Fernandes: Wanataka kuniuza!
Muktasari:
- Staa huyo fundi wa mpira kutoka Ureno, Fernandes, 31, wakati wa dirisha lililopita la majira ya kiangazi alihusishwa sana na klabu za Saudi Arabia huku jina lake likiendelea kutajwatajwa katika kuelekea uhamisho wa Januari.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO wa boli na nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes amesema bosi wa timu hiyo alitaka kumpiga bei kwenye dirisha la majira ya kiangazi na kwamba mazungumzo yake na kigogo huyo bado yanamuumiza hadi sasa.
Staa huyo fundi wa mpira kutoka Ureno, Fernandes, 31, wakati wa dirisha lililopita la majira ya kiangazi alihusishwa sana na klabu za Saudi Arabia huku jina lake likiendelea kutajwatajwa katika kuelekea uhamisho wa Januari.
Ofa ya Pauni 80 milioni iliwekwa mezani kutoka Al-Hilal wakati Man United ilipokuwa kwenye ziara Mei baada ya msimu wa Ligi Kuu England kumalizika.
Fernandes alisema kwamba amebaki Man United kwa sababu anaipenda timu hiyo na hilo pia limechangiwa na mazungumzo yake ya ana kwa ana na kocha Ruben Amorim.
Lakini, nahodha huyo hawezi kusahau kile alichoelezwa na mabosi wa Old Trafford kwa sababu walitamani kupata pesa na kwamba walikuwa tayari kumuuza kiungo huyo.
Fernandes aliiambia Canal 11: “Kutoka upande wa klabu, ilionekana ni kama vile, ‘kama utaondoka, haitakuwa mbaya kwetu.’ Iliniumiza sana. Zaidi ya kuniumiza, ilinihuzunisha sana kwa sababu mimi ni mchezaji ambaye sipendi kukosoa kitu. Siku zote nipo kwa ajili ya timu, siku zote nacheza iwe vizuri au vibaya. Najitoa kwa kila kitu.
“Lakini, ilifika wakati kwa upande wao, pesa ni kitu muhimu kuliko chochote. Klabu ilitaka niondoke, hilo lipo akilini mwangu. Niliwaambia wakurugenzi jambo hilo, lakini nadhani walikosa ujasiri wa kutimiza lengo hilo kwa sababu kocha alinihitaji. Kama ningesema nataka kuondoka, basi wangeniacha niondoke.”
Mkataba wa Fernandes unaripotiwa kuwa na kipengele kinachomruhusu mchezaji huyo kuuzwa endapo kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kulipa Pauni 57 milioni hasa kwa klabu za ng’ambo na kipengele hicho kitafanya kazi hadi mwakani.
Staa huyo wa Ureno amehusika kwenye mabao 11 katika mechi 16 za Ligi Kuu England alizocheza msimu huu na alitikisa nyavu kwenye sare ya 4-4 dhidi ya Bournemouth uwanjani Old Trafford usiku wa Jumatatu iliyopita.
Lakini, namba hizo bado hazimfanyi Fernandes kuondoka kwenye presha ya kupigwa bei kutokana na mabosi kuhitaji pesa.
Fernandes alisema: “Kwa sasa najiona kama barafu nyembamba. Hapa England, mchezaji anapofikisha umri wa miaka 30, wanaanza kufikiria kuanza upya. Ni kama samani za ndani tu. Ishu ya kuwa mtiifu haitazamwi kama muhimu tofauti na zamani. Ningeweza kuondoka kwenye dirisha lililopita. Ningevuna pesa nyingi. Nilikuwa naondoka msimu uliopita, sisemi wapi, lakini ningeshinda mataji mengi pia msimu uliopita.”
“Niliamua kubaki kwa sababu za kifamilia, lakini pia ni kwa sababu nampenda klabu kwa moyo wote. Mazungumzo ya kocha pia yalinishawishi kubaki.”
Fernandes aliongeza: “Kama siku moja nitaamua kwenda kucheza Saudi Arabia, nitafanya hivyo. Staili yangu ya maisha itabadilika, wanangu watakwenda kuishi kwenye eneo lenye jua baada ya miaka sita kukaa kwenye baridi na mvua nyingi Manchester. Nitakwenda kuishi kwenye ligi inayokua na yenye wachezaji wanaojiweza.”