WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wameendelea kuonyesha makali yao baada ya kupata ushindi wa 10 mfululizo katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2026/27, rekodi inayoiweka miongoni mwa timu 11 barani Afrika ambazo hazijapoteza mchezo katika ligi zao.
Ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC juzi Jumatatu umeifanya Simba kuendeleza rekodi ya asilimia 100 ya ushindi, ikiwa imekusanya pointi 30 katika mechi 10, huku ikifunga mabao 23 na kuruhusu sita, ikiwa na tofauti ya mabao 17.
Ushindi huo pia umefikisha mechi 20 mfululizo za ushindi kwa Simba tangu msimu uliopita, ikiendelea kujitengenezea nafasi ya kipekee katika orodha ya timu zenye mwenendo bora Afrika.
Simba ndiyo timu pekee kutoka Tanzania katika orodha hiyo, inayojumuisha vigogo wa soka kutoka nchi nyingine tano za Afrika.
Misri inawakilishwa na Pyramids na Al Ahly, huku Morocco ni AS FAR pamoja na RS Berkane, wakati Algeria ni MC Alger, MC Oran na CR Belouizdad. Afrika Kusini ni Mamelodi Sundowns pamoja na Orlando Pirates, huku Tunisia ikiwa na US Ben Guerdane na US Monastir.
Kwa upande wa Misri, Pyramids ndiyo inayoongoza kwa ubora wa matokeo ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi nane, zote ikishinda. Imefunga mabao 19 na kuruhusu manne.
Al Ahly ina pointi 20 katika mechi nane, ikiwa na ushindi sita na sare mbili, huku ikifunga mabao 15 na kuruhusu sita.
Morocco inawakilishwa na AS FAR iliyokusanya pointi nane katika mechi nne, ikiwa na ushindi mbili na sare mbili. Imefunga mabao matano na kuruhusu mawili.
RS Berkane nayo ina pointi saba katika mechi tano, ikiwa na ushindi mmoja na sare nne, huku ikifunga mabao manne na kuruhusu mawili.
Timu hizo mbili zimeendelea kulinda rekodi ya kutopoteza, tofauti na Raja Casablanca iliyopoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Berkane Novemba 1, 2026.
Algeria ina timu tatu zinazolinda rekodi zao. MC Alger ina pointi 13 katika mechi tano, ikiwa na ushindi nne na sare moja, huku ikifunga mabao saba na kuruhusu moja.
MC Oran ina pointi 15 katika mechi saba, ikiwa na ushindi nne na sare tatu. Imefunga mabao matano bila kuruhusu bao lolote.
CR Belouizdad imekusanya pointi 17 katika mechi saba, ikiwa na ushindi tano na sare mbili, huku ikifunga mabao 12 na kuruhusu saba.
Katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns ina pointi 26 baada ya kucheza mechi 10, ikiwa na ushindi nane na sare mbili. Imefunga mabao 27 na kuruhusu tisa.
Orlando Pirates ina pointi 25 katika mechi tisa, ikiwa na ushindi nane na sare moja, huku ikifunga mabao 21 na kuruhusu mawili pekee.
Kwa wastani wa pointi kwa kila mchezo, Pirates inaongoza kwa 2.78, ikifuatiwa na Sundowns yenye 2.6.
Tunisia inawakilishwa na US Ben Guerdane yenye pointi 17 katika mechi saba, ikiwa na ushindi tano na sare mbili. Imefunga mabao 12 na kuruhusu sita.
US Monastir ina pointi 12 katika mechi sita, ikiwa na ushindi tatu na sare tatu, huku ikifunga mabao nane na kuruhusu matano.
Kwa kulinganisha pointi, Simba inaongoza katika kundi hilo ikiwa na 30, ikifuatiwa na Mamelodi Sundowns yenye 26, Orlando Pirates 25 na Pyramids 24.
Hata hivyo, tofauti ya idadi ya mechi inapaswa kuzingatiwa katika tathmini hiyo, kwani Simba na Sundowns zimecheza mechi 10 kila moja, Pirates tisa na Pyramids nane.
Kwa upande wa ushambuliaji, Sundowns inaongoza kwa mabao 27, ikifuatiwa na Simba yenye 23 na Orlando Pirates yenye 21. Pyramids imefunga 19, huku Al Ahly ikiwa na 15.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Simba ina uwezo wa kushindana katika eneo la ushambuliaji na baadhi ya timu zenye nguvu kubwa barani Afrika, licha ya kutokuwa kinara wa mabao.
Uimara wa safu za ulinzi nao unatofautiana, huku MC Oran ikiwa haijaruhusu bao katika mechi saba, MC Alger ikiruhusu moja katika mechi tano na Orlando Pirates mawili katika mechi tisa.
Simba imeruhusu mabao sita katika mechi 10, ikiwa na eneo la kuboresha ili kuendelea kulinda rekodi yake ya ushindi.
Akizungumzia ushindi huo, kocha wa Simba, Steve Barker alisema si kila mchezo katika mfululizo huo utakuwa rahisi, akieleza kuwa wapinzani wamekuwa na ari kubwa ya kuivunja rekodi ya timu yake.
Alisema wakati wa mapumziko aliwakumbusha wachezaji wake namna walivyowahi kuwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika kipindi cha kwanza, kabla ya kurejea na kushinda.
“Si kila mchezo utakuwa rahisi. Kutakuwa na changamoto kama tulizokutana nazo leo. Nilipokwenda mapumziko niliwakumbusha wachezaji kwamba si muda mrefu uliopita tulikuwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga kipindi cha kwanza, lakini tulirejea na kushinda.