Hizi mechi za kutolea macho!
Muktasari:
- Goodison Park, wenyeji Everton wataikaribisha Manchester United inayocheza kichovu msimu huu, huku kipute hicho kikimpa David Moyes fursa ya kukutana na waajiri wa zamani. Vipi Moyes ataendeleza majanga huko Man United, ambayo kwa sasa ipo karibu na timu zilizopo kwenye vita ya kushuka daraja kuliko zilizopo kileleni. Ngoja tuone.
LONDON, ENGLAND: WIKIENDI ya kibabe sana kwenye Ligi Kuu England. Shughuli pevu zaidi itakuwa huko Goodison Park, Villa Park na Etihad. Patamu hapo.
Goodison Park, wenyeji Everton wataikaribisha Manchester United inayocheza kichovu msimu huu, huku kipute hicho kikimpa David Moyes fursa ya kukutana na waajiri wa zamani. Vipi Moyes ataendeleza majanga huko Man United, ambayo kwa sasa ipo karibu na timu zilizopo kwenye vita ya kushuka daraja kuliko zilizopo kileleni. Ngoja tuone.
Huko Villa Park, Chelsea itakwenda kukabiliana na Aston Villa katika mechi ambayo itakuwa na maana kubwa kwa Kocha Enzo Maresca juu ya usalama wa ajira yake huko Stamford Bridge. Kipigo kwa Chelsea kitamweka pabaya kocha Maresca, huku mwenzake wa Aston Villa, Unai Emery akisaka ushindi ili kujiweka pazuri kwenye mchakamchaka wa kusaka tiketi ya kuheza Ulaya msimu ujao.
Balaa lenyewe litakuwa huko Etihad, wakati Manchester City itakapokuwa nyumbani kuikaribisha Liverpool, mechi ambayo itabeba taswira nzima ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Arne Slot atakwenda ugenini kujaribu kusaka pointi muhimu ili kuendelea kutamba kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo, lakini Pep Guardiola atataka kuwapoza mashabiki baada ya kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akipambana pia kuhakikisha timu inamaliza ligi kwenye Top Four. Mechi ya kibabe sana.
Arsenal inayoikimbiza Liverpool kwenye mbio za ubingwa, yenyewe itatangulia kucheza ikiwa nyumbani mbele ya West Ham United. Ushindi kwenye mchezo huo wa Emirates, utawafanya Arsenal kupunguza pengo la pointi na kubaki tano na baada ya hapo Mikel Arteta na jeshi lake, ataomba mabaya kwa Liverpool, liwakute Etihad.
Mechi nyingine itashuhudia, Bournemouth iliyowasha moto kwa sasa ikikipiga na Wolves, wakati Fulham itakuwa kwenye vita kali dhidi ya Crystal Palace, wakati Ipswich Town itakuwa nyumbani kukipiga na Tottenham na Southampton itamalizana na Brighton.
Mchezo mwingine kwenye wikiendi hii, Newcastle United itakuwa St James' Park kukipiga na Nottingham Forest, ambayo imekuwa na maajabu makubwa msimu huu na kufanya mechi hiyo kutarajiwa kuwa na mvuto mkubwa. Litatokea nini, balaa hilo.
Namba za Man City na Liverpool, zenyewe zimekutana mara 55 kwenye Ligi Kuu England na sare ni 21, huku City ikishinda 12, mara 10 nyumbani na mbili ugenini, wakati Liverpool imeshinda 22, mara 18 nyumbani na nne ugenini. Tungoje sasa itakuwaje? Guardiola atatibua mpango wa Slot?
Everton na Man United zimecheza mechi 65 kwenye ligi na ubao unasoma Man United imeshinda 42, mara 23 nyumbani na 19 ugenini, wakati Everton imeshinda 10, nane nyumbani na mbili ugenini huku sare zikiwa 13. Kocha Ruben Amorim, ataendeleza rekodi nzuri ya Man United? Au ndo mwaka wa shida?
Arsenal kwa West Ham inajipigia tu, kwenye mechi 57 imeshinda 37 na sare 11, huku ikipoteza tisa tu.