Iraola awaonya wachezaji Liverpool
Muktasari:
- Liverpool ilionekana kutokuwa na makali wala mawazo mengi ya kutengeneza nafasi, hali iliyowakatisha tamaa mashabiki baada ya timu hiyo siku chache zilizopita kurejea kutoka nyuma na kuifunga Atletico Madrid 2-1.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Andoni Iraola, amewaambia wachezaji wake kuwa wanapaswa kuwa tayari kukabiliana na matokeo ya kupanda na kushuka wanapoendelea kuzoea mfumo wake mpya wa uchezaji.
Iraola ametoa kauli hiyo baada ya Liverpool kushindwa kupata ushindi mbele ya mashabiki wao katika sare ya bila kufungana dhidi ya Fulham Jumamosi iliyopita.
Liverpool ilionekana kutokuwa na makali wala mawazo mengi ya kutengeneza nafasi, hali iliyowakatisha tamaa mashabiki baada ya timu hiyo siku chache zilizopita kurejea kutoka nyuma na kuifunga Atletico Madrid 2-1.
Kocha huyo, ambaye katika michezo yake minne ya kwanza ya Ligi Kuu England ameambulia sare tatu na ushindi mmoja, amesema mchezo dhidi ya Fulham ndio uliomkatisha tamaa zaidi tangu achukue mikoba ya timu hiyo.
“Naelewa uchungu wa siku ile kwa sababu hata sisi tulikuwa tumekasirika,” amesema Iraola.
“Tulitoka kwenye michezo miwili mizuri na tuliona kuna maendeleo. Ipswich ilikuwa hatua mbele na Atletico Madrid pia, hivyo tulitaka mchezo mwingine uwe hatua zaidi. Lakini haukuwa hivyo; ulikuwa hatua moja nyuma.”
Iraola amesema changamoto kubwa sasa ni kuhakikisha Liverpool inapata mwendelezo wa kiwango katika kila mchezo.
“Lazima tukubali kwamba kutakuwa na kupanda na kushuka katika mchakato huu. Lakini tunajua tunataka kuelekea upande ambao tumeonyesha dhidi ya Atletico Madrid na Ipswich. Huo ndio mtindo wa soka tunaoutaka,” amesema.
MECHI NYINGI ZAMPA KAZI
Liverpool inakabiliwa na ratiba ngumu huku ikishiriki michuano minne, na Jana usiku ilitarajiwa kuwa mwenyeji wa Tottenham katika raundi ya tatu ya Carabao Cup.
Iraola anatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi, huku akisema bado anaendelea kujifunza ni wachezaji gani wanaweza kucheza mara kwa mara na ni akina nani wanaohitaji mapumziko.
“Baadhi ya wachezaji wanaweza kucheza kila baada ya siku tatu bila tatizo. Wana uimara na kiwango chao hakibadiliki sana. Lakini kwa wengine hatari ni kubwa zaidi na kiwango chao kinaweza kushuka,” amesema.
“Lazima nijue nani anaweza kucheza mechi tatu au nne mfululizo ndani ya siku chache na nani anahitaji kupumzishwa ili kiwango kisiathirike.”
Iraola pia alikiri kuwa bado hajui baadhi ya wachezaji wake watahimili vipi ratiba hiyo.
Alitoa mfano wa Jeremy Jacquet, akisema: “Ukinuliza Jeremy Jacquet atawezaje kucheza kila baada ya siku tatu kwa miezi miwili, sijui, kwa sababu hajawahi kufanya hivyo.”
GOMEZ KARIBU, BRADLEY BADO
Habari njema kwa Liverpool ni kwamba Joe Gomez yuko kwenye nafasi ya kurejea uwanjani kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuanza tena mazoezi kufuatia majeraha ya misuli aliyopata kipindi cha maandalizi ya msimu.
Hata hivyo, beki wa kulia wa Northern Ireland, Conor Bradley, bado yuko mbali na kurejea kikosini kutokana na jeraha la muda mrefu la goti.
“Hayuko karibu kuanza mazoezi na timu. Anafanya mazoezi peke yake, lakini ameanza kugusa mpira,” amesema Iraola.
“Nataka awe tayari haraka iwezekanavyo, lakini hili ni jeraha la muda mrefu. Giovanni Leoni yuko mbele yake kidogo, na bado itachukua muda kwa Conor kurejea.”