Hizi sura tatu mzuka mwingi
Muktasari:
- Lakini, kulikuwa na matumaini makubwa kwenye safu mpya ya ushambuliaji inayoundwa na mastaa watatu iliyotoa taswira namna kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim kitakavyokuwa na balaa kwenye msimu huu.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imepoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England msimu huu mbele ya Arsenal inayokimbizia ubingwa.
Lakini, kulikuwa na matumaini makubwa kwenye safu mpya ya ushambuliaji inayoundwa na mastaa watatu iliyotoa taswira namna kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim kitakavyokuwa na balaa kwenye msimu huu.
Man United ilionekana kujipata kwenye fowadi yake tofauti na msimu uliopita baada ya kutumia Pauni 200 milioni kuboresha eneo hilo la ushambuliaji.
Fowadi wawili - Bryan Mbeumo na Matheus Cunha walianzishwa kwenye mechi hiyo wakati straika Benjamin Sesko alianzia benchini na kuingia dakika 30 za mwisho. Mwanzoni mwa mchezo ilionekana kama Cunha angecheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, huku Mason Mount na Mbeumo wakichangia kwenye Namba 10 nyuma yake. Lakini, nafasi na majukumu ya Cunha yalikuwa tofauti kabisa maana yake mechi kuanza alibadilika na kucheza kila mahali hadi hapo alipoingia Sesko kwenye kipindi cha pili.
Mechi hiyo ilikuwa na ladha kwa mashabiki wa Man United jinsi fowadi yao mpya ya wakali watatu itakavyocheza kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu. Lakini, kiufundi fowadi hao watatu wanaleta kitu gani kikosini Man United?
Bryan Mbeumo
Wakati Man United iliponasa saini yake kwa kulipa Pauni 71 milioni Mbeumo hakukuwa na shaka juu ya ubora wake hasa baada ya kufunga mabao 20 na asisti tisa msimu uliopita.
Dhidi ya Arsenal, Mbeumo amegusa mpira mara 54, amepiga pasi 30 huku 24 zikifika sawasawa, ameshinda bato nne za kugombea mpira na mpinzani na amepiga mashuti matano. Kilikuwa kiwango bora.
Mbeumo alionekana kuuelewa vyema mfumo wa 3-4-2-1, ambao umekuwa ukitumiwa na kocha Amorim. Alicheza upande wa kulia na alikuwa hatari kwa Arsenal kwenye mikimbio yake ya bila mpira. Mwanzo ulikuwa mzuri.
Matheus Cunha
Huu ulikuwa usajili wa haraka sana Man United baada ya msimu kumalizika, wakati ilipokubali kulipa Pauni 62.5 milioni huko Wolves kupata saini ya Cunha.
Kama ilivyokuwa kwa Mbeumo, Man United ilivutiwa na kiwango cha Cunha cha msimu uliopita alipofunga mabao 17 na asisti sita.
Dhidi ya Arsenal, Cunha aligusa mpira mara 35, pasi 16 huku 14 zikiwa sahihi, mashuti manne na ameshinda mara nane bato za ana kwa ana, huku akikamilisha matukio manne ya kukokota mpira.
Wakati wengi wakiamini Cunha atacheza Namba 10 upande wa kushoto nyuma ya straika, kwenye mechi hiyo alianza kama straika, lakini alikimbia kutoka umbali mkubwa na kuwasumbua mabeki.
Dakika 30 za mwisho alipoingia Sesko, Cunha alirudi kwenye Namba 10.
Benjamin Sesko
Mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England, Sesko alicheza kwa dakika 30 tu na kipute hicho cha Arsenal alionyesha kitu ambacho mashabiki wa Man United wanaamini watakuwa salama chini yake.
Sesko aligusa mpira mara saba, alipiga pasi nne na zote zilikuwa sahihi, akashinda bato moja ya mapambano ya ana kwa ana na mpinzani, mashuti mawili.
Bila shaka, Sesko ataanza kwenye mechi ijayo, jambo ambalo litafanya safu kamili ya washambuliaji watatu wapya ikianza katika kikosi hicho cha Man United, ambapo atacheza kwenye nafasi ya straika na nyuma yake kutakuwa na wakali wawili Cunha na Mbeumo, watakaokuwa wakiichangia Namba 10.
Mikimbio ya Sesko na ubora wa kupiga pasi za mwisho za mastaa Cunha na Mbeumo bila ya shaka wapinzani wajao wa Man United watakuwa kwenye wakati mgumu wa kuikabili safu hiyo hatari ya ushambuliaji.