Kanuni mpya EPL zaanza kupunguza upotezaji muda uwanjani
Muktasari:
- Soka hufuata mazoea fulani na mojawapo iliyokera zaidi katika miaka ya karibuni ilikuwa ongezeko linaloonekana la upotezaji muda, huku wachezaji wakibuni njia mpya za kutumia muda, wakizitesa subira za waamuzi na mashabiki kwa kuvuruga kasi ya mpinzani au kuhakikisha muda mfupi iwezekanavyo unatumika kucheza soka katika jitihada za kulinda matokeo.
LONDON, ENGLAND: Kanuni mpya zilianzishwa msimu huu kwa lengo la kuharakisha uanzishaji wa mchezo katika Ligi Kuu England. Je, zinafanya kazi? Baada ya siku tano za mechi za msimu wa 2026/27 ukweli bado uko mbali, lakini wakati mwingine zinaweza kubadilisha mambo na kuwa bora.
Soka hufuata mazoea fulani na mojawapo iliyokera zaidi katika miaka ya karibuni ilikuwa ongezeko linaloonekana la upotezaji muda, huku wachezaji wakibuni njia mpya za kutumia muda, wakizitesa subira za waamuzi na mashabiki kwa kuvuruga kasi ya mpinzani au kuhakikisha muda mfupi iwezekanavyo unatumika kucheza soka katika jitihada za kulinda matokeo.
Shirikisho la Kimataifa la Bodi za Vyama vya Soka (IFAB), taasisi inayosimamia sheria za mchezo, iliamua kuwa imetosha, na ikatumia Kombe la Dunia 2026 kutoa maelekezo yaliyolenga kupunguza fursa ambazo wachezaji wangekuwa nazo za kupoteza muda wakati wa mchezo.
Hilo lilijumuisha kanuni ya sekunde tano kwa mipira ya kurusha na mipira ya kuanzisha mchezo kutoka langoni. Siyo kwamba mchezaji ana muda halisi wa sekunde tano wa kuutekeleza, bali kuanzia pale mwamuzi anapohisi muda unachezewa anaweza kuanza kuhesabu kwa kuinua mkono juu.
Pia kulikuwa na kanuni mpya kuhusu mabadiliko ya wachezaji, ambapo ikiwa mchezaji anatumia zaidi ya sekunde 10 kutoka uwanjani, basi anayeingia kuchukua nafasi yake lazima asubiri sekunde nyingine 60 kabla ya kuruhusiwa.
Inaonekana pia kuwa kanuni hiyo ilikuwa na athari. Muda wa wastani uliotumika kwenye mipira ya kuanzisha mchezo kutoka langoni na mipira ya kurusha ulipungua, kutoka sekunde 27.7 na 15.7 mtawalia katika Kombe la Dunia 2022 hadi sekunde 23.7 na 13.2. Hata hivyo, muda wa wastani wa kusimama mchezo kutokana na mabadiliko ya wachezaji haukubadilika sana kutoka sekunde 65.6 mwaka 2022 hadi 65.5 mwaka huu.
Katika Kombe la Dunia 2026 kulikuwa na matukio manne mpira wa kuanzisha mchezo kutoka langoni uligeuzwa kuwa kona baada ya kuchukua muda mrefu, huku mipira 12 ya kurusha ikitolewa kwa wapinzani kwa sababu hiyo hiyo. Pia kulikuwa na tukio moja la mchezaji wa akiba kulazimika kusubiri sekunde 60 kabla ya kuingia uwanjani. Kwa hiyo, kwa kiasi kikubwa maonyo yalizingatiwa au sheria hazikutekelezwa ipasavyo.
Kwa vyovyote vile, sheria hizo mpya kwa ujumla zilionekana kuwa zimefanikiwa, na Ligi Kuu England ikaamua kuzibeba kuanzia msimu huu.
MECHI TANO EPL
Katika siku ya tano tu ya mechi ambapo michezo 50 imeshachezwa na kutokana na mapumziko marefu ya mechi za kimataifa ni wakati mwafaka wa kuangalia athari ambazo kanuni hizo mpya zimeanza kuwa nazo katika Ligi Kuu England ambayo ni mashindano pendwa ya soka duniani.
Hadi sasa bado haujaonekana mpira wa kuanzisha mchezo kutoka langoni ukigeuzwa kuwa kona, lakini tukio lililokaribia zaidi ni kipa kushikilia mpira kwa muda mrefu wakati mchezo ukiendelea, jambo ambalo pia husababisha kutolewa kwa kona. Hilo lilitokea katika mchezo wa Leeds United dhidi ya Crystal Palace wakati mwamuzi Adam Herczeg, aliyekuwa akichezesha mchezo wake wa kwanza wa ligi hiyo aliamua kipa wa Palace, Walter Benitez, alikuwa ameushikilia kwa zaidi ya sekunde nane zilizoruhusiwa. Hata hivyo, kanuni hiyo ilianzishwa msimu uliopita, na wakati huo ilitekelezwa mara nyingine nane.
Pia, kumekuwapo na tukio moja tu msimu huu ambapo mchezaji aliyeingia uwanjani kama mbadala alilazimika kusubiri sekunde 60 kutokana na aliyekuwa anatoka uwanjani kuchelewa, na hilo pia lilihusisha Crystal Palace.
Katika kipigo cha nyumbani cha mabao 4-1 dhidi ya Manchester City mwishoni mwa Agosti, Anan Khalaili aliamuliwa kuwa ametumia muda mwingi kutoka uwanjani, hivyo Oscar Mingueza alilazimika kusubiri dakika nzima kabla ya kuingia. Ilionekana kama adhabu kali kidogo kwa Palace, ikizingatiwa walikuwa nyuma kwa mabao 3-1 wakati huo, lakini sheria ni sheria.
Kumekuwa na matukio manne ya mchezaji kuadhibiwa kwa kuchukua muda mrefu katika kurusha mpira na kumpa mpira mpinzani; Jorrel Hato wa Chelsea dhidi ya Fulham, Neco Williams wa Nottingham Forest dhidi ya Aston Villa, Riccardo Calafiori wa Arsenal dhidi ya Sunderland, na Olivier Boscagli wa Brighton dhidi ya Arsenal.
Hilo halionekani kuwa jambo kubwa sana katika michezo 50, hivyo je, kanuni hizo kweli zina athari katika kupunguza upotezaji muda? Opta imefanya tathmini kupitia takwimu za muda ambao mpira umekuwa ukichezwa uwanjani katika Ligi Kuu England tangu mwanzo wa msimu wa 2015/16, na imebaini kwa usahihi kiasi cha soka kilichochezwa, pamoja na muda ambao matukio mbalimbali huchukua kwa wastani.
REKODI HIZI HAPA
Baada ya siku ya tano ya mechi, wastani wa muda ambao mpira umekuwa ukichezwa katika michezo ya Ligi Kuu England msimu huu ni asilimia 57.7. Huo ni wastani wa juu zaidi tangu msimu wa 2020/21, ambao ulikuwa asilimia 58.0. Kwa upande wa jumla ya muda ambao mpira umekuwa ukichezwa kumekuwapo na dakika 56 na sekunde 35 za mchezo ukiendelea katika kila mechi msimu huu ambao ni wastani wa tatu wa juu kuwahi kurekodiwa baada ya msimu wa 2023/24 dakika 58:11 na 2024/25 zilipocheza 56:59. Msimu uliopita ilikuwa dakika 55 na sekunde 23 pekee, hivyo kwa sasa kuna zaidi ya dakika moja ya soka kwa kila mchezo.
Cha kufurahisha ni kwamba, inaonekana pia kuna athari katika muda wa nyongeza. Kwa wastani kuna dakika nane na sekunde nne za muda wa nyongeza kwa kila mchezo msimu huu, ambao ni wastani wa chini zaidi tangu 2021/22, ambapo ulikuwa dakika 7 na sekunde 29. Kwa upande wa wastani wa muda unaotumika kuanzisha tena mchezo, inaonekana umepungua kwa ujumla, jambo linaloashiria kuwa kanuni mpya kweli zina athari. Kwa mipira ya kurusha inachukua wastani wa sekunde 15.3 kurushwa, ikiwa ni zaidi ya sekunde mbili chini kwa kila mpira ukilinganisha na msimu uliopita ambapo ilikuwa 17.8. Huo ni wastani wa chini zaidi uliowahi kurekodiwa tangu 2016/17 ambapo ulikuwa sekunde 15.2, na inaonyesha kuna anguko kubwa ikilinganishwa na msimu uliopita.
Huenda hilo lisionekane kuwa jambo kubwa, lakini ukizingatia idadi ya mipira ya kurusha inayopigwa, ikiwa kasi hiyo itaendelea na idadi ya mipira ya kurusha ikawa sawa na msimu uliopita ambapo ilikuwa 13,615, hilo litamaanisha zaidi ya saa tisa na nusu za kusubiri mipira irushwe zingeokolewa katika msimu mzima. Kwa kila mchezo, ni karibu dakika moja na nusu sawa na sekunde 88.5 zilizookolewa.
Mipira ya kuanzisha mchezo kutoka langoni pia ina kasi zaidi. Kwa sekunde 27.7 kwa kila mpira msimu huu, huo ni wastani wa chini zaidi kuwahi kurekodiwa. Msimu uliopita ulikuwa mara ya kwanza ambapo wastani wa muda wa kuanzisha mchezo kutoka langoni ulivuka sekunde 30, ukiwa sekunde 30.4, lakini umepungua kwa karibu sekunde tatu kwa kila mpira wa kuanzisha mchezo kutoka langoni msimu huu.
Kwa ujumla, mipira 5,901 ya kuanzisha mchezo kutoka langoni ilipigwa msimu uliopita, hivyo tena, ikiwa kutakuwa na idadi hiyo hiyo ms imu huu, uokoaji wa sekunde 2.7 kwa kila mpira unaweza kumaanisha zaidi ya saa nne na dakika 40 za muda kuokolewa katika msimu mzima. Kwa kila mchezo, ni karibu sekunde 42 zilizookolewa.
Kwa upande wa mabadiliko ya wachezaji, kuna takwimu zinazorudi hadi mwanzo wa msimu wa 2020/21 pekee, lakini hata huko kumekuwa na upungufu. Kumepimwa kwa kusimama kwa mchezo kunakotokana na mabadiliko ya wachezaji badala ya kila mabadiliko ya mchezaji mmoja mmoja kwa sababu makocha mara nyingi hufanya mabadiliko ya wachezaji zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.
Msimu uliopita, kila kusimama kwa mchezo kutokana na mabadiliko ya wachezaji kulichukua wastani wa sekunde 76.1. Hadi sasa msimu huu, muda huo umeshuka hadi sekunde 64.3. Huo ni muda wa chini zaidi tangu 2021/22, ambapo ulikuwa sekunde 63.4, ingawa kuanzishwa kwa mfumo wa kubadilisha wachezaji watano msimu wa 2022/23 bila shaka kulichangia kuongezeka kwa muda huo katika miaka ya karibuni. Inafurahisha kuona kwamba kwa sasa umeshuka tena hadi viwango vilivyokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa mabadiliko ya wachezaji watano.
Jambo jingine lililojitokeza ni kwamba ucheleweshaji mwingine pia umepungua katika wiki za mwanzo za msimu huu, licha ya kutokuwapo na kanuni mpya maalumu za kufanya hivyo. Muda wa wastani wa kupiga kona ulikuwa ukiongezeka katika misimu miwili iliyopita, hasa kutokana na msisitizo mkubwa wa makocha wa mipira iliyokufa na mipango iliyofanyiwa mazoezi kwa umakini, lakini sasa umeshuka kutoka sekunde 36.1 msimu uliopita hadi sekunde 33.9 msimu huu, ambao ni muda wa chini zaidi tangu msimu wa 2023/24.
Mipira ya adhabu inapigwa baada ya wastani wa sekunde 33.3, ambao ni muda wa chini zaidi tangu 2020/21, wakati mipira ya adhabu ya moja kwa moja inachukua sekunde 74.5 kupigwa, ikiwa ni wastani wa chini zaidi tangu 2021/22 na zaidi ya sekunde 11 chini ya msimu uliopita.
Cha kufurahisha ni kwamba, penalti pia zinapigwa kwa kasi zaidi. Hali hiyo inaweza kubadilika kadiri wiki na miezi inavyokwenda, lakini hadi sasa kumekuwapo na penalti tisa pekee zilizopigwa Ligi Kuu England msimu huu , ingawa kwa sasa wastani wa muda wa kusubiri kabla ya penalti kupigwa ni sekunde 117.4 ambao ni muda wa chini zaidi tangu 2021/22 na karibu sekunde 47 chini ya msimu uliopita, ambapo ulikuwa sekunde 164.7. Hata hivyo, uhakiki mara chache tu mrefu wa VAR unaweza kuufanya muda huo uanze tena kuongezeka.
Kwa ujumla bado ni mapema, lakini kwa wenzetu maelekezo mapya ya kupambana na upotezaji muda yanaonekana kuwa na athari.