Hugo Ekitike afunguka usiyoyajua kuhusu Mohamed Salah
Muktasari:
- Ekitike raia wa Ufaransa, ameanza vyema maisha yake Anfield kufuatia uhamisho wake wa pauni milioni 79 kutoka Eintracht Frankfurt ya Ujerumani msimu huu.
MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Hugo Ekitike, amefichua maisha ya nyota wa kimataifa wa Misri, Mohamed Salah, namna anavyoishi ndani ya nje ya uwanja.
Ekitike raia wa Ufaransa, ameanza vyema maisha yake Anfield kufuatia uhamisho wake wa pauni milioni 79 kutoka Eintracht Frankfurt ya Ujerumani msimu huu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, tayari amefunga mabao matano katika mechi tisa chini ya kocha Arne Slot, pamoja na kutoa asisti moja.
Ekitike, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, ameeleza hisia zake kuhusu kucheza pamoja na Salah, mmoja wa wachezaji ambao amekiri kuwahusudu ndani ya kikosi cha Liverpool kwa sasa.
Katika mahojiano na BBC Sport, Kelly Somers amemuliza Ekitike: “Kucheza na Mohamed Salah ni vipi?”
Ekitike amejibu: "Ni vizuri sana. Mo ni mtu wa kuvutia sana, ni mchangamfu na ni rahisi kuzungumza naye. Ni mchezaji mzuri sana kucheza naye.
"Nilikuwa nikimtazama kwenye TV akifunga mabao, lakini ni mchangamfu na anajua kukimbia kwa mitego anapokuwa uwanjani. Unaweza kujifunza mengi kutoka kwake na kujiboresha. Ni jambo zuri kuwa naye uwanjani, na natumai tutafunga mabao mengi na kuleta ushindi mkubwa kwenye timu yetu."
Kelly Somers pia ametaka kujua Salah ni mtu wa aina gani nje ya uwanja, akauliza: "Yukoje anapokuwa nje uwanja?"
Ekitike amejibu: "Yuko poa sana. Zaidi ya nilivyomwona kwenye TV kwa sababu wakati mwingine unaona sura yake ikiwa ya kawaida sana bila tabasamu, nilidhani ni mtu wa mbinafsi… mtu asiyeongea sana. Lakini ni mchangamfu sana, kama wachezaji wengine wote hapa Liverpool. Wote ni wachangamfu na wanataka nizoee haraka."
Ekitike bado yuko katika hatua za awali kama mchezaji wa Liverpool, lakini tayari ameonyesha dalili kuwa anaweza kuwa nyota mkubwa.
Mashabiki wengi walikuwa na mashaka baada ya Liverpool kutumia kiasi kikubwa cha pesa kumsajili majira ya kiangazi, lakini mshambuliaji huyo wa zamani wa PSG sasa amewafunga midomo wakosoaji wake.
Kwa upande mwingine, Mohamed Salah hajaanza vyema sana msimu huu, akiwa amechangia mabao matatu na asisti tatu katika mechi tisa. Tangu alipojiunga na Liverpool kutoka Roma mwaka 2017, Salah amefunga mabao 248 na kutoa asisti 116 katika mechi 410.