Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Infantino apuuzia utata, akimtetea Trump Kombe la Dunia 2026

Muktasari:

  • "Tulieni tu, pumzikeni," Infantino aliwaambia waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Azteca siku moja kabla ya mechi ya ufunguzi kati ya Mexico na Afrika Kusini.

MEXICO CITY, MEXICO: Ukimsikiliza Rais wa FIFA, Gianni Infantino, unaweza kudhani utata uliozunguka Kombe la Dunia 2026 katika siku za hivi karibuni haukuwa jambo kubwa.

"Tulieni tu, pumzikeni," Infantino aliwaambia waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Azteca siku moja kabla ya mechi ya ufunguzi kati ya Mexico na Afrika Kusini.

Kauli hiyo imekuja licha ya matukio kadhaa yenye utata, ikiwemo mwamuzi wa Somalia, Omar Artan, kunyimwa kuingia nchini Marekani. Pia mshambuliaji wa timu ya taifa ya Iraq, Aymen Hussein, alihojiwa kwa saa kadhaa kwenye Uwanja wa ndege wa Chicago kabla ya kuruhusiwa kuingia.

Vilevile, timu ya Iran imelazimika kuweka kambi yake nchini Mexico badala ya Marekani, huku baadhi ya mashabiki wake wakifutiwa tiketi na baadhi ya wajumbe wa ujumbe wao kunyimwa viza.

Badala ya kuikosoa serikali ya Marekani au kuonyesha msimamo mkali kwa niaba ya FIFA, Infantino alieleza tukio la mwamuzi Artan kama jambo la "bahati mbaya" tu.

"Ni jambo la kusikitisha kilichomtokea mwamuzi kutoka Somalia, lakini hatuwezi kudhibiti kila kitu," alisema Infantino.

Kauli hiyo imezua ukosoaji mkubwa, hasa kwa kuwa Artan alirejeshwa kwao Mogadishu baada ya kuhojiwa kwa saa 11 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami na kushutumiwa kuwa na uhusiano na magaidi nchini kwake.

Infantino alisisitiza kuwa FIFA haiwezi kuamuru serikali kuhusu nani wa kuruhusiwa kuingia nchini na nani asiruhusiwe.

"Sisi si wafalme wa dunia ambao wanaweza kuziamuru serikali na vyombo vya usalama. Sisi ni shirika la michezo na tunafanya kadiri ya uwezo wetu," alisema Infantino.


Iran na changamoto za usafiri

Ingawa Iran imeruhusiwa kuingia Marekani kwa ajili ya mechi zake za hatua ya makundi, timu hiyo italazimika kuingia na kutoka Marekani ndani ya saa 24 kila inapocheza mechi zake.

Infantino, badala ya kuhoji vikwazo hivyo, alijivunia kwamba aliihakikishia Iran nafasi ya kushiriki mashindano hayo.

"Watu waliposema Iran haitaweza kuja Kombe la Dunia, niliwaahidi kwamba watakuja. Sijui ni nani mwingine angeweza kuhakikisha hilo katika mazingira haya," alisema Infantino.


Utetezi wa Trump

Pia, Infantino alimkingia kifua rais wa Marekani, Donald Trump, akisema Kombe la Dunia linalofanyika kwa kiasi kikubwa nchini Marekani lisingewezekana bila ushiriki wake.

"Nina uhusiano mzuri na Rais Trump na ninafurahia hilo. Bila ushiriki wake na mchango wake, nadhani isingewezekana kuandaa Kombe la Dunia nchini Marekani," alisema.

Aliongeza Trump alitambua mara moja ukubwa wa mashindano hayo na akaelekeza serikali yake kusaidia maandalizi.

Malalamiko kuhusu tiketi

Infantino pia alitetea mfumo wa bei za tiketi za Kombe la Dunia licha ya FIFA kukabiliwa na tuhuma za kupandisha bei kiholela na kuwapotosha mashabiki.

Alisema FIFA imekuwa ikifanya uamuzi wake kwa ushauri wa wataalamu na mawakili bora, huku akipuuza uchunguzi unaofanywa na mawakili wakuu wa majimbo ya California, New Jersey, New York na Texas kuhusu bei hizo.

Kwa jumla, mkutano huo wa waandishi wa habari ulionyesha wazi kwamba Infantino hakuwa tayari kuikosoa Marekani au serikali ya Trump kuhusu changamoto zilizowakumba baadhi ya waamuzi, timu na mashabiki kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia 2026. Badala yake, alisisitiza kuwa FIFA imefanya kila iwezalo ndani ya mamlaka yake, huku akitoa wito kwa watu “kutulia na kupumzika.”