Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Harry Kane sasa ataka Ballon d’Or

KANE Pict

Muktasari:

  • Kane, mwenye umri wa miaka 33, yupo katika kiwango bora zaidi cha maisha yake ya soka na sasa anaamini ana nafasi ya kutwaa tuzo hiyo inayotolewa kwa mchezaji bora zaidi duniani.

MUNICH, UJERUMANI: NAHODHA wa England na mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, amesema hana mpango wa kuweka ukomo katika malengo yake ya soka, huku sasa akitaka kutwaa tuzo ya Ballon d’Or baada ya msimu wa kihistoria uliomshuhudia akifunga mabao 73.

Kane, mwenye umri wa miaka 33, yupo katika kiwango bora zaidi cha maisha yake ya soka na sasa anaamini ana nafasi ya kutwaa tuzo hiyo inayotolewa kwa mchezaji bora zaidi duniani.

Nyota huyo wa Bayern pia amefichua kuwa bado ana hamu ya kushinda mataji makubwa katika ngazi ya klabu na taifa, akiwamo kuiongoza England kufikia mafanikio makubwa.

Akizungumza na TNT Sports kuelekea kampeni ya Bayern katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kane amesema huwa hapendi kujiwekea mipaka kabla ya kuanza msimu mpya.

“Sipendi kuweka ukomo wa kile ninachoweza kufanikisha kabla ya kila msimu. Wakati mwingine hujiwekea lengo kubwa sana na kuona ninaweza kufanya nini,” amesema Kane.

KAN 01

Msimu uliopita, Kane alifunga mabao 73, idadi ambayo ilikuwa karibu mabao 20 zaidi ya rekodi yake bora ya awali.

Mshambuliaji huyo amesema anataka kuendelea kucheza katika kiwango cha juu kwa muda mrefu, akitoa mfano wa mastaa kama Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Luka Modric ambao wameendelea kucheza hadi umri mkubwa.

“Unapowaona wachezaji kama Messi, Ronaldo na Modric wakiendelea kucheza hadi mwishoni mwa miaka yao ya 30, au Ronaldo na Modric wakiwa kwenye miaka yao ya 40, inanipa motisha ya kuamini kwamba na mimi naweza kufanya hivyo,” amesema.

Kane pia amesisitiza kuwa mafanikio ya baadaye yatategemea zaidi hamu na mawazo ya mchezaji, pamoja na malengo ambayo bado anataka kuyafikia.

KAN 02

Kwa sasa, anasema Bayern inampa nafasi nzuri ya kuendelea kupigania mataji ya Bundesliga na Ligi ya Mabingwa kila msimu.


BALLON D’OR YAMVUTIA

Licha ya msimu wake bora, Kane amesema anatambua kuwa ushindi wa Ballon d’Or hautegemei yeye pekee, bali kura na maamuzi ya wapiga kura wa tuzo hiyo.

England haijapata mshindi wa Ballon d’Or tangu Michael Owen alipoutwaa mwaka 2001. Owen tayari ameuelezea msimu wa Kane kuwa “mchezaji wa kiwango cha ajabu”, huku akitamani kumkaribisha nahodha huyo wa England katika kundi lake la kipekee la washindi.

Kane amesema anajivunia hatua aliyofikia, hasa akikumbuka kuwa zamani alikuwa shabiki aliyekuwa akiota siku moja kuwa mchezaji wa kulipwa.

KAN 03

“Najivunia sana msimu niliokuwa nao. Sio muda mrefu uliopita nilikuwa shabiki niliyetamani kuwa mchezaji wa kulipwa. Sasa niko hapa, nashinda tuzo kama Golden Shoe, na Ballon d’Or pia iko kwenye mjadala,” amesema.

Hata hivyo, Kane amesema kwa sasa hawezi kuamua hatma ya tuzo hiyo kwa kuwa uamuzi uko mikononi mwa wapiga kura.

“Ni jambo ambalo sasa haliko mikononi mwangu. Ni juu ya wapiga kura na watu wanaoamua. Msimu niliokuwa nao ulikuwa bora zaidi katika maisha yangu, hivyo tunapaswa kusubiri na kuona,” ameongeza.


LIGI YA MABINGWA

Mbali na Ballon d’Or, Kane ana kiu kubwa ya kuisaidia Bayern Munich kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Bayern ilifika hatua ya nusu fainali msimu uliopita kabla ya kutolewa na Paris Saint-Germain, ambayo baadaye ilitwaa ubingwa. Katika msimu wa kwanza wa Kane, Bayern ilitolewa hatua hiyo na Real Madrid, huku msimu uliofuata ikikwazwa na Inter Milan.

Bayern haijawahi kutwaa Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2020, lakini Kane anaamini safari hii wana nafasi kubwa ya kwenda mbali zaidi.

KAN 04

“Tunakaribia sana. Msimu uliopita tofauti ilikuwa ndogo sana. Tulitolewa na timu ambayo imetwaa Ligi ya Mabingwa mara mbili mfululizo, hivyo hakuna aibu,” amesema.

“Tunauingia msimu huu tukiwa na mtazamo kwamba huu lazima uwe mwaka wetu. Tunahitaji kutafuta njia ya kuhakikisha tunamaliza kazi.”

Kane anaamini kadri kocha Vincent Kompany anavyoendelea kubaki Bayern, ndivyo timu hiyo inavyozidi kuimarika kutokana na wachezaji kufahamiana zaidi na kujenga uelewano ndani ya uwanja.

Kwa sasa, Kane anaonekana kuwa na malengo mawili makubwa: kutwaa Ballon d’Or na kuisaidia Bayern Munich kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku ndoto yake ya kuipa England mafanikio makubwa kimataifa ikiwa bado haiishi.