Huko Man United kazi ipo

Muktasari:
- Kocha huyo mpya amekiri atakuwa kwenye hatari ya kufutwa kazi kama ilivyo kwa kocha mwingine yeyote endepo matokeo hayatakuwa mazuri.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA Ruben Amorim anafahamu wazi mashabiki wa Manchester United wamechoshwa na mwenendo wa klabu yao kwa sasa.
Kocha huyo mpya amekiri atakuwa kwenye hatari ya kufutwa kazi kama ilivyo kwa kocha mwingine yeyote endepo matokeo hayatakuwa mazuri.
Amorim amekuwa na kikosi hicho cha Old Trafford kwa mwezi mmoja, lakini kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wolves kwenye Boxing Day kimefanya Man United ipoteze tano kati ya saba kwenye Ligi Kuu England na kesho Jumatatu miamba hiyo inakabiliwa na mtihani wa kuikabili Newcastle United.
Bilionea mmiliki wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe ameshaonyesha jinsi asivyokuwa mvumilivu kwenye ishu ya kufukuza watu baada ya kumwonyesha mlango wa kutokea mkurugenzi wa michezo, Dan Ashworth baada ya kuwa na klabu hiyo kwa siku 159.
Man United imeshapoteza nusu ya mechi 10 za kwanza ilizocheza chini ya Amorim - wakati mtangulizi wake Erik ten Hag alipoteza mechi mbili kati ya 10 za mwisho alizokuwa kwenye klabu hiyo ya Old Trafford. Lakini, Ten Hag alishinda mechi tatu tu kati ya hizo, wakati Amorim ameshinda nne.
Man United imefunga mabao machache chini ya kocha mpya, mabao 17 tu, ukilinganisha na mabao 18 iliyofunga chini ya Ten Hag.
Man United imeruhusu mabao 17 chini ya Amorim, wakati Ten Hag alipokuwa na timu hiyo, nyavu zao ziliguswa mara 11 tu.
Amorim, ambaye alipokuwa Sporting Lisbon, timu yake ilifunga mabao 19 katika mechi tano za mwisho, amejiunga na Man United kwa mkataba utakaofikia ukomo majira ya kiangazi 2027 na amesema hadi muda huo kufika mwisho utakuwa mrefu sana kuhukumiwa kwa kile atafanya kwenye kikosi hicho.
Kocha, Amorim anafahamu wazi hatafika mwisho wa mkataba wake kama Man United itashindwa kupata matokeo mazuri, akidai kwamba hivyo anapaswa kubadili hali ya mambo kwa haraka zaidi. Man United ililipa fidia ya Pauni 8.3 milioni huko Sporting Lisbon kuvunja mkataba wa kocha huyo ili wamchukue.
Amorim alisema: “Kocha wa Manchester United kamwe, kwa hali yoyote ile hawezi kuwa na starehe. Wamelipa fidia kunipata. Nafahamu, usiposhinda, kila kocha anakuwa kwenye hatari, napenda hiyo kwa sababu ndiyo asili ya kazi yetu. Unaweza kusema kwamba nimekuwa hapa kwa mwezi mmoja, kwamba nimekuwa na vipindi vichache vya mazoezini, lakini hatushindi. Matarajio ni kushinda mechi nyingi, kuwa na wachezaji ambao wanajiamini na kuwa na uwezo wa kuonyesha kile tunachojifunza mazoezini ili kufanya timu kuwa na kiwango kizuri uwanjani.”
Man United hii ndiyo timu yenye kiwango kibovu zaidi kuwahi kutokea. Baada ya kipigo kutoka kwa Wolves, Amorim alikiri kwamba sasa wanapaswa kupambana kubaki kwenye Ligi Kuu England, wakishika nafasi ya 14 kwenye msimamo, pointi nane juu ya timu tatu za mkiani.
Hofu nyingine ni jinsi safu ya ulinzi ya Man United inavyotaabika kuuzua mipira ya kutenga, kona na friikiki. Imeruhusu mabao 10 kutokana na mipira hiyo ya kutenga, mabao matano kati ya hayo yamefungwa chini ya kocha Amorim.