Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KAMA ZARI: Senesi kutoka fukwe za Ibiza hadi Kombe la Dunia

KANSAS CITY, CANADA. WAKATI wachezaji wengi wakitumia kipindi hiki kupumzika baada ya msimu mrefu, beki mpya wa Tottenham Hotspur, Marcos Senesi amejikuta akikatisha likizo yake baada ya kupata zali la mentali.

Akiwa katika fukwe za Ibiza, Hispania, Senesi alipokea simu kutoka kwa viongozi wa timu ya taifa ya Argentina waliomtaka kuripoti haraka kambini kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho ambacho awali hakuitwa kwa ajili ya fainali za Kombe la dunia.

Beki huyo, 29, ambaye wiki hii amekamilisha usajili wake wa kujiunga na Tottenham akitokea Bournemouth, alikuwa akifurahia mapumziko pamoja na mpenzi wake, Kelci Bowers wakati ndoto yake ya muda mrefu ilipotimia kwa njia ambayo hakuitarajia.

Kwa siku kadhaa kabla ya simu hiyo, Senesi alikuwa akiishi kwa matumaini baada ya Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni kuanza kutafuta mbadala wa beki wa Marseille, Leonardo Balerdi, aliyepata majeraha yaliyomlazimisha kukosa mashindano hayo.

Kwa mujibu wa video iliyosambazwa na mpenzi wake kwenye mitandao ya kijamii, wawili hao walikuwa wakijiandaa kwenda kula chakula cha jioni walipopokea simu kutoka kwa viongozi wa timu ya taifa ya Argentina.

Bowers alisema tangu waliporejea kutoka likizo yao Miami na kwenda Ibiza, akili zao zilikuwa zimebaki kwenye jambo moja pekee, kusubiri kuona kama Senesi angepata nafasi ya mwisho kwenye kikosi cha Kombe la Dunia.

“Hatukuwahi kupumzika kikamilifu kwa sababu tulikuwa tunafuatilia kila kilichokuwa kinaendelea. Marcos alikuwa akiifikiria nafasi hii kila siku na sasa imekuwa kweli,” alisema Bowers.

Baada ya kumaliza mazungumzo ya simu, Senesi na mpenzi wake walionekana wakikumbatiana na kushangilia kwa furaha baada ya kutambua ndoto ya kucheza Kombe la Dunia ilikuwa imetimia rasmi.

Wito huo ni matokeo ya kiwango bora alichokionyesha msimu uliopita akiwa Bournemouth na alikuwa mmoja wa nguzo muhimu zilizoisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu England na kufuzu Europa League kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Katika msimu uliopita pekee, Senesi alicheza mechi 37 za Ligi Kuu England, akijitambulisha kama mmoja wa mabeki wa kati wenye uwezo mkubwa wa kusoma mchezo, kushinda mipira ya juu na kuanzisha mashambulizi kutoka eneo la nyuma.

Safari yake ya soka ilianzia katika klabu ya San Lorenzo nchini Argentina kabla ya kuhamia Feyenoord ya Uholanzi mwaka 2019, ambako aliendelea kung’ara na kusaidia timu hiyo kufika fainali ya Europa Conference League mwaka 2022.

Kiwango chake bora katika Ligi ya Uholanzi maarufu kama Eredivisie kiliivutia Bournemouth ambayo ilimsajili na kumfanya kuwa mmoja wa mabeki walioleta mabadiliko makubwa kwenye kikosi hicho ndani ya kipindi kifupi.

Licha ya kuwa na nafasi ya kuichezea Italia kutokana na asili ya familia yake, Senesi aliamua kusubiri ndoto yake ya kuichezea Argentina, uamuzi ambao sasa umezaa matunda baada ya kuitwa kwenye kikosi cha mabingwa hao wa dunia.

Hadi sasa ameichezea Argentina mechi tatu pekee za kimataifa, lakini Kombe la Dunia 2026 linampa nafasi ya kuandika ukurasa mpya katika historia yake na kuongeza thamani yake ndani ya kikosi hicho.

Argentina itaingia kwenye mashindano hayo ikiwa na dhamira ya kutetea taji ililotwaa mwaka 2022 chini ya nahodha wao, Lionel Messi huku Senesi akiwa mmoja wa nyuso mpya zinazotarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi.

Kwa Senesi, safari kutoka kwenye fukwe za Ibiza hadi kwenye fainali za Kombe la duniani ni ushahidi kuwa wakati mwingine bahati inaweza kugonga mlango kwa simu moja tu na ukawa mwanzo wa hadithi mpya kabisa katika maisha ya mchezaji.