Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Macho yako yanaona kama mimi Kombe la Dunia?


WALTER Sampaio alipopuliza filimbi yake juzi pale Atzeca katika pambano kati ya Mexico na Bafana Bafana nilimuwaza Mtangaza Baraka Mpenja wa Azam TV ambaye ana tabia ya kutushirikisha katika 'ujinga'. Huwa anatuuliza "Macho yako yanaona kama mimi?".


Anataka wote tuone kitu kwa jicho lake. Anataka tuone kitu katika thamani ile ile ambayo yeye anaiona. Macho yako yanaona kama mimi? Na mimi nikawaza hivyo hivyo. Kuna vitu naviwaza katika kombe hili la dunia na huwa nataka watu wengine wawaze kama ninavyowaza. Kuna mengi lakini nimewaza machache.

Moja. Hivi hadi lini tutasema Brazil ndiyo timu ambayo inaongoza kwa kutwaa mataji mengi zaidi ya Kombe la Dunia. Tangu nazaliwa imekuwa hivyo. Alipiga makombe mengi kwa mkupuo wakati Edson Arantes do Nascimento 'Pele' na genge lake likiwa katika ubora wao.

Mwaka 1958 pale Sweden kisha 1962 pale Chile halafu 1970 pale Mexico. Na Mexico ndio, ni katika uwanja huu huu wa Azteca ambao Sampaio alianzisha mechi juzi.

Maisha yamekuwa hivi kwa muda mrefu. Baadae alichukua tena mara mbili lakini hata kabla hajachukua hayo mawili yaliyofuata bado tumekuwa tukiimba Brazil ndiyo timu iliyochukua kombe la dunia kwa miaka mingi zaidi. Natamani ibadilike. Nyuma yake kuna Italia na Ujerumani. Hawa jamaa wamechukua mara nne wakiwa nyuma ya Brazil aliyetwaa mara tano.

Tatizo la kwanza linalokuja ni Waitaliano hawapo kombe la dunia. Na ni kwa mara ya tatu mfululizo sasa Waitaliano wanakosa kushiriki Kombe la dunia. Sijui kitu gani kinatokea kule Italia katika nyakati hizi kuna mafundi wanachanua. Kina Sandro Tonali, Ricardo Calafiori, Gianluigi Donnarumma na wengineo. Ni huzuni.

Wajerumani wapo. Wana Kai Havert kule mbele na wana wachezaji wazuri. Wao ndio ambao wanaweza kubadili mkondo wa historia. Wakitwaa tu taji la msimu huu basi moja kwa moja watabadilisha mkondo wa historia. Tutakuwa tunaongea habari nyingine Brazil na Ujerumani ndizo zimetwaa kombe la dunia mara nyingi zaidi kuliko wengine.

Hata hivyo, nina mashaka na Wajerumani wenyewe. Sidhani kama wana mastaa kama wa Ufaransa. Sidhani kama wana kiwango cha Hispania. Na kila ninapoutazama mstari wa mbele wa Brazil napata mashaka na Wajerumani. Kule kuna Vinicius Junior, Raphinha, Gabriel Martinelli, Hendrick, Neymar na wengineo. Ghafla unaweza kukuta kile ninachokitamani hakitokei. Ghafla ndio unaweza kusikia Brazil anaongoza kwa kuchukua mataji mengi ya kombe la dunia akiwa na mataji sita. Tusubiri.

Kitu kingine ambacho natamani kitokee katika macho yangu ni kuona bingwa mtetezi akitetea taji lake. Tangu nizaliwe mwaka 1977 sijawahi kushuhudia hili. Walishuhudia mababu zetu wakati kina Pele walipotetea kombe la dunia mwaka 1962. Walitwaa mwaka 1958 pale Stockholm kisha wakatetea miaka minne baadae pale Santiago Chile. Mwingine aliyewahi kutwaa akatetea ni Muitaliano. Alifanya hivyo mwaka 1934 kisha akafanya tena mwaka 1938.

Sisi wa kizazi hiki tunazeeka bila ya kuona watu wakitetea taji lao. Ni kweli wanarudi fainali lakini hawatetei. Diego Maradona alitwaa mwaka 1986 katika uwanja huu huu wa Azteca lakini akashindwa kutetea alipofika fainali miaka minne baadae pale Italia. Walitwangwa bao 1-0 katika fainali ya utata dhidi ya Ujerumani Magharibi. Kumbuka wakati Diego na wahuni wenzake wakitwaa mwaka 1986 walicheza na hawa hawa Ujerumani Magharibi.

Mwingine ambaye alikaribia kutetea ni Mbrazil. Mwaka 1994 pale Marekani alitwaa. Kisha miaka minne iliyofuata mwaka 1998 akakutana na Mfaransa pale Stade de France. Hata hivyo, Mbrazil alifungwa mabao 3-0. Shukrani kwa ubora wa Zinedine Zidane katika pambano la fainali. Alifunga mabao mawili na yule Mfaransa anayefunga nywele kisogoni, Manu Petit akafunga bao moja.

Mwingine ambaye alikuwa anakaribia kutetea ni Mfaransa. Hawa jamaa walichukua ubingwa mwaka 2018 pale Moscow, Russia halafu baada ya miaka minne wakarudi tena kucheza fainali pale Doha Qatar lakini wakafungwa kwa matuta na Argentina. Ilikuwa ni fainali ambayo Mungu aliipanga kwa ajili ya Lionel Messi. Mungu alipanga maandiko atokee mchezaji bora wa muda wote duniani na kisha mchezaji huyo ashinde kombe la dunia.

Ukiangalia vikosi ambavyo vilikwenda Doha usingeona nafasi ya Argentina. Messi aliwahi kukosa ubingwa wa kombe la dunia pale Maracana akiwa na miongoni mwa vizazi bora vya Argentina kina Gonzalo Higuian, Angel Di Maria, Sergio Kun Aguero halafu akaenda kutwaa kombe la dunia na kina Rodrigo De Paul. Kama sio Mungu alitimiza maandishi tunaweza kusema kitu gani zaidi?

Safari hii simuoni Messi na wenzake wakitetea kombe la dunia. Miaka minne baada ya pale miguu yake imezidi kuchoka lakini bado Argentina haijazalisha wachezaji wa ajabu wa kutetea kombe la dunia. Sidhani kama watafuata nyayo za Waitaliano na Wabrazil ambao waliwahi kutetea katika zama za kale.

Kitu kingine ambacho macho yangu yangependa yakione kama ambacho yako yangeweza kupenda kukiona ni kama tunaweza kupata bingwa mpya wa kombe la dunia. FIFA ina nchi wanachama 211 duniani lakini ni timu nane tu zimewahi kutwaa kombe la dunia. Nchi nane tu. Kumpata mtu anayechukua kombe la dunia ni kazi ngumu.

Hadi sasa waliowahi kutwaa kombe la dunia ni Brazil, Ujerumani, Italia, Argentina, Uruguay, England, Ufaransa na Hispania. Basi. Hakuna mwingine. Tunaweza kumpata bingwa mpya? Yaani ambaye atakuwa anachukua kwa mara ya kwanza. Yaani ambaye atatoka nje ya hawa. Tunahitaji maajabu lakini kama ikitokea basi dunia itafurahi. Kila mtu atafurahi.

Kuna mambo mengine ya hapa na pale ambayo tunasubiri pia kuona. Kwa mfano, Mjerumani Miroslav Klose miaka 12 iliyopita pale Brazil aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa kombe la dunia. Alitimiza mabao 16 katika fainali zile ambazo Wajerumani walitwaa taji lenyewe. Lionel Messi amebakiza mabao matatu aifikie rekodi yenyewe. Kylian Mbappe amebakiza mabao manne afikie rekodi ya Klose.

Hii inaweza kutokea. Messi yupo kundi moja na Algeria, Austria na Jordan ambayo itakuwa inashiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza. Kama hawa Jordan watakuwa wanacheza huku muda mwingi wakisubiri pambano liishe ili wakapige picha na Messi pamoja na kugombea jezi yake. Humu Messi anaweza kupata mabao matatu katika hatua ya makundi kabla ya kusaka mengine katika hatua zinazofuata.

Mbappe ana nafasi kubwa. Mabao manne hayawezi kumsumbua Mbappe. Yupo katika ubora wake ingawa kule Madrid wale Madridista wanamzomea kila kikicha. Mechi dhidi ya Norway, Iraq na Senegal haziwezi kumsumbua sana Mbappe. Na Mfaransa anaweza kwenda mbali zaidi hadi hata fainali. Mbappe katika ubora wake huu anaweza kwenda mbali zaidi na kuvuka hata rekodi ya Klose.

Kama kuna mtu ana nafasi ya kufunga zaidi na kuweka rekodi yake mpya katika rekodi hii ya Klose anaweza kuwa Mbappe. Mungu akimpa afya nje anaweza hata kuwa katika kombe la dunia lijalo la mwaka 2030 akiwa na umri wa miaka 31. Macho yako yanaona kama mimi?. Yanaona vitu vyote hivi nilivyoandika? Michuano mema.