Jezi ya Messi, kitambaa cha unahodha vyaibwa
Muktasari:
- Katika video hiyo, watu wawili waliokuwa wamefunika nyuso zao wanaonekana wameshika vitu hivyo huku wakivielekeza kwenye kamera. Vitu hivyo vyote viwili vya kumbukumbu vina thamani kubwa ya fedha na kihisia, huku ikitarajiwa kuongezeka zaidi kadiri muda unavyokwenda.
PARIS, UFARANSA: MAANDAMANO yanayoambatana na vurugu yaliyoyotawala Paris, Ufaransa katika siku za hivi karibuni yameathiri pia ulimwengu wa soka, ambapo video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imewaonyesha watu wawili wakiiba jezi ya mechi ya Barcelona na kitambaa cha unahodha vilivyosainiwa na Lionel Messi kutoka katika duka moja lililopo katikati mwa jiji hilo
Wizi huo ulitokea wakati wa vitendo vya uharibifu wa mali karibu na eneo la Place de la Republique, ambalo lina maduka mengi yenye vitu vya thamani zikiwamo jezi, vito na amvazi yaliyowahi kuvaliwa na mastaa wa miche mbalimbali duniani.
Katika video hiyo, watu wawili waliokuwa wamefunika nyuso zao wanaonekana wameshika vitu hivyo huku wakivielekeza kwenye kamera. Vitu hivyo vyote viwili vya kumbukumbu vina thamani kubwa ya fedha na kihisia, huku ikitarajiwa kuongezeka zaidi kadiri muda unavyokwenda.
Wizi huo ulitokea kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya PSG na Barcelona uliochezwa jijini Paris, juzi, ambapo klabu hizo zote mbili zimekuwa na nafasi kubwa katika maisha ya soka ya Messi.
Vitu vilivyovaliwa na kusainiwa na Messi vinauzwa kwa bei kubwa katika soko la vitu vya kumbukumbu vya soka, na miaka mitatu iliyopita, jezi sita alizovaa Muargentina huyo wakati Argentina ilipotwaa Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar ziliuzwa katikamnada kwa zaidi ya Dola 1 milioni ikiwa ni rekodi katika minada ya vitu vya kumbukumbu za soka.
Thamani ya vitu vilivyoibwa itategemea mambo kadhaa, ikiwemo mechi ambayo vilivaliwa, kiwango cha uchezaji cha Messi siku husika, hali ya vitu hivyo na mahitaji ya wakusanyaji wa kumbukumbu za soka.
Ingawa ni vigumu kubainisha thamani yake halisi, jezi na kitambaa hicho cha unahodha vinaweza kuuzwa kwa maelfu ya dola katika soko haramu iwapo havitapatikana kabla ya kuuzwa.