Mastaa Bongo wanavotoa albamu kwa kujipima ubavu
Muktasari:
- Katika miradi hiyo wanashirikiana na wenzao kutoka ndani na nje ya nchi, lakini wapo wanamuziki wametoa albamu au EP zikiwa hazina kolabo kabisa au kolabo moja pekee kama ifuatavyo.
Kila mara wanamuziki wa Bongo Fleva wanatoa albamu na Extended Playlist (EP) kwa ajili ya mashabiki wao, na mwishowe wapate fedha kutokana na mauzo hasa ya mtandaoni.
Katika miradi hiyo wanashirikiana na wenzao kutoka ndani na nje ya nchi, lakini wapo wanamuziki wametoa albamu au EP zikiwa hazina kolabo kabisa au kolabo moja pekee kama ifuatavyo.
1. Room Number 3 (2025): Ni EP ya pili kutoka kwa Mbosso na ya kwanza chini ya lebo yake ya Khan Music, ina jumla ya nyimbo sita ambazo zote hajashirikiana na mwanamuziki yeyote yule.
2. The African Princess (2018): Ni albamu ya kwanza na ya pekee kwa Nandy hadi sasa, ikiwa na nyimbo 12, na ni Aslay tu aliyesikika katika albamu hii.
3. PM (Poison Medicine) (2026): Ni EP ya tano kutoka kwa Ibraah, katika nyimbo zake tano ukiwemo ule maarufu, Uhakika, hajamshirikisha msanii yeyote.
4. Most People Want This (2023): Ni albamu ya tatu kwa Aika & Nahreel (Navy Kenzo), katika nyimbo zake 12, ni mmoja tu ndio wamefanya kolabo, nao ni ‘Hold On’ wakimshirikisha Fireboy DML kutokea Nigeria.
5. New Chui (2023): Ni EP ya pili kutoka kwa Rayvanny ambayo ina jumla ya nyimbo sita, huku akishirikishwa Abigail Chams pekee aliyesikika katika wimbo uitwao Stay.
6. University (2023): Ni albamu ya kwanza kuachiwa na kundi la Mabantu, ina nyimbo nane, huku wakimshirikisha msanii mmoja ambaye ni Baddest 47 aliyesikika katika wimbo, Shemeji.
7. After All (2025): Ni EP ya pili kutoka kwa Yammi ikiwa na nyimbo sita, humu amemshikisha Mdogo Sajent pekee aliyesikika katika wimbo, Sijafunzwa.
8. My Way (2026): Ni albamu ya pili ya Aslay, na ya kwanza chini ya Sony Music, ina nyimbo 14 huku msanii aliyeshirikishwa akiwa ni Chino Kidd ambaye amesikika katika wimbo unaokwenda kwa jina la Kipemba.
9. Melanin Therapy (2025): Ni EP ya kwanza kutoka kwa mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018, Phina, ina nyimbo tano bila kolabo yoyote.
10. Taste (2021): Hii ndio EP ya kwanza yake Nandy ambayo ilitoka ikiwa na nyimbo nne ambazo hakushirikiana na msanii yeyote. Baada ya EP hii zikafuata nyingine mbili, Wanibariki (2021) na Maturity (2022).