Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Henry ajitetea kwa kashfa ya Ballon d’Or, asema watu wamekuza mambo

HENRY Pict

Muktasari:

  • Henry, aliyekuwa mtangazaji mwenza wa hafla hiyo pamoja na Kate Scott wa CBS Sports, amekosolewa kwa kauli zake zilizowalenga nyota wa Barcelona, Lamine Yamal, mshindi wa tuzo kuu Harry Kane na Scott mwenyewe.

LONDON, ENGLAND: NYOTA wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry, amejitetea dhidi ya ukosoaji alioupata kutokana na namna alivyokuwa akiendesha hafla ya tuzo za Ballon d’Or Jumatatu, akisema watu wamekuza mambo yasiyokuwa na uzito.

Henry, aliyekuwa mtangazaji mwenza wa hafla hiyo pamoja na Kate Scott wa CBS Sports, amekosolewa kwa kauli zake zilizowalenga nyota wa Barcelona, Lamine Yamal, mshindi wa tuzo kuu Harry Kane na Scott mwenyewe.

Akizungumza kupitia video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumatano, Henry alieleza kuwa utani wake kwa Yamal haukuwa na nia ya kumshusha hadhi wala kuumiza hisia zake.

HEN 01

Katika hafla hiyo, Henry alimtania Yamal kuhusu kushinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi kwa mara ya tatu mfululizo, akimuuliza: “Hii ni tuzo yako ya tatu, sivyo? Lakini je, ndiyo tuzo uliyokuwa ukiitamani zaidi?”

Kauli hiyo ilizua mwitikio kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa ukumbini, huku wengine wakimkosoa Henry kwa namna alivyomzungumzia kijana huyo wa Hispania.

Hata hivyo, Henry alisisitiza kuwa anamkubali sana Yamal na angefurahia kumtazama akicheza.

“Mimi ni shabiki mkubwa wa Lamine Yamal. Sikuwa nikijaribu kumshusha hadhi yake hata kidogo. Ninaelewa kama hukupenda utani huo, lakini tafadhali usifanye hivyo. Yeye ni miongoni mwa wachezaji ambao ningelipa fedha ili niwaone wakicheza. Ninampenda,” amesema Henry mwenye umri wa miaka 49.

HEN 02

Pia alijibu ukosoaji kuhusu namna alivyomrekebisha Scott alipotamka jina la nyota wa zamani wa Brazil, Sócrates, akisisitiza kuwa mwenzake huyo alikuwa akishiriki katika utani huo.

Henry alidai Scott alitamka kwa makusudi sehemu ya jina hilo, naye akajibu kwa namna iliyokuwa sehemu ya mzaha wao, hivyo kukataa madai kwamba alimvunjia heshima.

“Hamkuupenda utani huo, ninaelewa, lakini tafadhali acheni kusema kwamba sikumheshimu Kate. Siwezi kufanya hivyo. Mnaweza kumuuliza mwenyewe; alikuwa akishiriki utani huo pamoja nami. Alitamka ‘Soc’ kwa makusudi, nami nikajibu ‘Soc’. Tafadhali acheni kubuni hadithi,” amesema.

Katika hafla hiyo, mshambuliaji wa Arsenal, Bukayo Saka, alishinda tuzo ya Socrates iliyotolewa kwa kutambua mchango wake katika shughuli za kibinadamu na hisani.

HEN 03

Henry pia alimtetea Kane, akisema mshambuliaji huyo alikuwa mshindi anayestahili tuzo ya Ballon d’Or, licha ya yeye mwenyewe kuonyesha wazi kuwa alitaka Mfaransa mwenzake, Kylian Mbappé, ashinde.

“Mimi ni Mfaransa, kwa hiyo nilikuwa lazima kumuunga mkono na kumtetea raia mwenzangu,” amesema Henry.

Ameongeza kuwa alimwambia Kane kuwa anastahili tuzo hiyo na ni mfano unaoonyesha kuwa bidii katika kazi ni kipaji pia.

“Nilimwambia, ‘Unastahili kushinda, unastahili tuzo hii. Wewe ni mfano unaoonyesha kuwa nidhamu ya kazi ni kipaji na kufanya kazi kwa bidii ni kipaji.’ Hongera, Harry Kane. Tangu Kombe la Dunia, nimekuwa nikimwita Sir Harry Kane,” amesema.

HEN 04

Henry alihitimisha kwa kuwataka wakosoaji kutuliza jazba, akisisitiza kuwa anawaheshimu Kane na Yamal na hakukusudia kumvunjia heshima Scott.

“Tafadhali, watu huko nje, tulieni. Ninampenda Harry Kane, ninampenda Lamine Yamal na sikumvunjia heshima Kate. Alikuwa akishiriki utani huo pamoja nami,” amesema Henry.