MDINGI RICH: Ndoto zake hazijazimwa na maisha
Muktasari:
- Ndivyo ilivyo pia kwa msanii Richard Mdingi anayefahamika kisanii Mdingi Rich, ambaye licha ya kukutana na changamoto mbalimbali za kiuchumi, bado anaamini siku moja atafika kwenye majukwaa makubwa ya muziki na kumiliki kampuni itakayosaidia kukuza vipaji vya wasanii.
KUNA wakati maisha yanamlazimisha mtu kuweka pembeni kitu anachokipenda ili apambane na hali halisi iliyopo. Hata hivyo, kwa baadhi ya watu, kufanya hivyo hakumaanishi wameachana na ndoto zao.
Ndivyo ilivyo pia kwa msanii Richard Mdingi anayefahamika kisanii Mdingi Rich, ambaye licha ya kukutana na changamoto mbalimbali za kiuchumi, bado anaamini siku moja atafika kwenye majukwaa makubwa ya muziki na kumiliki kampuni itakayosaidia kukuza vipaji vya wasanii.
JINA LAKE
Jina la Mdingi Rich lina historia yake. Msanii huyo anasema jina la Mdingi limetokana na jina lake la asili na ukoo, Richard Mdingi, lakini safari yake ya kisanii haikuanza kwa kutumia jina hilo.
“Nilikuwa natumia jina la Onster tangu shule ya msingi mpaka sekondari. Baadaye nikaja kuchagua Mdingi Rich kwa sababu nilitaka jina litakalowakilisha ukubwa wa kazi zangu, tungo ninazofanya na utajiri wa maudhui ninayowasilisha kwa jamii kupitia muziki,” anasema.
WIMBO WA KWANZA
Safari yake ya muziki ilianza rasmi kwa wimbo uitwao Dar Salama alioufanyia katika studio za Kiumbe Record zilizopo Tabata, Dar, akishirikiana na Sande Njoole anayefahamika pia kama Hasla.
Anasema kazi hiyo ilipokelewa vizuri na watu waliokuwa wakifuatilia muziki kupitia vituo vya redio, lakini changamoto kubwa ilikuwa kuifikisha kwa mashabiki wengi zaidi.
“Wimbo wangu wa kwanza ulikuwa Dar Salama. Nilifanya Kiumbe Record Tabata na Hasla. Mapokezi yalikuwa mazuri, watu wa idara za muziki redioni waliipenda kazi, lakini tatizo kubwa lilikuwa kuutangaza ‘promotion’. Unahitaji uwezo wa kifedha ili kazi yako ipigwe mara kwa mara na watu wengi waweze kuifahamu,”€ anasema.
MTAJI TATIZO
Anasema mtaji wa kuanzia ni tatizo kubwa kwa wasanii wengi, hasa wale wanaotaka kufanya kazi zenye ubora wa juu. Anaeleza kuwa zamani studio hazikuwa nyingi kama ilivyo sasa, akitaja baadhi ya studio zilizokuwa zikifanya kazi kipindi hicho kuwa ni za Master J, Said Comorie na P Funk ‘Majani’. Pamoja na ongezeko la studio, Rich anasema kuna mambo ambayo yanahitaji kurekebishwa katika tasnia hiyo.
“Siyo promosheni pekee, kuna suala la mtaji wa kuanzia. Zamani studio zilikuwa chache, lakini kulikuwa na nidhamu na ubora katika kazi za maproducer. Sasa studio zimeongezeka, lakini wakati mwingine unakutana na changamoto ya ubora na nidhamu ya kazi,” anasema.
MZIKI UMEBADILIKA
Anasema gharama za muziki zimeongezeka kwa sababu msanii anahitaji kuwekeza katika maeneo mengi zaidi ili kazi yake iweze kushindana kwenye soko. Kwa sasa, pamoja na kurekodi wimbo, kuna gharama za kutengeneza video zenye ubora wa kisasa, kufanya kazi na maproducer tofauti na kutafuta ladha mpya ya muziki.
“Unataka kujaribu ladha mpya, unahitaji kufanya kazi na produzya mwingine, unahitaji video nzuri na pia promosheni. Hayo yote yanahitaji fedha. Unaweza kuwa na kipaji na wimbo mzuri, lakini kama huna uwezo wa kugharamia mambo hayo inakuwa vigumu kuufikisha muziki wako kwa watu wengi,” anaongeza.
SAFARI YAKE NJE NA MZIKI
Lakini, nje ya muziki, maisha ya Mdingi Rich yana simulizi nyingine inayofafanua kwa nini safari yake haikuwa rahisi. Alisomea Usimamizi wa Fedha za Sekta ya Umma katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Magogoni, Dar es Salaam na kuhitimu stashahada mwaka 2013. Baada ya masomo alitafuta ajira kwa muda bila mafanikio, jambo lililomfanya 2015 ajiunge na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Zanzibar, ambako alitumikia kwa kipindi cha miaka miwili hadi 2017. Aliporejea Bara alikutana na ugumu wa ajira, jambo lililomlazimu kutafuta njia nyingine za kujipatia kipato.
“Nilikuwa nimejaribu kufanya biashara ya kuuza WiFi kwa miezi minne bila kupata mauzo wala kipato cha uhakika. Wakati huo pia kulikuwa na changamoto za kifamilia, mzee alikuwa anaumwa na kulikuwa na madeni ya benki. Niliona tangazo la kazi mtandaoni, nikaamua kuomba kazi ya ulinzi ili nipate mshahara ambao utanisaidia kulipa kodi na kutunza familia,” anasema msanii huyo.
CHANGAMOTO YA VIJANA WENGI
Kwa mujibu wake, mazingira hayo yanaonyesha namna ambavyo vijana wengi wenye vipaji wanavyoweza kujikuta wakishindwa kuendeleza ndoto zao kutokana na ukosefu wa fedha. Hata hivyo, ana ujumbe kwa vijana wanaopitia changamoto zinazofanana na zake, akiwataka kutokata tamaa wala kusubiri mpaka wawe na fedha nyingi ndipo waanze kuonyesha uwezo wao.
“Ningependa vijana wajue kwamba penye nia pana njia. Kama una kipaji cha kweli na unakipenda unachokifanya, usikate tamaa kwa sababu ya changamoto. Changamoto zinapaswa kukujenga na kukufanya uwe imara zaidi, si kukuondoa kwenye ndoto zako,” anasema.
“Siku hizi siyo lazima uwe na studio kubwa ndiyo uanze kuonyesha kipaji chako. Kuna ‘apps’ ambazo unaweza kutumia kwenye simu yako kurekodi na kutengeneza sample za kazi zako. Unaweza kuonyesha uwezo wako kupitia mitandao ya kijamii na watu wakaanza kukufahamu. Muhimu ni kuanza na kile ulicho nacho.”
NDOTO KUBWA
Licha ya kupitia misukosuko hiyo, Mdingi Rich anasema ndoto zake bado ni kubwa kuliko mazingira aliyopitia.
Anataka siku moja ajione akitumbuiza kwenye majukwaa makubwa ya muziki, huku akihamasisha vijana wengine wenye vipaji ambao wanapitia changamoto zinazoweza kuwakatisha tamaa.
Zaidi ya kuwa msanii anayefahamika, ana ndoto ya kuwa sehemu ya mabadiliko ya tasnia ya muziki nchini kwa kuwekeza katika miundombinu itakayowasaidia wengine.
“Nataka siku moja nifike kwenye majukwaa makubwa, lakini pia nataka niwe mtu wa kuwapa moyo vijana wenye vipaji. Ndoto yangu kubwa ni kumiliki kampuni au viwanda vya muziki vitakavyokuwa na uwezo wa kurekodi sauti, kutengeneza video, kufanya promotion na hata kusaidia upande wa maigizo,” anasema.