Henry ampigia saluti Lionel Messi
Muktasari:
- England ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Anthony Gordon kabla ya Messi kugeuza kabisa sura ya mchezo kwa kutoa pasi mbili za mabao zilizowapa ushindi mabingwa hao watetezi.
NEW YORK, MAREKANI: NGULI wa Ufaransa, Thierry Henry, ameshindwa kuficha hisia zake baada ya Lionel Messi kuiongoza Argentina kuichapa England mabao 2-1 na kutinga fainali ya Kombe la Dunia.
England ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Anthony Gordon kabla ya Messi kugeuza kabisa sura ya mchezo kwa kutoa pasi mbili za mabao zilizowapa ushindi mabingwa hao watetezi.
Messi alimtengea Enzo Fernandez pasi ya kusawazisha dakika ya 85, kabla ya kutoa krosi iliyomkuta Lautaro Martinez aliyefunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 39 sasa amefikisha mabao manane na asisti nne katika mechi saba za Kombe la Dunia 2026, huku pia akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi kwa mara ya tano kwenye mashindano hayo.
Henry amesema England ilimfanya Messi kuingia katika kiwango cha hatari mara baada ya Argentina kuwa nyuma.
“Usimwamshe mnyama. Nilishawahi kucheza naye Barcelona. Anapofikia hali hiyo huwa hawezi kuzuilika. Timu yake inapomhitaji, hupandisha kiwango na kufanya mambo ya ajabu,” amesema Henry.
Kauli hiyo imeongeza sifa kwa Messi ambaye anaendelea kuonyesha kuwa bado ni mmoja wa wachezaji hatari zaidi duniani licha ya umri wake kuwa mkubwa .