikia.

Hata hivyo, umaarufu mkubwa unakuja na changamoto zake na baadhi yao wamejikuta wakiteleza na kuingia katika matatizo ya kisheria, hali iliyosababisha kwenda jela na maisha yao ya soka kuharibika kabisa.

Baada ya kwenda jela, baadhi yao walishindwa kabisa kurejea na wengine walirejea uwanjani lakini walishindwa kurudisha viwango vyao vya awali.

Hapa tumekuletea wachezaji wanane waliowahi kufungwa jela na maisha yao ya soka yakaingia doa.

JE 08

8. Rene Higuita

Rene Higuita, maarufu kwa 'Scorpion Kick', alikuwa mmoja wa makipa wa kipekee duniani. Lakini mwaka 1993 alikamatwa kwa kuhusika kuwa kama mpatanishi wa mateka, jambo ambalo halikuruhusiwa kisheria Colombia.

Alikaa jela kwa zaidi ya miezi saba na baadae alirudi kucheza, lakini kiwango chake kilishuka na hakuweza kufanya yale aliyokuwa akifanya hapo awali.

Baada ya kurejea pia alikumbwa na hatia nyingine ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya na akapelekwa tena jela kabla ya kuachiwa.

JE 07

7. Tony Adams

Adams alikuwa nahodha wa Arsenal na timu ya taifa ya England, lakini maisha yake binafsi yalikuwa yakivurugwa na uraibu wa pombe. Mwaka 1990, alifungwa wiki nne jela kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa. Alikiri alihitaji msaada mkubwa, ili kuondokana na tatizo hilo, akasaidiwa  na baadaye akawa mmoja wa wanamichezo waliofanya vizuri, ingawa sio kwa kiwango kikubwa.

Tofauti na mastaa wengine, Adams alirejea kwenye soka na hata akaja kuanzisha taasisi ya kusaidia wanamichezo wanaopambana na uraibu wa pombe na dawa za kulevya.

JE 06

6. Marlon King

Marlon King alichezea klabu mbalimbali England kama Watford, Birmingham City na Gillingham. Hata hivyo, maisha yake ya nje ya uwanja yalikuwa na misukosuko. Alifungwa mara kadhaa kwa makosa ya kushambulia wanawake na kuiba.

Mwaka 2009 alihukumiwa kifungo cha miezi 18 kwa kosa la kumpiga mwanamke aliyemkataa klabuni. Ingawa alijaribu kurejea, jamii na klabu zilimkataa kwa sababu ya tabia za unyanyasaji wa kijinsia. Hatimaye aliamua kustaafu soka.

JE 05

5. Ched Evans

Evans alikuwa mshambuliaji mwenye kipaji aliyekuwa aking’ara akiwa na Sheffield United. Mwaka 2012, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kosa la unyanyasaji wa kijinsia, lakini miaka miwili baadaye aliachiwa baada ya kukata rufaa.

Hata hivyo, kesi hiyo iliharibu kabisa jina lake na alikumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa timu na mashabiki pale alipojaribu kutaka kurejea kiwanjani.

Klabu nyingi zilikataa kumsajili baada ya kutoka jela na baada ya hapo akaamua kustaafu.

JE 04

4. Benjamin Mendy

Beki huyu wa zamani Manchester City na timu ya taifa ya Ufaransa ambayo aliisaidia kuchukua ubingwa wa Kombe la Dunia 2018, alikumbwa na tuhuma nzito za ubakaji na unyanyasaji wa kingono kutoka kwa wanawake kadhaa.

Alikaa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja akisubiri kesi, lakini baadaye aliachiliwa na kusafishwa na mahakama, ingawa muda alioupoteza gerezani ulikuwa mwingi mno.

Manchester City ilivunja mkataba naye na hadhi yake kama mchezaji wa kiwango cha juu iliporomoka. Hata baada ya kutoka jela, hakuna timu kubwa iliyomhitaji na akajiunga na FC Lorient iliyokuwa ikicheza Ligi Daraja la Kwanza Ufaransa na baada ya hapo mapema mwaka huu alitimkia FC Zurich ya Switzerland.

JE 03

3. Joey Barton

Barton alikuwa kiungo mkabaji mwenye vipaji, lakini mtukutu. Mwaka 2008, alihukumiwa kifungo cha miezi sita baada ya kushambulia watu wawili mitaani wakati akiwa amelewa.

Kesi hiyo ilikuwa mwendelezo tu wa maisha yake ya vurugu na matumizi ya pombe kupindukia. Licha ya kurudi uwanjani na kuchezea timu kama Newcastle na QPR, haikuchukua muda kabla ya matatizo kumrudia. Alipostaafu na kuwa kocha, alikumbana tena na marufuku ya mwaka mmoja baada ya kukutwa amecheza kamari. Taaluma yake iligubikwa na utovu wa nidhamu.

JE 02

2. Adam Johnson

Johnson aliwahi kuwa moja ya wachezaji waliotarajiwa kung’ara zaidi England. Alikuwa amechezea timu kubwa kama Manchester City na Sunderland, pia aliwahi kuitwa timu ya taifa ya England.

Hata hivyo, mwaka 2016, Johnson alihukumiwa kifungo cha miaka sita baada ya kupatikana na hatia ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana mwenye umri wa miaka 15.

Aliachiwa kwa msamaha baada ya kutumikia miaka mitatu, lakini maisha yake ya soka yalikuwa yamekwisha kabisa. Timu zilimkataa, jamii ilimkataa na jina lake lilibakia kuwa doa katika historia ya soka la England. Wakati anahukumiwa kwenda jela alikuwa na umri wa miaka 27 tu.

JE 01

1. Bruno Fernandes de Souza

Bruno alikuwa kipa mahiri wa klabu ya Flamengo na alikuwa na kila dalili ya kuwa mmoja wa makipa wakubwa Brazil. Mwaka 2010, alikamatwa kwa tuhuma za kupanga mauaji ya mpenzi wake, Eliza Samudio, ambaye baada ya kumuua aliuficha mwili wake.

Kesi hiyo ya kushtusha ilitingisha si tu soka la Brazil, bali dunia nzima. Bruno alihukumiwa kifungo cha miaka 22 jela.

Licha ya kupewa nafasi ya kurudi uwanjani kwa muda mfupi baada ya kutumikia sehemu ya kifungo chake, upinzani mkubwa wa umma na mashinikizo kwa timu nyingine, ilimlazimu kustaafu kabisa. Hadi leo hii inabaki kuwa mojawapo ya kesi mbaya zaidi zinazomhusu mchezaji wa soka.