Estevao ondoka na kijiji, Alonso mmh
Muktasari:
- Alipotolewa dakika ya 86, mashabiki wa nyumbani walimsimamia kwa makofi, huku Alonso akimkumbatia. Katika mchezo huo, Estevao alipiga mashuti sita, akagusa mpira mara 12 ndani ya eneo la hatari la United, akatengeneza nafasi tatu, akapiga krosi nane na kufanikiwa kupiga chenga tano.
LONDON, ENGLAND: CHIPUKIZI Estavao Willian ametoa onyesho la kuvutia katika ushindi wa Chelsea wa mabao 2-0 dhidi ya Manchester United, akiongeza shinikizo kwa kocha Xabi Alonso kumpa nafasi ya kudumu kikosini.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 19 hakuwa ameanza mchezo wowote wa Ligi Kuu England msimu huu kabla ya kukutana na Man United Jumamosi. Katikati ya wiki, alikaa benchi bila kutumika Chelsea ilipofungwa kwa penalti na Liverpool, lakini mashabiki wa timu hiyo waliendelea kumshangilia Anfield.
Siku tatu baadaye, mashabiki wa Chelsea waliweka wazi walichotaka. Mapema katika mchezo wa Stamford Bridge, walikuwa wakiimba jina la utani “Steve-o”, walilompa mchezaji huyo aliyesajiliwa kutoka Palmeiras kwa pauni 38 milioni.
Akiwa uwanjani, Estevao alionyesha makali katika kikosi kilichokuwa bila mshambuliaji wa kati anayetambulika. Bao lake la mapema lilikataliwa kwa sababu ya kuotea, kabla ya bao jingine zuri alilofunga karibu na lango kipindi cha pili pia kukataliwa kwa uamuzi uliokuwa wa karibu na wa kwanza.
Alipotolewa dakika ya 86, mashabiki wa nyumbani walimsimamia kwa makofi, huku Alonso akimkumbatia. Katika mchezo huo, Estevao alipiga mashuti sita, akagusa mpira mara 12 ndani ya eneo la hatari la United, akatengeneza nafasi tatu, akapiga krosi nane na kufanikiwa kupiga chenga tano.
Idadi ya mashuti yake ilikuwa kubwa zaidi ya mchezaji mwingine yeyote wa Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu msimu huu. Takwimu zake nyingine pia zilikuwa miongoni mwa zilizokuwa juu zaidi kwa mchezaji wa Chelsea katika mchezo huo.
Nafasi ndogo aliyopewa hivi karibuni imeibua maswali. Kabla ya mchezo huo, alikuwa ameanza mechi moja tu msimu huu, dhidi ya Luton Town ya Ligi Daraja la Kwanza katika Kombe la Carabao mwezi Septemba.
Hali hiyo ilichochea taarifa katika vyombo vya habari vya Brazil zikidai kuwa huenda mchezaji huyo hakuridhika au akawa anataka kuondoka Chelsea. Hata hivyo, watu wa karibu na klabu pamoja na wanaomfahamu Estevao wamesema hakuna dalili za kutoridhika kwake.
Badala yake, amesifiwa kwa weledi wake nje ya uwanja na kuonekana kuwa amekosa nafasi kwa bahati mbaya, hasa kutokana na kiwango cha Morgan Rogers, Cole Palmer na Joao Pedro. Pia, Chelsea imekuwa ikipata mabao ya mapema, jambo lililoifanya benchi mara nyingi litumie wachezaji wa kuongeza uimara wa ulinzi.
Kabla ya mchezo dhidi ya United, kulikuwa na taarifa kuwa Alonso alikuwa akificha mpango wa kumchezesha Estevao, baada ya kuulizwa mara kadhaa kuhusu winga huyo. Hata hivyo, kocha huyo alithibitisha baada ya ushindi kuwa uamuzi huo ulikuwa umefanywa mapema, mara tu baada ya Chelsea kufungwa nyumbani na Tottenham wiki iliyopita.
“Baada ya mchezo dhidi ya Tottenham tulizungumza, naye alijua angecheza leo,” amesema Alonso.
“Alijibu kwa njia bora zaidi na kuonyesha kuwa anastahili nafasi zaidi na alikuwa tayari. Hicho ndicho unachotaka kutoka kwa mchezaji, kwa hiyo nina furaha sana kwa ajili yake.”
Alonso ameongeza kuwa Estevao alistahili kufurahia mchezo wake, alikuwa na uhusiano mzuri na mashabiki na alikaribia kufunga bao. Amesema winga huyo alipambana hadi mwisho licha ya kuchoka.
Kiwango hicho kinatarajiwa kuongeza shinikizo kwa Alonso kuhakikisha Estevao anaendelea kupata nafasi kikosini na kwamba kiwango hicho hakikuwa cha siku moja tu.