Jean-Philippe Mateta akaribia kumalizana na Juventus
Muktasari:
- Mateta amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ushambuliaji ya Palace, lakini ameshawaambia mabosi wake anahitaji kuondoka ili kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
JUVENTUS wameongeza kasi katika harakati za kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace na Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, 28, baada ya kufanya mazungumzo rasmi na mawakala wake Ijumaa ya wiki iliyopita.
Mateta amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ushambuliaji ya Palace, lakini ameshawaambia mabosi wake anahitaji kuondoka ili kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Mkataba wake wa sasa unamalizika mwaka 2027 na Palace inaonekana wagumu kumwachia kutokana na idadi ndogo ya wachezaji ilionao kwa sasa wengi wakikosekana kutokana na majeraha.
Juventus inamtazama kama mbadala wa muda mrefu wa Dusan Vlahovic, ambaye mustakabali wake Turin unaendelea kuwa na maswali akitajwa anaweza kuondoka dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mateta pia amewahi kuhitajika na timu kadhaa za England ikiwemo Manchester United ambayo pia ilishindwa na kujiondoa katika mchakato kutokana na kiasi kikubwa cha pesa kilichohitajika.
Ousmane Diomande
ARSENAL imeanza harakati za kuimarisha safu yao ya ulinzi kwa kutaka kuwasajili mabeki wawili chipukizi ambao ni beki wa kushoto wa Eintracht Frankfurt, Nathaniel Brown pamoja na beki wa kati wa Sporting Lisbon na timu ya taifa ya Ivory Coast, Ousmane Diomande, 22.
Kocha Mikel Arteta anatafuta mabeki vijana wenye uwezo wa kukua kwa haraka ndani ya mfumo wake.
Hata hivyo, klabu zote mbili wanazotoka mabeki hao zinahitaji ofa inayoanzia Pauni 60 milioni ili kuwauza.
Ruben Neves
MANCHESTER United bado ina mpango wa kuendelea kuimarisha safu yao ya kiungo kwa kumsajili kiungo wa Al-Hilal na timu ya taifa ya Ruben Neves, 28, dirisha hili la majira ya baridi.
Neves alikuwa akitajwa kutaka kuondoka Al Hilal kwa muda sasa ili kurejea Ulaya lakini timu hiyo inahitaji zaidi ya Euro 30 milioni kiasi ambacho kimekuwa kikizirudisha nyuma timu nyingi zinazomhitaji. Man United bado inafanya majadiliano ili kupunguziwa bei.
Eduardo Camavinga
LIVERPOOL imeanza kuelekeza macho yao kwa kiungo wa Real Madrid na Ufaransa, Eduardo Camavinga, 23, kama sehemu ya mpango wao wa muda mrefu wa kujenga kikosi.
Camavinga ambaye amekuwa na panda shuka katika kikosi cha kwanza cha Madrid anaonekana kuwa tayari kukubali ofa hiyo ya Majogoo lakini shida inaonekana kwa mabosi wa Madrid ambao hawataki kuona akiondoka. Liverpool inaweza kuweka kiasi kikubwa cha pesa ili kuishawishi Madrid iwauzie.
Marc Andre Ter Stegen
WEST HAM UNITED iliingia katika mazungumzo na Barcelona kuhusu uwezekano wa kumsajili kipa wao raia wa Ujerumani, Marc-Andre ter Stegen, 33, lakini dili hilo linaonekana kukwama.
Kwa mujibu wa taarifa, Ter Stegen ameweka kipaumbele cha kuendelea kucheza La Liga, huku Girona wakionekana kuwa karibu zaidi kunasa saini yake.
Ikiwa atajiunga na Girona, Ter Stegen atakuwa akianza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka baada ya miaka mingi ya mafanikio akiwa Camp Nou.
Kevin Schade
TOTTENHAM Hotspurs ipo kwenye ushindani mkali na Aston Villa pamoja na Newcastle United ili kumsajili mshambuliaji wa Brentford na Ujerumani, Kevin Schade, 24, dirisha hili.
Schade amezivutia klabu nyingi utokana na kasi yake, uwezo wa kucheza pembeni au katikati na Brentford hawana mpango wa kumuuza lakini itafikiria kufanya hivyo ikiwa ofa nono itawasilishwa mezani kwao.
David Datro Fofana
Chelsea inapanga kumrudisha mshambuliaji wao wa kimataifa wa Ivory Coast, David Datro Fofana, 23, kutoka Fatih Karagumruk ya Uturuki aliko kwa mkopo.
Awali Fofana alikuwa kwenye rada ya Celtic, lakini mpango wa Chelsea sasa ni kumrejesha Stamford Bridge ili kurahisisha mazungumzo ya uhamisho wa moja kwa moja kwenda timu zinazomhitaji ikiamini itakuwa rahisi kufanya majadiliano na timu mbalimbali wakati staa huyu akiwa viunga vyao.
Jadon Sancho
WINGA wa Manchester United na England, Jadon Sancho, 25, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo Aston Villa, anaweza kurejea tena Borussia Dortmund kwa mara ya tatu katika maisha yake ya soka.
Dortmund inapanga kumsajili Sancho bure mwishoni mwa msimu huu, pindi mkataba wake na Manchester United utakapomalizika. Klabu hiyo inaamini mazingira ya Signal Iduna Park ndiyo yanayomfaa zaidi mchezaji huyo kwani ameonyesha kiwango bora katika nyakati ambazo amekuwa kwenye viunga hivyo.