Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Isak katikati ya dili za usajili zilizokuwa gumzo Ulaya

Muktasari:

  • Sakata la Isak na Newcastle limekuwa gumzo zaidi kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

LONDON,  ENGLAND: STRAIKA, Alexander Isak ameripotiwa kurejea Newcastle kwenda kuzungumza na mabosi wa Newcastle United juu ya hatima yake kwenye dirisha hili la usajili.

Sakata la Isak na Newcastle limekuwa gumzo zaidi kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Isak aliripotiwa kuwaambia mabosi wa Newcastle kwamba anataka kuondoka baada ya kutambua Liverpool inahitaji saini yake. Straika huyo wa kimataifa wa Sweden aliondolewa kwenye kikosi wakati wa mechi za pre-season dhidi ya Celtic, kabla ya kuwekwa kando kwenye ziara ya Asia kwa madai kwamba ni mgonjwa.

Na kilichoripotiwa hivi karibuni, staa huyo alitumia viwanja vya timu yake ya zamani ya Real Sociedad kufanya mazoezi badala ya kutumia viwanja vya Newcastle, kabla na kuibukia makao makuu ya Newcastle huko Benton, asubuhi ya Jumatatu kujadili hatima yake.

Liverpool ilipeleka ofa yake ya kwanza ya Pauni 110 milioni kwa ajili ya mshambuliaji Isak, lakini Newcastle iligomea ikimthaminisha staa wao kwa Pauni 150 milioni, hiyo ikiwa ni mbinu tu ya kumzuia staa huyo asiondoke St James’ Park.

Miamba ya soka ya Saudi Arabia, Al-Hilal nayo imeingia kwenye vita ya kusaka huduma ya mshambuliaji huyo ikitaka huduma yake kwenye dirisha hili la kiangazi.

Isak anataka kujiunga na Liverpool, lakini kwenye kikosi cha Newcastle ambako hataki kucheza bado ana mkataba wa miaka mitatu, hivyo kufanya hilo kutokea itawabidi miamba ya Anfield ilipe ada ambayo wenye mchezaji wao wanataka walipwe, Pauni 150 milioni.

Hata hivyo, sakata hilo la Isak linaingia kwenye orodha ya usajili wa mastaa uliokuwa gumzo kubwa kwenye dirisha la usajili kabla ya kukamilika au kukwama.


Luis Figo (Barcelona kwenda Real Madrid)

Ni wachezaji wachache waliowahi kuzivugura timu za El Clasico na mmoja wao ni Luis Figo, wakati alipoweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali 2000 alipohama kutoka Barcelona kwenda Real Madrid. Figo aliondoka Camp Nou baada ya kufichua kwamba hakuwa akipendezwa na yaliyokuwa yakiendelea kwenye timu hiyo. Sakata lake lilikuwa gumzo kwelikweli na mashabiki wa Barca walionyesha hasira zao wakati walipomrushia kichwa cha nguruwe wakati aliporudi Camp Nou kwa ajili ya mechi mwaka 2002. Figo alishinda Ballon d’Or mwa 2001 na Ligi ya Mabingwa Ulaya 2002.


Steven Gerrard (Liverpool kwenda Chelsea/Real Madrid)

Mwaka 2005, iliaminika na dunia nzima kwamba kocha Jose Mourinho amefanikiwa kumshawishi Steven Gerrard kuondoka kwenye klabu ya ujana wake, Liverpool kwenda kufanya mapinduzi Stamford Bridge. Baada ya kushindwa kumsajili kwenye dirisha la mwaka uliopita, Chelsea ilirudi tena Anfield na Pauni 32 milioni kwa ajili ya kunasa saini ya kiungo huyo, kitu ambacho kiliwakasirisha mashabiki wa Liverpool kiasi cha kuchoma moto jezi za kiungo huyo. Liverpool iligomea ofa hiyo ya Chelsea. Kisha wakaja, Real Madrid kutaka saini ya Gerrard na ahadi ya mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki, kitu kilichoibua gumzo kubwa, lakini hakuna timu hata moja kwa wakati huo iliyofanikiwa kumnasa.


Viktor Gyokeres (Sporting CP kwenda Arsenal)

Straika wa Sweden, Viktor Gyokeres amekuwa gumzo kubwa kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya vuta nikuvute na klabu yake ya Sporting CP hadi kugomea mazoezi kabla ya kukamilisha uhamisho alioutaka wa kwenda kujiunga na Arsenal. Staa huyo alilazimika hadi kutoweka kwenye kambi ya Sporting ili kulazimisha uhamisho wake wa kwenda kujiunga na Arsenal, ambayo awali iliweka ofa yake mezani na kushindwa kufikia makubaliano juu ya mambo machache tu ikiwamo malipo ya bonasi. Lakini, sasa sakata hilo limemalizika, Gyokeres yuko zake Arsenal.


Kaka (AC Milan kwenda Man City)

Kwenye dirisha la kwanza la usajili baada ya matajiri wa Abu Dhabi kuichukua Manchester City, Septemba 2008, kitu cha kwanza ilichotaka kufanya ni kwenda AC Milan kung’oa huduma ya kiungo wa Kibrazili, Kaka. Man City ilimtaka Kaka aende kuwa nembo yao kwenye kikosi hicho cha Etihad. Kilichoelezwa ni kwamba iliweka mezani ofa ya uhamisho wa Pauni 100 milioni, pamoja na mshahara wa Pauni 500,000 kwa wiki. Dili hilo lilikuwa gumzo kwelikweli na kutawala habari za usajili kwenye dirisha hilo, lakini Kaka alikataa kwenda Man City, lakini mwaka uliofuatia, alienda kujiunga Real Madrid.


Harry Kane (Tottenham kwenda Man City)

Harry Kane alifikia uamuzi wa kukata tamaa na kutaka kuachana na Tottenham mwaka 2021 baada ya timu hiyo kushindwa kukamatia tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya huku ikimfuta kazi kocha Jose Mourinho. Kwa muda wote aliokuwa akijitoa kwa ajili ya klabu hiyo aliona sasa inatosha, akatafute timu nyingine. Man City iliposikia hivyo, ilijaribu kwenda kumsajili, huku kocha Pep Guardiola akimpamba kwamba ni mchezaji aliyemhitaji kwelikweli kwenye kikosi chake. Ofa ya Pauni 100 milioni iliwekwa mezani, lakini Spurs ilikataa. Man City haikushia hapo, ilikuwa tayari kulipa Pauni 127 milioni, lakini Kane alibaki Spurs, hadi hapo alipokubali kujiunga na Bayern Munich misimu miwili iliyopita.


Kylian Mbappe (PSG kwenda Real Madrid)

Hili ni sakata la usajili lilidumu kwa muda mrefu. Kylian Mbappe alikamilisha uhamisho wake wa kujiunga na Real Madrid mwaka 2024, lakini alifanya hivyo baada ya kufukuziwa kwa zaidi ya mwaka ambapo klabu yake ya Paris Saint-Germain iligoma kumruhusu kuondoka hadi hapo mkataba wake ulipomalizika na kutua Bernabeu bure kabisa. Mbappe alikuwa tayari kwenda kujiunga na Real Madrid, ambayo iliripotiwa kuweka mkwanja mrefu mezani, lakini PSG iligoma na kubaki na mchezaji huyo, ambapo ilikuwa tayari ikose pesa ili tu mchezaji abaki. Sakata lake lilidumu kwa muda mrefu na vitisho vingi.


Lionel Messi (Barcelona kwenda PSG)

Huu ni uhamisho ambao si Barcelona wala Lionel Messi walioutaka utokee, lakini hali mbaya ya uchumi iliyokuwa ikiikabili klabu hiyo ilijikuta ikishindwa kufanya kitu mwaka 2021. Barca ilishindwa kumpa ofa ya mkataba mpya mchezaji huyo kutokana na kubanwa na kanuni za La Liga za kuhusu mshahara na hivyo, Messi akatimkia PSG bure kabisa baada ya vuta nikuvute kubwa. Kilikuwa kipindi kigumu kwenye historia ya Barcelona kushindwa kumbakiza kwenye timu mchezaji wao bora kabisa na kumfanya aondoke bure kwenda kujiunga na wapinzani ambao ni wagumu kwao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.


Neymar (Santos kwenda Barcelona)

Uhamisho huo ulikuwa gumzo kwa miaka minne kabla ya Neymar kukamilisha dili lake la kutoka Brazil kuhamia Ulaya. Tangu mwaka 2009, akiwa Santos ya Brazil, Neymar alikuwa sehemu ya vita kali ya timu za Barcelona na Real Madrid kuwania saini yake hadi hapo miamba ya Camp Nou ilipofanikiwa kumsajili 2013. Sakata hilo lilikuwa zito kiasi cha kuhamia hadi mahakamani, wakati ilipodaiwa baba yake Neymar, alidanganya ada iliyolipwa ili kukwepa kulipa kodi stahiki kwenye mamlaka za Hispania. Neymar alikwenda kuwa mchezaji mahiri huko Barcelona kabla ya kuondoka kwenda Paris Saint-Germain kwa ada iliyovunja rekodi ya uhamisho duniani, Pauni 198 milioni.


Cristiano Ronaldo (Man United kwenda Real Madrid)

Wakati Real Madrid inapogonga hodi kwenye klabu kuhitaji huduma ya mchezaji, mara nyingi inaibuka kuwa washindi na hicho ndicho walichokifanya huko Manchester United mwaka 2009 ilipokwenda kuulizia huduma ya Cristiano Ronaldo. Mara ya kwanza kabisa Los Blancos ilihitaji saini ya Ronaldo kwenye dirisha la majira ya kiangazi 2008, Man United iligoma na kwenda kuishtaki Real Madrid huko FIFA kwa sababu ilikuwa ikitumia njia isiyo sahihi kumshawishi mchezaji wao. Lakini, gumzo kubwa lilikuwa 2009, ambapo Ronaldo alihama kwenda Real Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia kwa wakati huo, Pauni 80 milioni.


Carlos Tevez (Man United kwenda Man City)

Jina jingine kubwa kabisa kwenye soka lililovuruga klabu mbili mahasimu, wakati Carlos Tevez alipohama kutoka Man United kwenda Man City. Mkali huyo wa Argentina, Tevez alikuwa akicheza kwa mkopo Man United akitokea West Ham na mwaka 2009 alibebwa jumla, huku Man City ikiaminika kwamba ilimlipa mshauri wa mshambuliaji huyo, mkwanja wa Pauni 25.5 milioni ili kumsajili. Na kilichoelezwa ni kwamba Tevez alikuwa amekasirishwa kwa kitendo cha kukosa nafasi ya kucheza Man United, licha ya kwamba alifunga mabao 15 katika msimu wa 2008-09. Kitendo cha kukosa nafasi za kucheza kilimfanya kutimkia Man City, huku uhamisho wake ukiwa gumzo kubwa ikiwamo Man City kuweka bango kubwa la kumkaribisha Tevez Manchester baada ya kunasa saini yake.