Hela yaongezwa kumnasa Mbeumo

Muktasari:
- Man United ilishuhudia ofa yao ya kwanza ya Pauni 55 milioni ikikataliwa na Brentford kwa ajili ya fowadi huyo Mcamerooni, ambaye pia amekuwa akiwindwa na kocha wake wa zamani, Thomas Frank huko Tottenham Hotspur. Newcastle pia inahitaji saini yake.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Manchester United imepeleka ofa ya pili huko Brentford kwa ajili ya kuinasa saini ya winga Bryan Mbeumo na mzigo uliowekwa mezani unazidi mkwanja wa Pauni 60 milioni.
Man United ilishuhudia ofa yao ya kwanza ya Pauni 55 milioni ikikataliwa na Brentford kwa ajili ya fowadi huyo Mcamerooni, ambaye pia amekuwa akiwindwa na kocha wake wa zamani, Thomas Frank huko Tottenham Hotspur. Newcastle pia inahitaji saini yake.
Mbeumo, 25, anatazamwa kama mchezaji anayewindwa kwa nguvu zote na Kocha wa Man United, Ruben Amorim dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya miamba hiyo ya Old Trafford kufunga mabao 44 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita
Mabosi wa Brentford wanaaminika watakuwa tayari kufanya mazungumzo endapo kama ofa yao itaongezeka baada ya klabu hiyo ya London Magharibi kugomea ofa ya awali ya Pauni 45 milioni jumlisha na nyongeza ya Pauni 10 milioni.
Mbeumo amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake huko Brentford na hilo linaifanya Man United kuwa na matumaini ya kunasa saini yake na kumvuta staa huyo Carrington kwa ajili ya mechi za pre-season kuanzia wiki inayoanzia Julai 7.
Amorim anamtaka Mbeumo akaongoze safu ya ushambuliaji sambamba na Matheus Cunha, ambaye alishanaswa na miamba hiyo kwa ada ya Pauni 62.5 milioni akitokea Wolves. Man United itahitaji pia mshambuliaji wa kati na kwenye hilo baada ya kuhusishwa sana na wakali kama Viktor Gyokeres na Victor Osimhen, ripoti sasa zinafichua mipango imehamia kwa straika wa Chelsea, Christopher Nkunku, akisakwa dirisha hili la majira ya kiangazi ili akakipige Old Trafford.
Fowadi huyo Mfaransa alikuwa kwenye rada za kocha Amorim kwenye dirisha la Januari, alipomtaka aje kwenye timu yake kama suluhisho la kipindi kifupi la kwanza kumaliza tatizo la ufungaji katika timu yake. Na wiki za karibuni amekuwa akifukuzia saini ya mchezaji huyo kwa kuzungumza na Chelsea pamoja na mawakala wa mshambuliaji huyo.
Chelsea wanataka kuachana na Nkunku baada ya kuipiku Man United kwenye usajili wa Liam Delap. Januari mazungumzo yalikuwa kama Chelsea itakuwa tayari kumchukua Alejandro Garnacho, ili apishane na Nkunku mlangoni.
Garnacho yupo sokoni kwa sasa baada ya kuwatibua mashabiki wa Man United kwa kitendo cha kuvaa jezi ya Aston Villa yenye jina la Marcus Rashford wakati akiwa mapumzikoni - na amekuwa akihusishwa pia na The Blues.
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca aliulizwa kuhusu hatima ya Nkunku huko Marekani kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu kabla ya timu yake kumenyana na Esperance ya Tunisia, alisema: “Chris yupo na sisi. Ni mchezaji wetu. Alifanya vizuri kwa siku nne au tano zilizopita, hivyo tunaweza kufikiria kumpa nafasi.”