Graeme Souness: Manchester United wa kawaida sana
Muktasari:
- Mashetani Wekundu walipoteza pointi katika mechi ya tatu mfululizo ya nyumbani ya Ligi Kuu Jumatatu usiku, baada ya kutoa sare ya mabao 4-4 katika mechi iliyokuwa ya kusisimua dhidi Bournemouth.
MANCHESTER, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa Liverpool, Graeme Souness amesema kuwa suala la Manchester United kumaliza ndani ya nafasi nne za juu na kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya bado ni ndoto kwani ni timu ya kawaida sana.
Mashetani Wekundu walipoteza pointi katika mechi ya tatu mfululizo ya nyumbani ya Ligi Kuu Jumatatu usiku, baada ya kutoa sare ya mabao 4-4 katika mechi iliyokuwa ya kusisimua dhidi Bournemouth.
Matokeo hayo yaliifanya Man United kuendelea kubakia katika nafasi ya sita na kushindwa kuzishusha Crystal Palace na Chelsea zilizopo katika nafasi ya nne na ya tano.
Souness, ambaye amewahi pia kukosoa uamuzi wa kuajiriwa kwa Amorim hapo awali, amesema haoni mazingira yoyote ambayo yatawawezesha mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu England kuingia kwenye nafasi nne za juu msimu huu.
“Manchester United bado ni timu ya kawaida,” amesema Souness alipokuwa akizungumza na Sky Bet.
“Je, ni kosa la Ruben Amorim? Hapana. Kwangu Matheus Cunha na Bryan Mbeumo ni wachezaji wazuri, lakini wengine ni wa kiwango cha kawaida, hivyo sioni wakimaliza katika Top 4.”
“Manchester United ni klabu kubwa zaidi kwenye soka letu, labda ya pili au ya tatu kwa ukubwa duniani. Lakini kwa sasa wanapitia kipindi kigumu. Ili kurejea katika makali yao kwanza wanahitaji kurejea katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ambako huko watakuwa na mapato zaidi, watanunua wachezaji bora zaidi, na kuvutia nyota wakubwa waliopo sokoni.”
Man United ilifanya maboresho makubwa katika kikosi chake katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, baada ya kuwasajili Mbeumo, Cunha na Benjamin Sesko kwa jumla ya Pauni 214 milioni.
Hata hivyo, ukosefu wa safu bora ya ulinzi unaonekana kuwa ni tatizo kubwa na ameweka wazi kwamba kukosekana kwa mwendelezo wa matokeo mazuri ni mtihani mwingine ambao Amorim anatakiwa aujibu.
“Tatizo alilonalo Ruben Amorim na wachezaji wake ni kwamba hajui wachezaji wataamkaje. Hajui ni Manchester United ipi itaonekana, leo wanaweza kucheza vizuri lakini kesho wakaharibu, hilo sio jambo zuri. Ni mbaya sana kocha ukiwa katika hali hiyo.”
“Unaweza kukaa chumba cha kubadilishia nguo kama kocha au meneja, ukawaangalia wachezaji wako kabla ya mechi na kufikiria, ‘Leo wote wako tayari, tutakuwa na siku nzuri’. Halafu wanaingia uwanjani na wasionyeshe kiwango bora.”