Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabosi Simba, Yanga wacheza kamari eneo la ulinzi


ZIMEBAKI siku 13 tu kabla usajili wa majembe mapya haujafungwa huku timu za Simba na Yanga zikiwa zimesajili mastaa kibao, lakini zikichunia eneo la ulinzi ambalo ni muhimu kwa timu hizo.


Usajili kwa ajili ya wachezaji wapya kwenye Ligi Kuu Bara, Championship pamoja na First League unatarajiwa kufungwa Agosti 15 mwaka huu, ikiwa ni siku moja tu tangu ligi hiyo itakapokuwa imeanza. Timu za Simba na Yanga zimekuwa na presha kubwa ya kuboresha vikosi vyao, Simba ikiwa inataka kurudisha ufalme wake wa kuchukua makombe makubwa, huku Yanga ikiendelea kuboresha kikosi chake ili iendeleze utawala kwenye ligi baada ya kuchukua ubingwa mara tano mfululizo.

Hata hivyo, timu zote zimeonekana kuboresha vikosi vyao, Simba imesajiliwa mastaa wapya sita hadi sasa ambao ni Kelvin Nashon, Nathaniel Chilambo, Bakari Msimu, Ibrahim Doumbia, Keletso Makgalwa na Ibraheem Jabaar, watatu ni wazawa na watatu kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wa Yanga, yenyewe imeshusha kundi kubwa zaidi la mastaa, baada ya hadi sasa kuwa imeshasajili wachezaji kumi wapya, achana na kiungo mkabaji ambaye walitarajia kumshusha usiku wa kuamkia leo, wachezaji wapya Yanga zikiwa zimebaki siku chache usajili ufungwe ni Juma Issa Abushiri, Hussein Juma Mihambo, Abdulnasir Assa ‘Gamal’ Mohamed Mussa, Erick Mwijage, Cheikh Ibrahima Toure, Albert Kangwanda, Housseine Zakouani, Suleiman Mbarouk na Peter Shalulile.

Katika kundi hilo, Yanga imesajili wachezaji watano wazawa, lakini pia ikiwa imesajili watano wageni ili kuhakikisha kuwa timu hiyo inafanya vizuri msimu ujao wa ligi. Hata hivyo, vikosi vyote vimeonekana kuwa na imani kuwa na maeneo yao ya ulinzi wa kati pamoja na makipa wao kukiwa hadi sasa hakuna mchezaji yeyote mkubwa ambaye amesajiliwa kwenye maeneo hayo hali ambayo inaonyesha kuwa mabosi wa timu hizo wameridhishwa na kile ambacho kilitokea msimu uliopita.

Katika usajili huu, Yanga imemsajili beki wa kati kutoka Mashujaa Mohamed Mussa lakini anaonekana kuwa msaidizi wa wale waliopo baada ya Yanga kuwategemea zaidi, Ibrahim Hamad Bacca, Dickson Job pamoja na Bakari Mwamnyeto kwenye eneo hilo ambalo ni mhimili muhimu kwenye timu, hakuna shida kwenye makipa endapo Djigui Diarra atakuwa fiti msimu mzima.

Mastaa hao ambao wamekuwa panga pangua kwenye timu hiyo kwa misimu kadhaa, msimu uliopita kwenye ligi waliruhusu mabao tisa, huku Job akikosekana kwenye michezo kadhaa kutokana na kusumbuliwa na majeraha, Bacca akikosekana kwenye michezo kadhaa kutokana na kufungiwa mechi tano kutokana na utovu wa nidhamu hali hiyo ilimfanya Mwamnyeto ambaye amekuwa haaminiki sana kwenye kikosi hicho kucheza baadhi ya michezo muhimu. Kutokana na taarifa kuwa Frank Assinki ambaye alisajiliwa kutoka Singida BS anaweza kurudi kwenye timu yake ya zamani, Yanga itategemea zaidi ubora na utimamu wa walinzi wake watatu, Job ambaye bado hayupo fiti kwa asilimia 100, Mwamnyeto ambaye mkataba wake umemalizika lakini klabu hiyo imeshatoa taarifa kuwa atapewa mkataba mpya pamoja na Bacca ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kwa misimu ya hivi karibuni, shida itakuwa endapo mmoja kati yao atakuwa nje.


ANGALIZO

Ili kuwa na kikosi imara kinachoweza kushiriki michuano mbalimbali ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga inalazimika kuwa na beki mwingine wa kati mwenye uzoefu wa kimataifa anayeweza kuisaidia kwenye mchezo ambao mlinzi mmoja kati ya Bacca au Job atakosekana, lakini pia wakati mwingine kuwapumzisha kutokana na ratiba kubana kwa kuwa kuna michuano ya Kombe la Mataifa Afrika mwakani, mashindano ambayo yanaandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda hivyo yanalazimisha kila kitu kwenda kwa kasi kubwa.

Kwa upande wa Simba, hawana sababu yoyote ya kuziba masikio kwenye eneo la ulinzi wa kati pamoja na kipa kutokana na msimu uliopita pekee kuruhusu mabao 11, ikiwa ni timu ya pili nyuma ya Yanga iliyoruhusu mabao mengi. Kiuhalisia eneo la ulinzi kwa ujumla limekuwa tatizo kubwa kwa Simba na linawezekana limechangia kwa sehemu kubwa timu hiyo kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu mitano mfululizo, msimu uliopita timu hiyo ilikuwa na walinzi wawili tu bora, Rushine de Reuck pamoja na Olivier Toure, hakukuwa na mbadala zaidi kwa mabeki hao na hofu ilikuwa kubwa endapo mmoja wao angekosekana kutokana na walinzi wengine Abdulrazack Hamza na Wilson Nangu kuwa nje karibu msimu mzima kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Hofu kwa Simba ilikuwa ni endapo Rushine atakosekana kwenye timu hiyo na mashabiki walikuwa wanashika kichwa kila alipokuwa akipata majeraha kwa kuwa pia iliwachukua muda mashabiki wa timu hiyo kukubali kiwango cha Toure, kipa Mamadou Kassali pamoja na kutumika msimu uliopita, bado anaonekana kuwa anahitaji msaidizi sahihi ambaye anaweza kumpa presha ili apunguze baadhi ya makosa.

Endapo Simba itakuwa inamtegemea Hussein Abel kuwa kipa msaidizi msimu ujao, litakuwa tatizo lingine kwa kuwa kipa huyo hajapata nafasi mara kwa mara kwenye timu hiyo, na kama wakikosekana wote atadaka nani, hakuna sababu yoyote zaidi ya Simba kusajili kipa imara.


ANGALIZO

Inawezekana Simba inaamini kuwa Nangu au Hamza mmoja wao anaweza kurejea kikosini haraka, lakini hii ni sawa na kucheza kamari kwa kuwa wachezaji hao wameshakaa nje kwa muda mrefu jambo ambalo linaonyesha kuwa wanaweza wasirudi kwenye ubora.

Kutokana na kuzidiwa na Yanga kwa mabao waliyoruhusu kwa misimu yote mitano mfululizo, hii ni picha kuwa sehemu pekee iliyoinyima Simba ubingwa kwenye kipindi chote ni eneo la ulinzi, hivyo walitakiwa kuhakikisha sehemu hii inakuwa imara tofauti na hali halisi. Endapo Simba haitafanya usajili wa beki wa kati mwenye uzoefu wa kutosha na kuamini kuwa Vedastus Masinde anaweza kuwa mbadala wa Toure na Rushine, kuna uwezekano wakawa na wakati mgumu zaidi endapo mmoja kati yaao tegemeo atakuwa nje kwa sababu yoyote ile.


WAPYA SIMBA

Simba imewasajili Kelvin Nashon (Pamba Jiji) kiungo mkabaji, Nathaniel Chilambo (Azam FC) beki wa kulia, Bakari Msimu (Coastal Union) kiungo mshambuliaji, Ibrahim Doumbia (AS Korofina) mshambuliaji, Keletso Makgalwa (Sekhukhune United FC) kiungo mshambuliaji na Ibraheem Jabaar (Stellenbosch FC) kiungo mshambuliaji.


WAPYA YANGA

Juma Issa Abushiri (Fountain Gate) kiungo mshambuliaji, Hussein Mihambo (Mashujaa) mshambuliaji, Abdulnasir Assa ‘Gamal’ (Mashujaa) beki wa kulia, Mohamed Mussa (Mashujaa) beki wa kati na  Erick Mwijage (KMC) kiungo mshambuliaji.

Wengine ni Cheikh Ibrahima Toure (Al-Jabalain) mshambuliaji, Albert Kangwanda (Red Arrows) kiungo mshambuliaji, Housseine Zakouani (Al-Zulfi) kiungo mshambuliaji, Suleiman Mbarouk (JKU) kiungo mshambuliaji na Peter Shalulile (Mamelodi Sundowns) mshambuliaji.