Frank Lampard aifufua Coventry City
Muktasari:
- Ushindi huo wa mabao 1-0 dhidi ya Sunderland ulipatikana kupitia kichwa cha John Hartson, mbele ya mashabiki 20,946 kwenye Uwanja wa Highfield Road, wakati timu hiyo ikiwa chini ya kocha Gordon Strachan.
COVENTRY, ENGLAND: MWAKA 2001, kundi la muziki la Hear'Say lilikuwa kileleni mwa chati za muziki, mchezo wa nyoka kwenye simu ulikuwa gumzo na Tony Blair akiwa Waziri Mkuu wa Uingereza.
Lakini Aprili mwaka huo, ilipata ushindi wake wa mwisho katika Ligi Kuu England, kabla ya kusubiri kwa miaka 25 ili kurejea kwenye kilele cha soka la nchi hiyo.
Ushindi huo wa mabao 1-0 dhidi ya Sunderland ulipatikana kupitia kichwa cha John Hartson, mbele ya mashabiki 20,946 kwenye Uwanja wa Highfield Road, wakati timu hiyo ikiwa chini ya kocha Gordon Strachan.
Tangu siku hiyo, Coventry imepitia safari yenye misukosuko mikubwa, kuiita safari ya kupanda na kushuka inaweza kuwa ni kupunguza uzito wa yaliyotokea.
Mwisho wa msimu wa 2000/01, ilishuka daraja na kutumia misimu 11 iliyofuata katika daraja la pili, kabla ya kushuka tena hadi League One mwaka 2012.
Baadaye, klabu hiyo iliingia katika kipindi kigumu kilichohusisha adhabu za kupunguziwa pointi na kuwekwa chini ya usimamizi wa kiutawala kutokana na matatizo ya kifedha.
Baada ya kuondoka Highfield Road mwaka 2005, Coventry ilijikuta katika mgogoro mkali kuhusu Uwanja wa Ricoh na suala la kodi mwaka 2013.
Hali ilifikia hatua mbaya zaidi ilipolazimika kucheza mechi zake nje ya mji wa Coventry, kwenye Uwanja wa Northampton Town, kabla ya kushuka hadi daraja la nne kwa mara ya kwanza baada ya miaka 59 mwaka 2017.
Bila shaka, baadhi ya mashabiki waliojazana katika jukwaa la Bridgford Stand kwenye Uwanja wa City Ground Jumamosi walikuwa miongoni mwa walioshuhudia miaka hiyo migumu ya Coventry.
Hivyo, shangwe na mlipuko wa hisia baada ya filimbi ya mwisho, kufuatia bao la Jay Dasilva lililoamua mchezo, vilionekana kama kuwasili kwa Coventry kwenye kipindi cha furaha baada ya miaka ya mateso.
“Tumekuwa na mwanzo mgumu, hivyo kupata pointi zetu za kwanza za Ligi Kuu ni jambo kubwa kwetu,” amesema kocha wa Coventry, Frank Lampard.
“Niliwaona wachezaji wakifanya vizuri. Walionyesha mapambano, bidii, umoja na pia uelewa wa kiufundi. Walipambana kwa ajili ya kila mmoja, na hilo ndilo unalohitaji ili kushinda mchezo wa Ligi Kuu.”
‘TUBAKI NA MIGUU CHINI’
Coventry ilikuwa imekwama kwenye ushindi 99 wa Ligi Kuu kwa zaidi ya robo karne, kabla ya ushindi huo kuiwezesha kufikisha ushindi 100 hatimaye.
Lampard anatumaini ushindi huo unaweza kuwa hatua muhimu katika msimu ambao lengo kuu la klabu ni kuepuka kushuka daraja.
“Ni muhimu kwa baadhi ya wachezaji,” amesema Lampard.
“Kwa wengi wao, huu ni mwanzo wao wa kucheza Ligi Kuu. Hawajawahi kuwa hapa kabla, hivyo wanahitaji kujisikia kuwa wanastahili kuwa katika kiwango hiki na kucheza kwa mtazamo huo.”
Lampard alikiri kuwa wachezaji wake wanapaswa kuwa na ustahimilivu wa kukabiliana na changamoto za msimu mrefu wa Ligi Kuu.
Ushindi huo uliopatikana baada ya kichapo cha mabao 5-0 nyumbani dhidi ya Brighton ulifanya matokeo hayo kuwa ya thamani zaidi kwa kocha huyo.
“Kuna mambo mengi tunayoweza kujifunza. Wakati mwingine msimu huu tunaweza kupata vipigo kama hivyo, kwa sababu huo ndio uhalisia wa timu zinazopanda Ligi Kuu,” Lampard ameongeza.
“Ni muhimu kukabiliana navyo kwa namna sahihi, kujifunza kutokana navyo na kubaki pamoja.
“Unapopoteza, ni rahisi kulaumiana na kuelekeza lawama pande tofauti. Lakini kundi letu lina nguvu na lina umoja mkubwa. Ushindi huu utatupa hisia nzuri, lakini tutabaki na miguu chini kwa sababu ni ushindi mmoja tu. Hata hivyo, ulikuwa muhimu kwetu.”