Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya nani bingwa, Morocco au Senegal kusikilizwa Oktoba 8

Muktasari:

  • Hatma ya ubingwa wa AFCON 2025 kati ya Morocco na Senegal inaingia hatua nyingine Oktoba 8, 2026, wakati CAS itakaposikiliza rufaa ya Senegal dhidi ya CAF na Morocco. Hata hivyo, uamuzi wa mwisho hautatolewa siku hiyo.

Lausanne, Uswisi. Hatma ya ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kati ya Morocco na Senegal itaingia hatua nyingine Oktoba 8, 2026, wakati Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) itakaposikiliza rufaa ya Shirikisho la Soka la Senegal (FSF) dhidi ya CAF na Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF).

Usikilizwaji huo utafanyika katika makao makuu ya CAS jijini Lausanne kuanzia saa 3:30 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki na utafanyika bila uwepo wa vyombo vya habari ndani ya ukumbi.

Hata hivyo, licha ya kesi hiyo kusikilizwa Oktoba 8, CAS haitatoa uamuzi siku hiyo, hivyo suala la nani atatambuliwa rasmi kuwa bingwa wa AFCON 2025 litaendelea kusubiri hukumu ya baadaye.

Mgogoro huo ulianza katika fainali ya AFCON 2025 iliyochezwa Januari 18, 2026 jijini Rabat, Morocco.

Senegal ilishinda mchezo huo kwa bao 1-0 baada ya muda wa ziada na kwa matokeo ya uwanjani ikaonekana imefanikiwa kutwaa ubingwa.

Hata hivyo, fainali hiyo iligubikwa na mvutano baada ya wachezaji wa Senegal kutoka nje ya uwanja kwa muda wakipinga uamuzi wa mwamuzi wa kutoa penalti kwa Morocco.

Baada ya tukio hilo, suala hilo lilipelekwa kwenye vyombo vya nidhamu vya CAF.

Machi 17, 2026, Bodi ya Rufaa ya CAF ilifanya uamuzi uliobadilisha matokeo ya fainali hiyo.

CAF iliipa Morocco ushindi wa mabao 3-0 baada ya kuikuta Senegal na hatia ya kugomea mchezo.

Uamuzi huo uliifanya Morocco kutambuliwa na CAF kama bingwa wa AFCON 2025.

Senegal ilipinga uamuzi huo na kupeleka kesi CAS, ikitaka uamuzi wa CAF ubatilishwe na matokeo ya uwanjani yabakie kama yalivyo.

CAS ilithibitisha kupokea rufaa hiyo, huku Morocco na CAF wakiwa sehemu ya mchakato huo wa kisheria.

Baada ya maandalizi ya kesi hiyo, CAS ikapanga Oktoba 8, 2026 kuwa tarehe ya kusikiliza hoja za pande zote.

Wawakilishi wa Senegal na Morocco wanatarajiwa kuhudhuria usikilizwaji huo na CAF itawakilishwa na mawakili wake.

Jopo litakalosikiliza kesi hiyo linaongozwa na Profesa Gérald Simon wa Ufaransa, likiwa na Profesa Luigi Fumagalli wa Italia na Profesa Dk Ulrich Haas wa Ujerumani.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, jopo litaendelea na mashauriano kabla ya kutoa uamuzi. CAS haijaweka wazi tarehe ya kutangaza hukumu hiyo.

Kwa hiyo, Oktoba 8 haitakuwa siku ya kujulikana rasmi bingwa mpya wa AFCON 2025, bali ni siku ambayo CAS itasikiliza kwa kina rufaa ya Senegal.

Hadi hukumu itakapotolewa, mgogoro unabaki ukiwa na kumbukumbu mbili tofauti.

Senegal ikiwa mshindi wa fainali kwa matokeo ya uwanjani, huku Morocco ikiwa bingwa kwa mujibu wa kanuni na uamuzi wa CAF.

Sasa macho ya soka la Afrika yanaelekezwa Lausanne kusubiri uamuzi wa mwisho wa CAS kuhusu nani atakayebaki kwenye rekodi rasmi kama bingwa wa AFCON 2025.