Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huyu ndiye mkurugenzi wa ufundi Simba SC

MKURUGENZI Pict

Muktasari:

  • Ujio wa Janza unatarajiwa kuongeza nguvu katika benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu, Steve Barker, huku klabu hiyo ikilenga kuwa na mfumo imara wa uendeshaji wa soka unaoweza kuleta ushindani na matokeo chanya.

SIMBA SC imefikia makubaliano ya kumuajiri mtaalamu wa soka kutoka Zambia, Honour Janza (66), kuwa Mkurugenzi mpya wa ufundi wa klabu hiyo, akipewa jukumu la kuimarisha mifumo ya kiufundi na kuongeza ufanisi wa timu hiyo inayoshiriki mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa imefuzu hatua ya makundi kwa mara ya saba tangu 2003.

Ujio wa Janza unatarajiwa kuongeza nguvu katika benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu, Steve Barker, huku klabu hiyo ikilenga kuwa na mfumo imara wa uendeshaji wa soka unaoweza kuleta ushindani na matokeo chanya.

Janza anaingia Simba akiwa na uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, akiwahi kushika nafasi mbalimbali za ukocha na usimamizi wa kiufundi katika timu za taifa na klabu, ikiwemo Zesco United ya Zambia ambako alihudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi kuanzia mwaka 2023 hadi 2026.

Uteuzi huo ni sehemu ya kuimarisha eneo la kiufundi ili kuhakikisha mipango ya usajili, maendeleo ya wachezaji na maandalizi ya timu vinaendana na malengo ya klabu.


MKUR 06

JANZA NI NANI?
Janza ni mzaliwa wa Lusaka nchini Zambia, alikozaliwa Agosti 15, 1960. Katika safari yake ya soka, amejijengea uzoefu kupitia majukumu ya ukocha na usimamizi wa ufundi, akifanya kazi katika mazingira tofauti ya ushindani barani Afrika.

Miongoni mwa sifa zake za kitaaluma ni Leseni B ya Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA) na Leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ambazo ni sehemu ya maandalizi yake katika taaluma ya ukocha.

Uzoefu wake unajumuisha kuinoa timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo, pamoja na kufanya kazi katika klabu mbalimbali za Zambia na Tanzania, huku pia akiwa miongoni mwa wakufunzi wa makocha wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).


MKUR 05

CHIPOLOPOLO ILIMPA JUKUMU KUBWA
Safari ya Janza katika ngazi ya timu ya taifa ilianza kwa majukumu ya kukuza vipaji na baadaye kuingia katika benchi la ufundi la kikosi cha wakubwa cha Zambia maarufu Chipolopolo.

Mwaka 2009 hadi 2010 alikuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Zambia chini ya umri wa miaka 20, kabla ya kuteuliwa kuwa Kocha Msaidizi wa Chipolopolo kuanzia mwaka 2011 hadi 2014.

Mwaka 2014 alipandishwa kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2015. Katika kipindi hicho, aliiongoza Zambia kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizofanyika Equatorial Guinea mwaka 2015.

Mbali na majukumu ya benchi la ufundi, Janza alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ) kuanzia mwaka 2009 hadi 2017, nafasi iliyompa uzoefu katika kupanga na kusimamia maendeleo ya soka kwa mtazamo mpana zaidi ya timu moja.

Pia amewahi kuwa Kocha Mkuu wa muda wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, uteuzi uliofanyika Agosti 2022.


MKUR 04

SAFARI YAKE YA KLABU
Baada ya kufanya kazi katika ngazi ya timu ya taifa, Janza aliendelea na majukumu mbalimbali ya ukocha na usimamizi wa kiufundi katika klabu za Afrika.

Mwaka 2017 hadi 2018 alikuwa Kocha Mkuu wa Red Arrows ya Zambia, kabla ya kwenda Mbabane Swallows ya Eswatini ambako alihudumu katika nafasi hiyo kuanzia mwaka 2019 hadi 2020.

Mwaka 2020 hadi 2021, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa NAPSA FC ya Zambia, akirejea katika jukumu la kusimamia masuala ya kiufundi ya klabu.

Mwaka 2021 hadi 2022, alijiunga na Namungo FC ya Tanzania akiwa Kocha Mkuu. Kipindi hicho kilimpa nafasi ya kufanya kazi katika Ligi Kuu Tanzania Bara na kufahamu mazingira ya soka la hapa nchini.

Baada ya kuondoka Namungo, Janza aliendelea na safari yake nchini Zambia, akijiunga na Zesco United mwaka 2023 kama Mkurugenzi wa Ufundi, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2026 kabla ya kufikia makubaliano ya kujiunga na Simba.

Hivyo kwa Tanzania, si mgeni akiwa amefundisha klabu na timj ya taifa. Pia mara kadhaa amekuwa pale Kituo cha Ufundi cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kilichopo Mnyanjani jijini Tanga akiwanoa makocha mbalimbali.

MKUR 03

SIMBA IMEMCHUKUA KWA AJILI YA NINI?
Katika muundo wa klabu za kisasa, Mkurugenzi wa Ufundi ana jukumu muhimu la kuhakikisha uamuzi wa kiufundi unafuata dira moja na unajenga msingi wa mafanikio ya muda mrefu.

Janza anatarajiwa kushirikiana na Barker na viongozi wengine wa Simba katika kuimarisha mfumo wa timu, kutambua mahitaji ya kikosi na kushauri kuhusu usajili wa wachezaji wanaoweza kuongeza ushindani.

Pia, uzoefu wake unaweza kutumika katika kuimarisha utambuzi wa vipaji, kuweka misingi ya falsafa ya mchezo na kusaidia maendeleo ya wachezaji wa vijana ili waweze kupata nafasi katika kikosi cha wakubwa.

Hata hivyo, majukumu halisi ya Janza yatategemea mgawanyo wa kazi utakaowekwa na uongozi wa Simba, hasa katika ushirikiano wake na Kocha Mkuu na kitengo cha usajili.

MKUR 02

BARKER APATA NGUVU NYINGINE
Ujio wa Janza unaongeza mtaalamu mwingine katika muundo wa kiufundi wa Simba, wakati Barker akiendelea na jukumu la kuandaa kikosi kwa ajili ya mashindano yanayoikabili klabu hiyo.

Ushirikiano kati ya Mkurugenzi wa Ufundi na Kocha Mkuu unaweza kuwa muhimu katika kuhakikisha mahitaji ya kikosi yanaeleweka, usajili unafanyika kwa kuzingatia mahitaji halisi na maandalizi ya timu yanaendana na malengo ya msimu.

Kwa kuwa Janza amewahi kufanya kazi katika soka la Zambia na Tanzania, anatarajiwa kutumia uzoefu huo kusaidia Simba kukabiliana na changamoto za ushindani wa ndani na wa kimataifa.


MKUR 01

MTIHANI WAKE MSIMBAZI
Pamoja na uzoefu wake wa zaidi ya muongo mmoja katika majukumu tofauti ya soka, Janza anakabiliwa na matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki wa Simba, ambao wanataka kuona timu yao ikifanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Changamoto yake haitakuwa tu kusaidia timu kupata matokeo ya haraka, bali pia kujenga mfumo wa kiufundi unaoweza kuendeleza mafanikio kwa muda mrefu.

Ubora wa usajili, maendeleo ya vijana, ushirikiano na benchi la ufundi na uwezo wa klabu kutekeleza mipango yake vitakuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya kupima mchango wake.

Matarajio ya Simba ni kwamba uzoefu wa Janza utasaidia kuimarisha muundo wa kiufundi na kuongeza ushindani wa Wekundu wa Msimbazi katika safari yao ya kutafuta mafanikio ya ndani na ya kimataifa.