Ishu ya straika, Man United yatua kwa Keane

Muktasari:
- Vigogo wa Man United wamemuongeza Kean katika orodha ya mastraika wanaowataka baada ya kuona kumekuwa na ugumu kwa wale ambao imekuwa ikiwafukuzia tangu kuanza mwaka huu.
MANCHESTER United inaonyesha nia ya kumsajili straika wa Fiorentina na timu ya taifa ya Italia, Moise Kean, 25, ambaye ana kipengele cha kuondoka ikiwa timu inayomtaka italipa Euro 52 milioni kuanzia Julai 1 hadi 15.
Vigogo wa Man United wamemuongeza Kean katika orodha ya mastraika wanaowataka baada ya kuona kumekuwa na ugumu kwa wale ambao imekuwa ikiwafukuzia tangu kuanza mwaka huu.
Mkataba wa staa huyo Fiorentina unatarajiwa kumalizika ifikapo 2029 na msimu uliopita alicheza mechi 44 za michuano yote na kufunga mabao 25.
Mbali ya Kean, Man United inahusishwa na Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon na Bryan Mbeumo wa Brentford, lakini wote hao inaonekana kukutana na ugumu.
Francisco Conceicao
JUVENTUS imeweka kipaumbe cha kwanza cha kumsajili staa wa FC Porto, Francisco Conceicao katika dirisha hili la majira ya kiangazi kabla ya kugeukia kwa winga wa Manchester United, Jadon Sancho mwenye umri wa miaka 25. Awali ilielezwa, Juventus kipaumbele chake kilikuwa Sancho, lakini inaonekana kiasi cha pesa kinachotakiwa na Man United ni kikubwa zaidi kuliko ilivyo kwa Conceicao.
Jamie Gittens
BAYERN Munich imejiunga kwenye kinyang’anyiro cha kumfukuzia ili kumsajili Jamie Gittens, 20, ambaye pia anahitajika katika kikosi cha Chelsea. Mabingwa hao wa Ujerumani wanaripotiwa kuwa tayari kutoa kiasi kisichopungua Pauni 55 milioni kwa ajili ya kumsajili mchezaji huyo wa Borussia Dortmund katika dirisha hili la usajili huko Ulaya. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2028.
Nicolas Jackson
TAARIFA zinaeleza Chelsea haina mpango wa kumuuza mshambuliaji wake wa kimataifa wa Senegal, Nicolas Jackson, 24, kwa sasa licha ya kupatikana kwa ofa nono kutoka timu za Saudi Arabia. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca anadaiwa kuwa bado na imani na Jackson licha ya staa huyo kutoonyesha kiwango bora hivi karibuni.
Jarell Quansah
MABOSI Liverpool wamekubaliana kumuuza beki raia wa England, Jarell Quansah, 22, kwenda Bayer Leverkusen katika dirisha hili la majira ya kiangazi kwa Pauni 35 milioni 35, lakini wameweka kipengele cha kumnunua ikiwa watahitaji kufanya hivyo muda wowote. Jarrel ambaye mkataba wake na Liverpool unamalizika 2029, msimu uliopita alicheza mechi 25.
Noni Madueke
WINGA wa Chelsea na timu ya taifa ya England, Noni Madueke, 23, yupo kwenye rada za Arsenal ambayo inapamabana ili kuinasa saini yake katika dirisha hili la majira ya kiangazi barani Ulaya. Madueke anaripotiwa kutaka kuondoka katika kikosi cha Chelsea ili kutimkia sehemu ambayo atapata nafasi kubwa zaidi ya kucheza. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2030.
Federico Chiesa
NAPOLI na AC Milan zipo katika vita kali ya kuwania saini ya mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Italia, Federico Chiesa, 27, katika dirisha hili la usajili. Chiesa sio mmoja kati ya wachezaji ambao wanapata nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Liverpool, jambo linalosababisha atamani kuondoka mwisho wa msimu huu.
Andreas Christense
AC Milan ni miongoni mwa timu zilizojiingiza katika vita ya kuwania saini ya beki wa Barcelona na timu ya taifa ya Denmark, Andreas Christensen, 29, ambaye amepewa ruhusa ya kuondoka ikiwa atapata timu itakayokuwa tayari kumsajili. Mabosi wa Barca wanataka kumuondoa Andreas sababu tayari wana mabeki wa kati watano.