Inter sasa yampigia hesabu Sancho kisa ishu ya Lookman
Muktasari:
- Sancho hajaonekana kwenye kikosi cha Manchester United tangu mwezi Januari mwaka jana kufuatia mvutano mkubwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag. Wakati huo, Sancho alikataa kuomba msamaha kwa matamshi ya wazi dhidi ya kocha huyo, jambo lililomfanya afungiwe kushiriki mazoezi ya kikosi cha kwanza.
INTER Milan imefikiria kumsajili winga wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho, mwenye umri wa miaka 25, kama itashindwa kufikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Nigeria, Ademola Lookman, 27, kutoka Atalanta.
Sancho hajaonekana kwenye kikosi cha Manchester United tangu mwezi Januari mwaka jana kufuatia mvutano mkubwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag. Wakati huo, Sancho alikataa kuomba msamaha kwa matamshi ya wazi dhidi ya kocha huyo, jambo lililomfanya afungiwe kushiriki mazoezi ya kikosi cha kwanza.
Januari 2024, Man United walimtoa kwa mkopo kwenda Borussia Dortmund, klabu yake ya zamani, ambapo alionyesha mwelekeo mzuri zaidi. Alicheza mechi 21, akafunga mabao 3 na kutoa asisti 3, akiisaidia Dortmund kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ingawa ilifungwa na Real Madrid.
Katika msimu iliopita alicheza kwa mkopo Chelsea na hapo awali kulikuwa na taarifa kuwa timu hiyo ilipewa nafasi ya kumsajili Sancho moja kwa moja mwishoni mwa msimu, kwa mujibu wa kipengele kilichokuwepo katika mkataba wake, lakini ilikataa, badala yake ikalipa Pauni 5 milioni kama fidia ya kutotumia kipengele hicho.
Ademola Lookman amekuwa akiwindwa na vigogo mbalimbali barani Ulaya baada ya kiwango bora alichoonyesha msimu juzi ambapo alifunga hat-trick katika fainali ya Europa League dhidi ya Bayer Leverkusen.
Atalanta ipo tayari kumuuza lakini kwa timu itakayokuwa tayari kutoa Euro 60 milioni, kiasi ambacho Inter haitaki kulipa.
Sancho bado ana mkataba wa kuendelea kuwa mchezaji wa Man United hadi Juni 2026, lakini mashetani wekundu hao wamemweka sokoni na wanahitaji Pauni 20 milioni.
Tyrique George
RB Leipzig ya Ujerumani imetuma wawakilishi wake kwenda England kwa ajili ya kufanya mazungumzo ili kuipata huduma ya kiungo wa Chelsea, Tyrique George mwenye umri wa miaka 19, katika dirisha hili.
Awali, Chelsea ilitaka kumtumia staa huyo kama sehemu ya mabadilishano ili kumpata Xavi Simons, 22, lakini mabosi wa Leipzig walikataa na kusisitiza kwamba wanataka pesa ili kumuuza Simons, pia watatoa pesa kumnunua Tyrique.
Dele Alli
TIMU kadhaa za Ligi Daraja la Kwanza ziko katika vita ya kuiwania saini ya kiungo wa zamani wa Como, Dele Alli, 29, ambaye ameambiwa kuwa hayupo katika mipango ya klabu hiyo ya Serie A, kuelekea msimu ujao. Alli amekuwa akipitia changamoto kwa muda mrefu baada ya kiwango chake kushuka akiwa na Tottenham na ripoti zinaeleza huenda akatimkia Saudi Arabia au Marekani ambako baadhi ya timu zimeonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.
Alvaro Morata
GALATASARAY inataka Euro 6 milioni kutoka Como ili kuvunja mkataba wa Alvaro Morata ambaye anacheza katika kikosi chao kwa mkopo akitokea AC Milan.
Mabosi wa Galatasaray walimsajili Morata kwa mkopo katika mkataba ambao unatarajiwa kumalizika Januari mwaka huu lakini Como inapambana kumpata katika dirisha hili.
Giovanni Leoni
LIVEPROOL imemuweka katika rada zake beki wa kati wa Parma, Giovanni Leoni, 18, ambaye aling’ara katika Ligi Daraja la Kwanza akiwa na timu hiyo msimu uliopita.
Leoni ambaye ni sehemu ya kikosi cha Italia cha wachezaji wenye umri chini ya miaka 21, mkataba wake na Parma unamalizika mwaka 2027. Parma inahitaji Pauni 30 milioni ili kumuuza Leon ambaye msimu uliopita alicheza mechi 32.
Arnau Martinez
CRYSTAL Palace ipo katika hatua nzuri kumsajili beki wa kulia wa Girona na timu ya taifa ya vijana ya Hispania, Arnau Martinez, 22, katika dirisha hili lakini inakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa Juventus ya Italia. Martinez ni miongoni mwa mabeki waliotoa pasi nyingi za mabao (6) ndani ya La Liga msimu uliopita. Palace inamtazama kama mrithi wa Joel Ward.
Nathan Collins
LIVERPOOL inataka kutuma ofa kwenda Brentford ili kumsajili beki wa kati wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Ireland, Nathan Collins, 24, katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Collins ambaye alicheza mechi 30 za EPL msimu uliopita ni mmoja kati ya mabeki waliowekwa kwenye rada za Liverpool tangu kuanza kwa dirisha hili kuimarisha safu yao ya ulinzi.
Marc Cucurella
CHELSEA ipo katika mazungumzo na wawakilishi wa beki wao wa kushoto Marc Cucurella ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika mwaka 2028. Inadaiwa Chelsea imeingia naye katika mazungumzo ya kumpa mkataba mpya baada ya kuona kuna timu kibao ikiwamo Al Nassr ya Saudi Arabia ambayo pia inahitaji huduma yake. Katika msimu uliopita alicheza mechi 54.