Prime
Aziz KI atia neno Yanga
STAA aliyerejea Yanga, Stephanie Aziz KI, amefurahia mapokezi aliyopewa klabuni hapo akidai anaipenda zaidi lakini akawatumia salamu mashabiki wa timu hiyo akisema msimu huu mabosi wamesajili timu tishio Afrika.
Yanga imemrudisha Aziz KI, ikimfanyia ukaribisho wa kistaa kupitia tukio maalum lililofanyika juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Katika utambulisho huo wa Aziz KI, uwanja huo ulijaa kutokana na muitikio wa mashabiki wa timu hiyo, huku akipewa jezi namba 10 aliyokuwa anaitumia kabla ya kuondoka Mei 2025.
Baada ya kuondoka kwa Aziz KI, jezi hiyo ilikuwa ikitumiwa na Pacome Zouzoua ambaye ameumia na hataweza kucheza msimu huu ambapo kwa mujibu wa uongozi wa klabu hiyo, Pacome aliridhia kumpa namba hiyo mwenzake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz KI amesema kwa muda mrefu alikuwa anasubiri hatua hiyo ya kurejea Yanga na kwamba amefurahishwa na hatua ya usajili uliofanyika msimu huu ukiwaleta mastaa wenye uwezo mkubwa.
Aziz KI amesema kwa namna usajili ulivyofanyika anaamini msimu huu Yanga haitakiwi kupigania kubakisha makombe ya ndani pekee, akitaka kwenda kuandikwa historia kubwa kwenye mashindano ya Afrika, watakaposhiriki Ligi ya Mabingwa.
“Yanga ni sehemu ya maisha yangu, ni kama najiona nimerudi kuungana na familia niliyotengana nayo kwa zaidi ya mwaka mmoja, napenda kila kitu kwenye klabu hii, mashabiki wetu wazuri lakini pia viongozi wenye maono ya mbali,” amesema Aziz KI.
“Narudi kwenye timu kubwa, yenye kikosi kilichosajiliwa vizuri, unajua hapa ni nyumbani, nilikuwa napata nafasi ya kuangalia mazoezi ya timu wakati na mimi nikifanya mazoezi, mashabiki wanatakiwa kutambua kwamba tuna kikosi kikubwa.
“Timu ya namna hii inakulazimisha kujituma, wakati wote tunahitaji kupambana sio tu kubakisha mataji ya ndani lakini pia kufanya vizuri kwa kufika mbali katika mashindano ya Afrika, akili zetu zinatakiwa kulenga huko.
“Nilikwambia mapema wakati msimu uliopita ukimalizika kwa ligi ya hapa, niliona namna wachezaji waliomaliza msimu uliopita walivyokuwa na uchovu, maboresho makubwa kama haya yalikuja wakati muafaka na wachezaji karibu wote viwango vyao ni vikubwa."
Kabla ya kuondoka Aziz KI, msimu wa 2023-2024 alifunga mabao 21 na kubeba tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara sambamba na kutangazwa mchezaji bora (MVP).
Baada ya kuwa na wakati mzuri kwa misimu mitatu kuanzia 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025 alipotua Yanga akitokea ASEC Mimosas, Aziz KI aliuzwa kwenda Wydad Athletic ya Morocco ambako alicheza kwa miezi sita, akanunuliwa na Al Ittihad ya Libya ambako nayo imeiuzia Yanga.
Yanga imemrudisha Aziz KI baada ya kumkosa Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku pia hatua ya kuuzwa Allan Okello aliyetimkia AS FAR Rabat ikikoleza usajili huo.
Katika usajili wa Yanga dirisha kubwa lililofungwa Agosti 15, 2026, wachezaji wapya wazawa ni Juma Issa Abushiri kutoka Fountain Gate, Hussein Juma Mihambo (Mashujaa), Abdulnasir Assa 'Gamal' (Mashujaa), Mohamed Mussa (Mashujaa), Erick Mwijage (KMC), Suleiman Mbarouk (JKU) na Seleman Mwalimu 'Gomez' (Wydad Casablanca).
Kwa upande wa kimataifa kuna Cheikh Ibrahima Toure kutoka Al-Jabalain, Albert Kangwanda (Red Arrows), Housseine Zakouani (Al-Zulfi), Peter Shalulile (Mamelodi Sundowns), Fred Duval Ngoma (Olympique de Safi), Oumar Farouk Comara (Golden Arrows) na Aziz KI (Al-Ittihad).