Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kadi za kidijitali zatikisa soka Uruguay

KADi Pict

Muktasari:

  • Tukio hilo la kihistoria lilitokea Oktoba 15, dakika ya 12 ya mchezo wa hatua ya 16 bora ya Copa AUF Uruguay kati ya Nacional na Rentistas, uliopigwa katika Uwanja wa Gran Parque Central, mjini Montevideo.

MONTEVIDEO, URUGUAY: MASHABIKI wa soka wameshangazwa na jaribio jipya la teknolojia ya waamuzi nchini Uruguay, baada ya mwamuzi Eduardo Varela kutumia kifaa kinachofanana na simu janja kuonyesha kadi ya njano 'kidijitali' badala ya kutumia kadi za kawaida.

Tukio hilo la kihistoria lilitokea Oktoba 15, dakika ya 12 ya mchezo wa hatua ya 16 bora ya Copa AUF Uruguay kati ya Nacional na Rentistas, uliopigwa katika Uwanja wa Gran Parque Central, mjini Montevideo.

Mchezaji wa Rentistas, Juan Pablo Plada, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuonyeshwa kadi ya njano ya kidijitali baada ya kumchezea rafu Maxi Silvera wa Nacional.

Badala ya kutoa kadi ya plastiki mfukoni, Varela alitoa kifaa chenye mwonekano wa simu janja kilichoonyesha rangi ya njano. Picha za tukio hilo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mjadala miongoni mwa mashabiki.

KAD 01

Baadhi ya mashabiki walionyesha kutoridhishwa na ubunifu huo. Shabiki mmoja aliuelezea kuwa teknolojia isiyo na manufaa katika soka, huku mwingine akidai kuwa huenda maendeleo hayo yakafungua njia ya kuondolewa kwa waamuzi uwanjani siku zijazo.

Teknolojia hiyo imebuniwa kupitia ushirikiano kati ya Shirikisho la Soka la Uruguay na kampuni binafsi ya teknolojia. Mbali na kurahisisha utoaji wa kadi za njano na nyekundu, kifaa hicho kina uwezo wa kurekodi uamuzi ya kinidhamu moja kwa moja.

Pia, kinaweza kurekodi mabao, mabadiliko ya wachezaji na matukio ya penalti, kisha kutuma taarifa hizo kwenye mfumo wa usimamizi wa mashindano.

KAD 02

Ofisa wa masuala ya uamuzi nchini Uruguay, Marcelo De Leon, amesema lengo la muda mrefu ni kuwezesha taarifa za mechi kupatikana mara moja kwa mamlaka za soka na baadaye vyombo vya habari.

Kifaa hicho kimeundwa kufanya kazi hata bila kuunganishwa na mtandao wa kawaida wa Wi-Fi, jambo linaloweza kukifanya kuwa na manufaa katika viwanja vidogo ambavyo havina huduma thabiti ya intaneti.

Hata hivyo, jaribio hilo limekumbana na changamoto kadhaa. Katika majaribio ya awali ya mchezo kati ya Defensor Sporting na Plaza Colonia, mwanga mkali wa jua uliripotiwa kufanya skrini ya kifaa hicho isiwe rahisi kuonekana.

Tatizo hilo pia lilijitokeza katika mchezo wa jioni kati ya Nacional na Rentistas, ambapo skrini ndogo ya kifaa hicho ilionekana kuwa na changamoto ya kuonekana kwa uwazi ikilinganishwa na kadi za kawaida.

KAD 03

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu uwezo wa teknolojia hiyo kuhakikisha wachezaji, mashabiki na watazamaji wa televisheni wanaona kwa urahisi uamuzi wa mwamuzi.

Kwa sasa, mamlaka za soka nchini Uruguay zinaichukulia teknolojia hiyo kama jaribio, huku wabunifu wake wakifanya maboresho ili kuongeza mwonekano wa skrini kabla ya kuanza kuitumia kwa upana zaidi.