Jamie Carragher: Carrick hawezi kuibeba Man United
Muktasari:
- Carrick, 45, alipewa kazi ya kuwa kocha wa kudumu wa Manchester United msimu huu wa kiangazi baada ya kufanya vizuri alipokabidhiwa timu hiyo kwa muda kufuatia kufukuzwa kwa Ruben Amorim mwezi Januari.
MANCHESTER, ENGLAND: Gwiji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, amedai Michael Carrick hana kile alichokiita “sifa” ya kutosha kuirejesha Manchester United kwenye kilele cha soka la England na Ulaya.
Carrick, 45, alipewa kazi ya kuwa kocha wa kudumu wa Manchester United msimu huu wa kiangazi baada ya kufanya vizuri alipokabidhiwa timu hiyo kwa muda kufuatia kufukuzwa kwa Ruben Amorim mwezi Januari.
Katika kipindi chake cha muda, Carrick aliiongoza United kupata ushindi dhidi ya Arsenal, Manchester City na Liverpool, matokeo yaliyoiwezesha kumaliza katika nafasi ya tatu na kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya misimu miwili bila kushiriki michuano hiyo.
Mwanzo huo mzuri wa Carrick kwenye benchi la United umeongeza matumaini miongoni mwa mashabiki kwamba anaweza kuiongoza klabu hiyo kutwaa taji lake la kwanza la Ligi Kuu England tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu mwaka 2013.
Hata hivyo, Carragher amewataka mashabiki wa United kuwa na subira kabla ya kuanza kuamini kwamba Carrick ndiye atakayeirudisha klabu hiyo kwenye utawala wake wa zamani.
“Sisemi kwamba mambo yataharibika. Kile ambacho Manchester United imekuwa nacho kwa miezi sita iliyopita, wanahitaji kuendelea kuwa nacho kwa miezi 12 zaidi kutokuwa klabu inayohusishwa na vurugu au kuwa habari kila wakati. Carrick anakupa hilo,” Carragher amesema kwenye kipindi cha The Overlap Fan Debate.
Kwa mujibu wa Carragher, utulivu ambao Carrick ameleta tangu alipopewa nafasi ya kuiongoza United ni jambo muhimu kwa klabu hiyo, lakini bado haoni ushahidi wa kutosha kwamba kocha huyo ana uwezo wa kuifikisha timu kwenye kilele cha soka.
United inatarajiwa kuanza msimu wa 2026/27 ikiwa na presha kubwa, huku mashabiki wakitarajia kuona kikosi hicho kikibadilika kutoka timu inayopambana kurejea kwenye ushindani wa juu hadi kuwa moja ya timu zinazowania ubingwa.