KIKAO KIZITO! Bosi akutana na Amorim
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa, Amorim yuko chini ya shinikizo kubwa katika benchi la Man United baada ya timu yake kushinda mechi moja tu kati ya tano za mwanzo za msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND: BOSI wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe, aliruka kwa helikopta kwenda jijini Manchester ili kufanya mazungumzo na Ruben Amorim kufuatia mwanzo mbaya wa msimu wa klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa, Amorim yuko chini ya shinikizo kubwa katika benchi la Man United baada ya timu yake kushinda mechi moja tu kati ya tano za mwanzo za msimu huu.
Kwa mujibu wa gazeti la The Athletic, bosi huyo mmiliki wa kampuni ya Ineos, alitua kwa helikopta katika kituo cha mazoezi cha Carrington kwa ajili ya kufanya mikutano kadhaa, ukiwamo mmoja na Amorim.
Inadaiwa kuwa kikao hicho kilikuwa kimepangwa muda mrefu na Ratcliffe, lakini hali ya kutoridhisha ya timu kwa sasa ndiyo ilikuwa mada kuu iliyojadiliwa baina ya wawili hao.
Katika mechi tano tu za msimu huu, Man United tayari imepata kipigo cha fedheha kutoka kwa timu ya Ligi Daraja la Pili (League Two) Grimsby, kupoteza mbele ya Arsenal na Man City na kulazimika kupata penalti ya dakika ya 97 ili kuibuka na ushindi dhidi ya Burnley waliotabiriwa kushuka daraja tangu kuanza kwa msimu huu.
Tangu awe kocha wa Man United, Amorim ameandika rekodi mbaya zaidi kwa kupoteza mechi nyingi kuliko kocha yeyote katika kipindi cha miaka 80 iliyopita.
Amorim ameshinda asilimia 36.2 tu ya mechi zake akiwa kocha wa United.
Makocha waliopita kuanzia kwa Erik ten Hag alifutwa kazi akiwa na asilimia 54.7 ya ushindi katika muda wake aliokuwa kocha wa timu hiyo.
David Moyes, ambaye alitimuliwa msimu wake wa kwanza, alipata ushindi asilimia 52.9 ya mechi zote.
Tangu afike Manchester Novemba mwaka jana, Man United ya Amorim ndiyo timu yenye rekodi mbaya zaidi kati ya klabu zote za Ligi Kuu England ambazo zimebaki katika ligi msimu huu.
Kati ya klabu 17 zilizopo kila msimu bila kushushwa daraja wala kupandishwa, Manchester United ndio timu inayoongoza kufanya vibaya kuliko nyingine.
Imekusanya alama 31 tu katika mechi 31, ikishinda mechi nane tu.
Mambo hayajaonyesha kuanza kubadilika msimu huu pia, kwani Man United imekusanya pointi nne pekee katika michezo minne ya mwanzo ya Ligi Kuu England ambayo ni rekodi yao mbaya zaidi tangu kuanza kwa mfumo mpya wa ligi msimu wa 1992-93.
Hata hivyo, Amorim amebaki imara katika falsafa yake, akisisitiza kwamba ni bora afukuzwe kazi kuliko kubadilisha mfumo wake.
Akizungumza baada ya kipigo cha 3-0 kutoka kwa Manchester City Jumapili ya wiki iliyopita, Amorim alisema: "Hii si rekodi ambayo tunapaswa kuwa nayo Manchester United. Nakubali, lakini sitabadilisha.
"Tutakuwa tunazungumza kuhusu hili kila mechi tunayopoteza. Nimecheza kwa mtindo wangu na nitaendelea kucheza kwa mtindo wangu hadi pale nitakapohitaji kubadilisha mwenyewe nitakapoona inafaa."
Hadi sasa, Sir Jim Ratcliffe amebaki na msimamo wa kumuunga mkono Amorim na Machi mwaka huu alisema hadharani kwamba anamkubali sana kocha huyo Mreno.