Juventus yajitosa kwa Sancho, Napoli bado ipo
Muktasari:
- Sancho ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Chelsea, mkataba wake na Man United unamalizika mwakani na mashetani hao wapo tayari kumwachia kwani hayupo katika mipango ya kocha wao Ruben Amorim.
JUVENTUS ya Italia ni miongoni mwa timu zinazohitaji saini ya winga wa Manchester United, Jadon Sancho, 25, dirisha hili la majira ya kiangazi lakini inakumbana na upinzani mkali kutoka Napoli.
Sancho ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Chelsea, mkataba wake na Man United unamalizika mwakani na mashetani hao wapo tayari kumwachia kwani hayupo katika mipango ya kocha wao Ruben Amorim.
Fundi huyu mwenye umri wa miaka 25, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026, msimu uliopita alicheza mechi 42 za michuano yote, amefunga mabao matano na kutoa asisti 10.
Mbali ya timu za Ulaya, huduma ya Sancho pia inahitajika na baadhi ya timu za Saudi Arabia lakini winga huyu hana mpango wa kuachana na soka la kiushindani kwa sasa.
Joao Palhinha
FULHAM imeingia katika vita dhidi ya Manchester United ili kumrejesha kiungo wa kati wa kimataifa wa Ureno, Joao Palhinha, 29, katika dirisha hili. Mabosi wa Fulham wanataka kumsajili staa huyu kwa mkopo wa msimu mmoja jambo ambalo Man United pia inataka kufanya. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Msimu uliopita hakucheza kwa kiwango kizuri Bayern Munich na alicheza mechi 17 za Bundesliga na hajafunga wala kuasist.
Paul Pogba
AS Monaco inaweza kukumbana na ushindani kutoka Al-Ittihad ya Saudi Arabia katika mpango wao wa kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 32, Paul Pogba, ambaye kwa sasa yupo huru baada ya adhabu yake ya kufungiwa kujihusisha na soka kutokana na kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni kuisha. Waarabu hao wanataka Pogba akijiunge na wafaransa wenzake Ng’olo Kante na Karim Benzema waliokiwasha pamoja timu ya taifa.
Illia Zabarni
MABINGWA wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain, imetuma ofa ya pili kwenda Bournemouth kwa ajili ya kumsajili beki kisiki wa timu hiyo na timu ya taifa ya Ukraine, Illia Zabarnyi katika dirisha hili. Taarifa zinaeleza PSG imewasilisha ofa ya Pauni 55 milioni lakini Bournemouth wamekataa ofa hiyo na kusisitiza wanahitaji Pauni 70 milioni.
Andre Onana
KIPA wa Manchester United na timu ya taifa ya Cameroon, Andre Onana, yupo katika rada za AS Monaco ambayo inafanya mazungumzo na wawakilishi wake kwa ajili ya kufanikisha usajili wa mchezaji huyo mwenye miaka 29. Ripoti kutoka Skysports zinaeleza kuwa Onana ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, anatajwa kuondoka kwa sababu Man United ipo katika mchakato wa kutafuta kipa mpya.
Ilkay Gundogan
MANCHESTER City iko tayari kumuacha kiungo wao wa kimataifa wa Mjerumani, Ilkay Gundogan, 34, aondoke katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Gundogan anahusishwa na baadhi ya timu za Saudi Arabia pamoja na Uturuki ambako Galatasaray ndio inaonekana kumhitaji sana. Nyota huyo alionyesha kiwango bora City tangu ajiunge nayo mwanzoni msimu uliopita akitokea Barcelona.
Antoine Semenyo
TOTTENHAM wamewasiliana na Bournemouth kuhusu uwezekano wa kuipata saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana mwenye umri wa miaka 25, Antoine Semenyo. Semenyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2029, msimu uliopita alicheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao 13.
Lucas Digne
BEKI wa Aston Villa na timu ya taifa ya Ufaransa, Lucas Digne, 31, ameanza mazungumzo na Atletico Madrid kuhusu uwezekano wa kujiunga na timu hiyo ya La Liga, ambayo ipo tayari kumpa mshahara wa pauni 8 milioni kwa mwaka. Digne ambaye mkataba wake na Villa unamalizika mwaka 2026, msimu uliopita alicheza mechi 45 za michuano yote.