Chipukizi Gabriel apagawisha Man United
Muktasari:
- Mara baada ya kugusa mpira kwa mara ya kwanza, alikumbana na mtihani mgumu baada ya kuchezewa faulo kali na beki wa kimataifa wa Uruguay, Jose Maria Gimenez, iliyomwangusha chini.
STOCKHOLM, SWEDEN: CHIPUKIZI mwenye umri wa miaka 15, JJ Gabriel, ameandika historia kwa kucheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa cha Manchester United wakati timu hiyo ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid mjini Stockholm.
Ingawa alicheza dakika nane pekee mwishoni mwa mchezo, Gabriel alipata nafasi ya kuonyesha uwezo wake na kuthibitisha kwa nini anatajwa kuwa mmoja wa vipaji vinavyopewa matumaini makubwa katika akademi ya United.
Mara baada ya kugusa mpira kwa mara ya kwanza, alikumbana na mtihani mgumu baada ya kuchezewa faulo kali na beki wa kimataifa wa Uruguay, Jose Maria Gimenez, iliyomwangusha chini.
Hata hivyo, baada ya kujishika mgongo kwa sekunde chache, Gabriel alisimama na kuendelea na mchezo kana kwamba hakuna kilichotokea, akionyesha uthabiti wa hali ya juu licha ya umri wake mdogo.
Mwanzoni alipata wakati mgumu kupata nafasi katikati ya uwanja, lakini alipohamishiwa upande wa kulia alionekana kuwa huru zaidi na kuanza kuonyesha ubora wake.
Msisimko wa mechi yake ya kwanza ulimfanya ashindwe kuudhibiti vizuri pasi mbili safi kutoka kwa Mason Mount, lakini baadaye aliingia ndani akitokea pembeni na kupiga shuti lililozuiwa na mabeki wa Atletico.
Gabriel pia alionyesha utulivu kwa kubadilishana pasi fupi na Leny Yoro kabla ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mpinzani aliyekuwa na nguvu zaidi kimwili.
Licha ya kutokuonyesha kila kitu anachokifanya katika soka la vijana, kupewa nafasi hiyo ni mafanikio makubwa kwa mchezaji ambaye wenzake wengi wa umri wake bado wanaendelea na mapumziko ya shule kabla ya kuanza masomo ya mwaka wa mitihani.
"Ni mchezaji mzuri sana. Bado ni mdogo na ana mengi ya kujifunza na kuboresha, lakini ni mnyenyekevu na anaendelea kufanya kazi kwa bidii. Nimefurahi amecheza dakika zake za kwanza na natumaini ataendelea kupiga hatua," amesema Yoro.
Yoro mwenyewe alicheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha Lille akiwa na miaka 16 na miezi sita mwaka 2022, hivyo anaelewa changamoto za kuingia kwenye soka la wakubwa akiwa na umri mdogo.
"Ninajiona ndani yake. Natumaini ataendelea kujifunza na kukua kwa sababu ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa," ameongeza.
Amad arudi kwa kishindo
Wakati huo huo, kurejea kwa Amad Diallo kutoka majukumu ya Kombe la Dunia kumeibua matarajio makubwa kwa mashabiki wa Manchester United.
Ingawa Ivory Coast ilitolewa katika hatua ya 32 bora nchini Marekani, Amad alikuwa mmoja wa wachezaji waliojitokeza baada ya kufunga mabao mawili.
Idadi hiyo ililingana na mabao aliyofunga katika msimu mzima akiwa Manchester United, huku akiongeza pia mabao matatu aliyoyafunga kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), jambo lililoonyesha kiwango chake kilikuwa bora zaidi akiwa na timu ya taifa kuliko klabu.