IMEKUWAJE? Panda, shuka za mastaa waliotimka Old Trafford
Muktasari:
- Wengine waliuzwa moja kwa moja, huku wengine wakitolewa kwa mkopo wakiwa na matumaini ya kwenda kupata muda zaidi wa kucheza na kurudisha viwango vyao.
MANCHESTER, ENGLAND: BAADA ya msimu uliopita kuwa na panda shuka nyingi ndani ya Manchester United, baadhi ya wachezaji waliamua kutafuta malisho mapya katika dirisha la majira ya kiangazi.
Wengine waliuzwa moja kwa moja, huku wengine wakitolewa kwa mkopo wakiwa na matumaini ya kwenda kupata muda zaidi wa kucheza na kurudisha viwango vyao.
Katika makala hii tunachambua viwango vya wachezaji hao katika timu zao mpya ambao baadhi wanaonekana kukiwasha na wengine hali imeendelea kuwa vilevile.
ALEJANDRO GARNACHO - CHELSEA
Amekuwa na mwanzo wa kusua sua tangu alipotua katika vunga vya Stamford Bridge. Baada ya kujiunga na Chelsea kwa dau la Pauni 40 milioni kutoka Man United, Garnacho alipata nafasi ya kuanza mechi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo katika michuano ya Carabao Cup dhidi ya Lincoln City, lakini hakufanya vizuri.
Alicheza kwa dakika 59 bila kufanya dribble yoyote na hakutengeneza nafasi kubwa ya hatari. Mashabiki wa Lincoln walimzomea muda wote, wakimtupia maneno makali alipokuwa akitoka uwanjani.
Hadi sasa amecheza mechi tatu tu za michuano yote na hajafunga wala kutoa asisti. Kocha Enzo Maresca amesisitiza anamwamini sana lakini anataka kumpa muda kabla hajaingia katika mfumo.
MARCUS RASHFORD - BARCELONA
Rashford alikuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa walioondoka Manchester United katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, akijiunga na Barcelona kwa mkopo wa msimu mmoja.
Tangu atue katika kikosi hicho amekuwa mchezaji tegemeo na ameanza karibia mechi zote msimu huu na alifunga mabao mawili muhimu katika mechi dhidi ya Newcastle katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hadi sasa tangu kuanza kwa msimu huu, Rashford amefunga mabao matatu na kutoa asisti tano katika mechi 10 za michuano yote.
ANTONY - REAL BETIS
Winga huyu wa kimataifa wa Brazil aliamua kurejea Real Betis baada ya kufanya vizuri alipokuwa akicheza kwa mkopo msimu uliopita ambapo alifanikiwa kucheza hadi fainali ya UEFA Conference League.
Antony alishindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa Old Trafford licha ya kusajiliwa kwa Pauni 85 milioni mwaka 2021, hali iliyosababisha atolewe kwa mkopo msimu uliopita na kuuzwa kabisa msimu huu.
Kwa sasa mambo yanaonekana kuwa mazuri kwake na tangu kuanza kwa msimu huu wa 2025/26, amecheza mechi tano za La Liga, akafunga bao moja na kutoa asisti moja, lakini amekuwa na usaidizi mzuri kwa timu katika mfumo wa Betis pia ana usahihi wa pasi kwa asilimia 90.
RASMUS HOJLUND - NAPOLI
Taarifa zilisema Rasmus hakutaka kuondoka Manchester United, lakini alilazimika kufanya hivyo baada ya kocha kumwambia kwamba hana nafasi katika kikosi chake.
Ameanza vizuri akiwa Napoli ambao ni mabingwa watetezi wa Serie A. Hadi sasa amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu Italia na mawili katika Ligi ya Mabingwa.
Kiujumla amecheza mechi sita za michuano yote na amefunga mabao manne.
ANDRE ONANA - TRABZONSPOR (UTURUKI)
Baada ya kupoteza namba katika kikosi cha kwanza cha Manchester United, kipa huyu wa kimataifa wa Cameroon alihamia Trabzonspor kujaribu kupata nafasi na hatimaye kuwaka tena.
Mechi ya kwanza haikuwa bora sana kwake, lakini alianza vizuri baadaye kwa kutoa asisti katika mechi yake ya pili ya Ligi Kuu Uturuki.
Hadi sasa, amecheza mechi nne na ameruhusu mabao matano, pia amemaliza mechi moja bila ya kuruhusu bao. Ameokoa mikwaju 12 kati ya 15 iliyoelekezewa katika lango lake.
JADON SANCHO - ASTON VILLA
Sancho alijiunga na Aston Villa kwa mkopo kabla ya dirisha lililopita la majira ya kiangazi kufungwa. Ameshacheza dakika nane tu kwenye Ligi Kuu England na dakika 74 kwenye Carabao Cup dhidi ya Brentford (Villa ilitolewa kwa penalti).
Hadi sasa bado hajafunga wala kutoa asisti. Kocha Unai Emery amesema bado anajenga utimamu wa mwili kabla ya kumpa nafasi zaidi.
VICTOR LINDELOF - ASTON VILLA
Kama ilivyokuwa kwa Sancho, beki Victor Lindelof pia alijiunga na Aston Villa katika dirisha lililopita lakini yeye ilikuwa ni kwa usajili wa moja kwa moja baada ya mkataba wake na Man United kumalizika.
Amecheza dakika 25 tu kwenye mechi za michuano yote. Hata hivyo, anatarajiwa kupewa nafasi zaidi kwenye michuano ya Kombe la FA kutokana na uzoefu wake mkubwa.
CHRISTIAN ERIKSEN - WOLFSBURG
Kiungo wa kimataifa wa Denmark, Christian Eriksen amejiunga na Wolfsburg ya Bundesliga baada ya kuachwa na Man United.
Amecheza mechi tatu ambazo zote alitokea benchi ikiwamo ile dhidi ya Borussia Dortmund, ambayo walipoteza kwa 1-0.
Alikosolewa na mchezaji wa zamani wa Denmark, Thomas Gravesen, kwa kufanya mazoezi na timu ya Sweden ya Malmo kabla ya kusaini rasmi na Wolfsburg.
Licha ya kutopewa nafasi kubwa ya kucheza, kocha wa Wolfsburg amesema Eriksen atakuwa sehemu muhimu ya kikosi chake katika mechi zijazo.
TOBY COLLYER - WEST BROMWICH ALBION
Chipukizi mwenye kipaji Toby Collyer ametimkia West Brom kwa mkopo. Hadi sasa amecheza mechi nane za Championship ambazo baadhi aliingia akitokea benchini.
Anafanya vizuri katika eneo la kiungo mkabaji na anatabiriwa kuwa huenda akarejeshwa Old Trafford msimu ujao iendapo ataendelea kuonyesha makali yake ya sasa.
HARRY AMASS - SHEFFIELD WEDNESDAY
Beki huyu wa kushoto amejiunga na Sheffield Wednesday, timu ambayo inapitia kipindi kigumu cha kiuchumi. Alianza katika kikosi cha kwanza kwa mechi mbili akiwa kwenye nafasi ya winga wa kushoto ambapo alionyesha kasi na ubunifu. Lengo la kutolewa kwa mkopo ni kumpa uzoefu wa kucheza mara kwa mara kabla ya kurudishwa na kuanza kutumika.