Joao Felix: Saudi inamtajirisha
Muktasari:
- Ronaldo alisema watu waliokuwa wanasema hivyo hawajui chochote kuhusu mpira. Upande mwingine Joao anaonekana kuangalia maslahi zaidi kwani dili hilo limempa karibia mara mbili ya mshahara ambao alikuwa anaupokea akiwa na Chelsea.
RIYADH, SAUDI ARABIA: WIKI iliyopita moja kati ya mijadala ilikuwa ni komenti ya Cristiano Ronaldo ambaye aliwajibu watangazaji na wachambuzi wa soka waliokuwa wakikosoa uamuzi wa staa mwenzake wa Ureno, Joao Felix kuamua kwenda Saudi Arabia wakati umri wake ukiwa bado unaruhusu kupambana katika soka la ushindani Ulaya.
Ronaldo alisema watu waliokuwa wanasema hivyo hawajui chochote kuhusu mpira. Upande mwingine Joao anaonekana kuangalia maslahi zaidi kwani dili hilo limempa karibia mara mbili ya mshahara ambao alikuwa anaupokea akiwa na Chelsea.
Hapa chini tunakusogezea utajiri ambao staa huyu anao na jinsi atakavyotajirika zaidi baada ya kutua Al Nassr ambako anakunja mkwanja wa kutosha.
ANAPIGAJE PESA
Chanzo chake kikuu cha mapato ni mshahara ambao amekuwa akipokea katika timu mbalimbali alizopita. Alipokuwa Chelsea alikuwa akilipwa Euro 8 milioni kwa mwaka ambayo ilifikia Euro 170,000 kwa wiki kwa mjumuisho wa bonasi.
Hata hivyo, staa huyu ambaye ametua Al Nassr katika dirisha lililopita kwa sasa ndio anapokea mshahara mkubwa zaidi kuwahi kuupata katika maisha yake ya soka.
Katika mkataba wake wa miaka miwili kila msimu mmoja unamwezesha kupata Euro 17.5 milioni ambapo kwa wiki mbali ya bonasi anaweza kukunja Euro 336,538. Na ikiwa pamoja na bonasi, anaweza kupata hadi Euro 400,000 kwa wiki.
Mbali ya mshahara staa huyu pia anapata pesa kupitia mikataba ya udhamini aliyoingia na kampuni mbalimbali.
Awali, alikuwa chini ya Adidas ambayo ilikuwa ikifanya naye kazi kama balozi wao lakini kwa sasa tangu Februari 2025, amesaini dili na kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo ya Mizuno kutoka Japan ambayo inakadiriwa kumpa Dola 4 milioni kwa mwaka kwa kuwa balozi wao.
NYUMBA
Hadi sasa taarifa kutoka kwa watu wake wa karibu zinadai ana nyumba moja huko Ureno katika mji wa Viseu ambako ndio amezaliwa.
Kwa makadirio, nyumba hiyo ina thamani ya Dola 1 milioni. Mbali ya mjengo huo Joao amewahi kuishi nchi mbalimbali ambako mara nyingi amekuwa akikodi nyumba na kulipa kila mwezi.
Inaelezwa kwa wastani kodi yake kwa mwezi inafikia dola 20,000.
NDINGA
Anamiliki magari mbalimbali kama:
BMW M8 Competition - Dola 130,000
BMW X4 M Competition - Euro 130,300
Mercedes-Benz GLE53 AMG - Dola 80,000
Ferrari 488 - Dola 240,000
Audi A6 - Dola 56,000
MSAADA KWA JAMII
Aprili 2020, Joao Felix alitoa msaada wa vifaa kwa hospitali za mji wa Viseu, kwa ajili ya kusaidia watu waliokuwa na maambukizi ya virusi vya Corona.
Staa huyu pia amekuwa akishiriki katika matamasha mbalimbali ya mechi za hisani ambayo yana lengo la kukusanya pesa kwa ajili ya kusaidia watu wasiojiweza.
Vilevile amekuwa akisaini vitu kama mikoba, jezi na skafu ambavyo huenda kuuzwa katika minada na pesa inayopatikana hutumika kutoa misaada.
FAMILIA NA BATA
Anadaiwa kuwa katika uhusiano na mrembo Valentina Rueda Velez, raia wa Colombia ambaye ameonekana naye maeneo tofauti tangu Juni mwaka huu.
Kabla Valentina, Felix alikuwa katika penzi zito na mwigizaji raia wa Ureno Margarida Corceiro ambaye aliachana naye Juni, 2023. Hadi sasa bado hajafanikiwa kupata mtoto.