Hii kiboko! Red kadi 51 mechi moja
Muktasari:
- Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Brazil, O Tempo, polisi wa kijeshi waliitwa baada ya uharibifu mkubwa kutokea kwenye Uwanja wa Parque do Sabia.
RIO DE JANERIO, BRAZIL: Mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Mashindano ya Vijana chini ya miaka 20 ya jimbo la Minas Gerais nchini Brazil imeingia katika historia baada ya kutolewa kadi nyekundu 51 kufuatia vurugu zilizozuka uwanjani.
Jumla ya wachezaji 43 na maafisa wanane wa benchi la ufundi walitolewa kwa kadi nyekundu katika mchezo kati ya Uberlandia na Mamore. Rekodi ya awali ilikuwa kadi 36, zilizotolewa mwaka 2011 katika mechi ya daraja la tano nchini Argentina kati ya Club Atletico Claypole na Victoriano Arenas.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Brazil, O Tempo, polisi wa kijeshi waliitwa baada ya uharibifu mkubwa kutokea kwenye Uwanja wa Parque do Sabia.
Ripoti ya mwamuzi inaeleza kuwa ugomvi ulizuka kipindi cha pili baada ya mchezaji wa Mamore, Davi, kuwachokoza watu wa benchi la wapinzani wakati akishangilia bao lililoifanya timu yake kuongoza kwa mabao 3-1.
Kocha wa makipa wa Uberlandia, Paulo Sergio Dias Dos Santos, aliingia uwanjani kumkabili Davi, hali iliyosababisha mapigano na kutolewa kwa kadi nyekundu. Wachezaji watatu walikuwa tayari wameonyeshwa kadi nyekundu kabla ya tukio hilo.
Ripoti ya polisi ilitaja milango 14 iliyovunjwa, uharibifu katika vyumba vya kuoga, madirisha yaliyovunjika na uharibifu wa viti vya benchi, meza na viti vingine.
Mchezo ulisimamishwa kwa takribani dakika 40 kabla ya mwamuzi Fernando Patrick Drosghic Modesto kuamua kuumaliza bila kukamilika.
Baadaye, Uberlandia ilitangaza kuwa imekubali kuachia mchezo wa marudiano wa nusu fainali. Mamore ilikuwa imebakiwa na wachezaji saba pekee kutokana na kadi nyekundu zilizotolewa.
Uberlandia ilieleza uamuzi huo kuwa ni “ishara ya uungwana wa michezo”. Kwa matokeo hayo, Mamore itasonga mbele kucheza fainali, huku Uberlandia ikielekeza nguvu zake kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya tatu.