Isak afanya mazoezi peke yake akiisubiri Liverpool
Muktasari:
- Isak hakusafiri na kikosi cha Newcastle kwenda Singapore kwa ajili ya ziara ya maandalizi ya msimu mpya, ambapo klabu ilieleza kuwa amekosekana kwa sababu ya “majeraha madogo ya paja”.
LIVERPOOL, ENGLAND: STRAIKA wa Newcastle, Alexander Isak ameonekana akifanya mazoezi peke yake katika klabu yake ya zamani, Real Sociedad, huku hatima yake ndani ya Newcastle United ikiwa bado haijulikani.
Isak hakusafiri na kikosi cha Newcastle kwenda Singapore kwa ajili ya ziara ya maandalizi ya msimu mpya, ambapo klabu ilieleza kuwa amekosekana kwa sababu ya “majeraha madogo ya paja”.
Badala yake, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameendelea kufanya mazoezi yake binafsi katika klabu ya Sociedad, ambako aliwahi kucheza mechi zaidi ya 100 kati ya mwaka 2019 na 2022.
Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Mail, bado haijafahamika kama Newcastle ilihusika rasmi kumpangia Isak arudi Sociedad kwa ajili ya kuendelea na programu ya mazoezi kwa wakati huu.
Isak bado ni mchezaji anayewindwa sana na Liverpool, ambayo inaripotiwa kuwa tayari kutoa Pauni 150 milioni kwa ajili ya kumsajili nyota huyo wa Sweden.
Vilevile kumekuwa na timu za Saudi Arabia zinazimhitaji, lakini inaelezwa kuwa Isak mwenyewe anataka kuendelea kucheza barani Ulaya.
Akizungumza kuhusu hatima ya Isak wiki hii, kocha wa Newcastle Eddie Howe alisisitiza kuwa hawajapokea ofa yoyote rasmi kwa ajili ya mchezaji huyo: “Bado ni mchezaji wetu, ana mkataba nasi. Kwa kiasi fulani, sisi tunaamua nini kinafuata kwake. Ningependa aendelee kubaki nasi, lakini si jambo lililo mikononi mwangu kabisa. Hatujapokea ofa rasmi kutoka klabu yoyote kwa ajili ya Alex. Natamani abaki na acheze nasi tena msimu ujao.”
Iwapo Isak ataondoka Newcastle katika dirisha la majira haya ya kiangazi, Newcastle imepanga kumsajili mshambuliaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, kama mbadala wake.
Sesko, mwenye umri wa miaka 22, alihusishwa kuondoka Bundesliga tangu msimu uliopita, lakini alikubali kuongeza mkataba na Leipzig hadi mwaka 2029.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kuna makubaliano ya ‘maalum’ kati ya Sesko na Leipzig ambayo yataruhusu kuondoka kwake kwa dau la kati ya Pauni 60 hadi 70 milioni kwenda baadhi ya klabu.
Iwapo Newcastle itaamua kumfuatilia Sesko, itatakiwa kushinda vita dhdi ya Manchester United, ambayo tayari imefikia hatua nzuri katika harakati za kumsajili staa huyu.
Mkurugenzi wa usajili wa Newcastle, Christopher Vivell, anatajwa kuwa shabiki mkubwa wa Sesko, kutokana na historia yake ya kufanya kazi naye huko Leipzig na pia akiwa Red Bull Salzburg, klabu ya zamani ya Sesko.
Newcastle inatumaini itaweza kumshawishi Sesko kuhamia St. James’ Park iwapo Isak atauzwa kwenda Liverpool.