Guardiola atoa kauli "sitaki aibu"

Muktasari:
- Sasa unaambiwa, kasema wakati wowote anasepa klabuni hapo kama mambo yataendelea kwenda ndivyo sivyo ili kukwepa aibu.
MANCHESTER, ENGLAND: ACHANA na mchezo wa jana wa Liverpool dhidi ya Manchester City, si unakumbuka ni juzi kati tu Pep Guardiola aliongeza mkataba wa kuendelea kuifundisha City hadi mwaka 2026?
Sasa unaambiwa, kasema wakati wowote anasepa klabuni hapo kama mambo yataendelea kwenda ndivyo sivyo ili kukwepa aibu.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja, Guardiola amekuwa akipitia kipindi kigumu cha maisha yake ya ukocha baada ya kupoteza mechi tano na kutoa sare moja katika mechi zao sita za mwisho.
Kocha huyu hakuwahi kupata matokeo mabaya kiasi hiki katika maisha yake ya ukocha hali inayosababisha atamani kuondoka ili kuondokana na aibu hiyo.
Fundi huyu kutoka Hispania inadaiwa ameshafanya hadi kikao na mabosi wakubwa wa timu hiyo kujadili hali ya timu na nini kifanyike.
“Bado niko na furaha na nataka kuendelea kujaribu kuweka mambo sawa, lakini sitaki kukaa mahali nahisi mimi ni tatizo. Sitaki kukaa hapa kwa sababu tu nina mkataba. Rais wangu anajua hilo. Nilimwambia, ‘Nipe nafasi ya kujaribu kurudisha hali ya timu kawaida’, na hususani pale wakati kila mchezaji atarudi kutoka kwenye majeraha,” alisema Guardiola.
“Baada ya wachezaji kurudi kutoka kwenye majeraha tutaona kile kitakachotokea, baada ya hapo, ikiwa mambo yataendelea kuwa mabaya, nitahitaji kuondoka kwa sababu haitokuwa na maana ya kile nilichofanya kwa miaka tisa iliyopita.”
“Ni muda mrefu sana, sikuwahi kuwaambia mabosi nahitaji kupewa muda, sio rahisi kusema hivyo lakini naamini nahitaji muda kwa sababu bado nina kazi ya kufanya.”
“Niliwahi kuwa Barcelona. Naweza kusema ni timu yangu, mahali nilikozaliwa. Nilikuwa huko kwa miaka minne, nilishinda mataji 14. Nilikuwa na Messi, mchezaji bora wa wakati wote. Neymar alikuwa anakuja kwenye timu lakini bado nikasema ‘naondoka’.
“Watu walikuwa wanajiuliza, ‘Kwa nini unaondoka kwenye mji ambao ulizaliwa na una wachezaji kibao wa kizazi bora kama Xavi, Iniesta, Puyol, ambao walitamba sana duniani na hata kushinda Kombe la Dunia na Kombe la Ulaya?’ Niliwaambia naondoka kwa sababu nilijisikia kufanya hivyo, hata hapa pia ni hivyo hivyo, niliongeza mkataba kwa sababu nilijisikia kuongeza, sio kwa sababu ya kile nilichofanya hapo awali au kikosi nilichonacho.”
Baada ya mchezo wao dhidi ya Liverpool jana, Manchester City itakuwa na ratiba nyingine ngumu zaidi katika mechi zao tano zijazo za michuano yote na itaanza dhidi ya Nottingham Forest ambayo tangu kuanza kwa msimu huu imeonyesha kiwango bora, pia itavaana na Crystal Palace ambayo haionekani kuwa ngumu sana lakini tatu zilizobakia ambazo ni dhidi ya Juventus katika Ligi ya Mabingwa na Ligi Kuu England mbele ya Manchester United na Aston Villa.