Inter Milan yaingia vitani na Liverpool saini ya Guehi
Muktasari:
- Guehi ambaye ni tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Palace na timu ya taifa ya England, mkataba wake na Palace unatarajiwa kumalizika mwakani.
BEKI kisiki wa Crystal Palace, Marc Guehi ambaye anahitajika sana na Liverpool, ameingia katika rada za Inter Milan ambayo ipo tayari kupigana vikumbo na Majogoo hao wa Jiji la Liverpool kuhakikisha inaipata huduma yake katika dirisha hili.
Guehi ambaye ni tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Palace na timu ya taifa ya England, mkataba wake na Palace unatarajiwa kumalizika mwakani.
Beki huyu mwenye umri wa miaka 25, ameripotiwa kugoma kuongeza mkataba mpya licha ya kupewa ofa nono, hali inayoonyesha kwa kiasi kikubwa kwamba anataka kuondoka katika dirisha hili.
Mbali ya Inter na Liverpool, klabu yake ya zamani, Chelsea, pia imehusishwa kutaka kumsajili beki huyo wa timu ya taifa ya England, huku Newcastle pia ikimfuatilia kwa karibu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Calciomercato, Palace ambayo ni bingwa mtetezi wa Kombe la FA inataka mchezaji mbadala wa Guehi ambaye yuko tayari kuingia kikosini mara moja na baada ya hapo itamuuza staa huyu bila ya shida katika dirisha hili.
Inter Milan inaripotiwa kutaka kutoa Pauni 35 milioni kama ada ya uhamisho ya beki huyu wa kimatafa wa England ambaye msimu uliopita alicheza mechi 44 za michuano yote na kufunga mabao matatu.
Guehi ana asili ya Ivory Coast ambako ndiko alikozaliwa, lakini anachezea timu ya taifa ya England.
Gianluigi Donnarumma
MANCHESTER United imeanzisha mazungumzo na Paris St-Germain kwa ajili ya kumsajili kipa wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Italia, Gianluigi Donnarumma, mwenye umri wa miaka 26.
Staa huyu ambaye pia anawindwa na Chelsea, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao.
Donnarumma ambaye ni kipa namba moja wa PSG ameonyesha nia ya kuondoka na amekataa kusaini mkataba mpya licha ya kuwekewa mezani ofa na timu yake.
Alexander Isak
MABOSI wa Newcastle wamemwongeza katika orodha yao mshambuliaji wa Fulham na Brazil, Rodrigo Muniz, 24, ambaye inataka kumsajili katika dirisha hili ili akawe mbadala wa mshambuliaji wao wa kimataifa wa Sweden, Alexander Isak, 25, ambaye amefikia makubaliano ya kujiunga na Liverpool, katika dirisha hili. Muniz ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Fulham, msimu uliopita alicheza mechi 36 za michuano yote na kufunga mabao 11, Vigogo wa Fulham wapo tayari kumuuza kwa Pauni 40M.
Eberechi Eze
CRYSTAL Palace imeiambia Arsenal italazimika kulipa walau Pauni 35 milioni kama ada ya uhamisho ya awali ili kuipata saini ya mshambuliaji Eberechi Eze, katika dirisha hili. Kiujumla Palace inahitaji Pauni 67.5 milioni ili kumuuza Eze ambaye ameonyesha kuwa tayari kuondoka ili kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine. Kiungo huyu mshambuliaji wa England mwenye umri wa miaka 27, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Yann Bisseck
MABOSI wa Crystal Palace wako tayari kutoa Pauni 27.6 milioni kwenda Inter Milan kwa ajili ya kumsajili beki wa kati wa klabu hiyo na Ujerumani, Yann Bisseck, 24, katika dirisha hili. Bisseck ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029, ameonyesha nia ya kutaka kuondoka. Msimu uliopita alikuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Inter na tayari vigogo hao wameanza kusaka mrithi wake.
Robin Roefs
SUNDERLAND imefikia makubaliano na NEC Nijmegen ili kumsajili kipa wa klabu hiyo ambaye ni raia wa Uholanzi, Robin Roefs, mwenye umri wa miaka 22, katika dirisha hili.
Ripoti kutoka tovuti ya Athletic zinaeleza, Roefs atasaini mkataba wa miaka mitano na timu hiyo ambayo italipa takribani Pauni 15 milioni kama ada yake ya uhamisho.
Mkataba wa kipa huyu na Nijmegen unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 msimu uliopita alicheza mechi 33 za michuano yote na kati ya hizo 10 alimaliza bila ya kuruhusu bao.
Tyler Morton
OLYMPIQUE Lyon imefikia makubaliano binafsi na kiungo wa Liverpool, Tyler Morton, 22, lakini bei ya uhamisho ya karibu Pauni 8 milioni inayohitajika na klabu yake inadaiwa kuwa ni kikwazo. Mabosi wa Lyon kwa sasa wanapambana kuhakikisha Liverpool inashusha bei. Mkataba wa sasa wa Morton unatarajiwa kumalizika mwaka 2026.
Fabio Silva
AS Roma inataka kusajili wachezaji mbalimbali kutoka England katika dirisha hili ambao ni pamoja na mshambuliaji wa Wolves na timu ya taifa ya Ureno, Fabio Silva, 23, pamoja na winga wa Manchester City Muargentina mwenye umri wa miaka 19 Claudio Echeverri. Taarifa kutoka Skysports, zinaeleza wawakilishi wa Roma wameshawasili England.