Kulikoni Mwanzo mbaya EPL Coventry, Spurs, Aston Villa?
Muktasari:
Haijalishi nini kilitokea msimu uliopita kumekuwapo na kipindi chote cha majira ya joto cha kurekebisha mambo. Usajili mpya, pengine kocha mpya, na mbinu mpya. Nini kinaweza kwenda vibaya? Oh, kila kitu? Safi kabisa.
LONDON, ENGLAND: TOTTENHAM Hotspur bado hawajafunga bao, Coventry bado hawajafunga wala kupata pointi, huku Aston Villa wakianza msimu kwa kusuasua tena.
Lakini, mwanzo mbaya una maana gani hasa, na je timu hizo zinaweza kujifunza chochote kutokana na mwanzo mbaya zaidi katika historia ya Ligi Kuu England? Matumaini yaliyopo mwanzoni mwa msimu mpya yanaweza kulevya pia.
Haijalishi nini kilitokea msimu uliopita kumekuwapo na kipindi chote cha majira ya joto cha kurekebisha mambo. Usajili mpya, pengine kocha mpya, na mbinu mpya. Nini kinaweza kwenda vibaya? Oh, kila kitu? Safi kabisa.
NDO KWANZAA
Tuko katikati tu ya Septemba, lakini kwa baadhi ya watu matumaini hayo kwa kiasi kikubwa yameyeyuka na badala yake kuibuka wasiwasi. Hofu ya msimu huu inaweza kuwa wa aina gani, na jinsi ambavyo mwisho wa Mei ijayo inaonekana kuwa mbali sana.
Coventry City walikuwa na kila sababu ya kuupani kwa hamu msimu wa 2026-27, msimu wao wa kwanza kurejea Ligi Kuu England tangu 2001, huku wakitoka katika msimu bora kabisa wa kushinda ubingwa wa Championship.
Na walikuwa wakipanda kilele cha wimbi la mafanikio. Kikosi hicho cha Frank Lampard ndicho pekee katika Ligi Kuu England ambacho hakijapata hata pointi moja msimu huu baada ya mechi nne, na bado hakijafunga hata bao moja, na mechi mbili kati ya hizo walicheza ugenini dhidi ya timu mbili zenye nguvu zaidi katika ligi, Arsenal na Manchester City.
Coventry walicheza vizuri kwa kiasi kikubwa katika mchezo wa pili kati ya hiyo, dhidi ya Man City na huenda walistahili kupata kitu. Hata hivyo, kipigo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya wenzao waliopanda daraja, Hull City na kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Brighton katika Uwanja wa Coventry Building Society Arenai, ni vigumu zaidi kuelezeka, na namna walivyodhalilishwa itakuwa iliwafanya watambue wazi kwamba ligi hiyo ina mambo magumu.
Coventry wamekuwa timu ya nane iliyopanda daraja kushindwa katika mechi nne za kwanza za msimu wa Ligi Kuu. Kati ya timu saba zilizotangulia, ni moja pekee iliyofanikiwa kuepuka kushuka daraja; Southampton 2012-13.
Ukiangalia timu zote zilizopoteza mechi nne za kwanza katika msimu wa ligi hiyo hali inakuwa ya kutia moyo kidogo kwa Conventry. Kumekuwa na matukio 18 kabla ya Coventry, na timu nane kati ya hizo ziliweza kuepuka kushuka daraja mwishoni mwa msimu, huku ya hivi karibuni ikiwa Everton 2024-25.
Kwa Coventry, waangalie Crystal Palace msimu wa 2017-18. Chini ya kocha mwingine aliyeitwa Frank (de Boer), Eagles hawakufunga bao wala kupata pointi hata moja katika mechi tano za kwanza na Mholanzi huyo alifukuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na Roy Hodgson, lakini mfululizo huo haukuishia hapo kwani Palace walicheza mechi saba bila kufunga bao wala kupata pointi.
Hata hivyo, ubora wa Hodgson hatimaye ulifanya kazi. Palace hawakuepuka tu kushuka daraja, bali kwa kushangaza walimaliza katika nafasi ya 11. Haishauriwi Coventry wamfukuze Frank. Bila shaka amejijengea sifa njema kutokana na kazi kubwa aliyofanya kuwapandisha Ligi Kuu England.
Pia, kumshawishi Hodgson mwenye umri wa miaka 79 kutoka kustaafu. Mfululizo mwingine wenye urefu sawa wa kushindwa kupata pointi mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu England ni wa Portsmouth, ambao hawakushinda hata mechi moja kati ya saba za kwanza 2009-10.
Walifunga mabao matatu katika mfululizo huo, lakini tofauti na Palace, hawakuboresha sana hali yao katika msimu mzima.
Portsmout walimaliza mkiani wakiwa na pointi 19, na ingawa walikatwa pointi tisa kwa kuingia katika usimamizi wa kampuni kutokana na matatizo ya kifedha, bado wangemaliza mkiani hata bila adhabu hiyo.
Kwa upande mwingine kuna Norwich City waliopoteza mechi sita za kwanza msimu wa 2021-22 na kumaliza mkiani wakiwa na pointi 22, huku timu nyingine tatu zikipoteza mechi tano za kwanza katika Ligi Kuu ikiwa ni Southampton 1998-99, Sunderland 2005-06 na Wolves uliopita.
Southampton walinusurika kushuka daraja na kumaliza nafasi ya 17, lakini Sunderland na Wolves zote zilishuka Championship baada ya kumaliza katika nafasi ya 20.
SASA ITAKUWAJE?
Coventry wanakwenda Nottingham Forest leo wakijaribu hatimaye kupata pointi ya kwanza, lakini siyo wao pekee walioanza msimu kwa hali isiyokuwa na furaha. Mambo yalipaswa kuwa tofauti kwa Tottenham baada ya kumaliza katika nafasi ya 17 katika misimu miwili mfululizo ya ligi hiyo.
Kocha Roberto De Zerbi aliwasaidia Spurs kubaki Ligi Kuu kwa tofauti ndogo sana ya pointi msimu uliopita, na klabu ikamuunga mkono katika dirisha la usajili lililopita. Hata hivyo, soka mara chache huwa rahisi hivyo, na hadi sasa Spurs wanajifunza hilo kwa vitendo.
Mechi nne za msimu mpya zimepita na kama Coventry, bado hawajafunga bao. Angalau wana pointi mbili baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Nottingham Forest na Everton, lakini hali ile ya kuumiza bado ianwakabili.
Ni mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo kushindwa kufunga katika mechi nne za kwanza za ligi katika msimu mmoja na, kama ilivyotajwa, ni Crystal Palace 2017-18 pekee iliyokuwa na mwanzo mrefu zaidi wa msimu wa ligi bila kufunga bao, ikiwa ni mechi saba.
Lakini, zimepita dakika 407 tangu Spurs wafunge bao la mwisho katika ligi na ni mara ya kwanza kushindwa kufunga katika mechi nne mfululizo tangu Septemba 2006. Mbali na Spurs na Coventry msimu huu, kumekuwapo na matukio matano yaliyotangulia ya timu kushindwa kufunga katika mechi nne za kwanza za Ligi Kuu England katika msimu mmoja. Mbali na Palace iliyotajwa hapo awali kulikuwa na Sheffield Wednesday 1994-95, Newcastle United 2005-06, Swansea City 2011-12 na Aston Villa uliopita. Muhimu zaidi, hakuna hata moja kati ya timu hizo iliyoshuka daraja. Nafasi ya chini kabisa ambayo timu yoyote kati ya hizo ilimaliza ilikuwa ya 13, iliyoshikiliwa na Sheffield Wednesday 1994-95.
Hilo linapaswa kutoa matumaini makubwa kwa Spurs. Villa walifunga bao lao la kwanza msimu wa 2025-26 katika mechi ya tano, na hatimaye wakaenda kuwa na msimu bora zaidi, wakimaliza katika nafasi ya nne na kushinda UEFA Europa League. Hata hivyo, unapaswa pia kuitaja Villa ya msimu huu.
Unai Emery amefanya maajabu katika kipindi chake na huenda akalazimika kufanya hivyo tena baada ya kikosi chake kudhoofika kwa kuuza wachezaji muhimu katika kipindi cha usajili wa dirisha kubwa lililopita.
Labda bila kushangaa kutokana na hali hiyo, wameanza msimu kwa kusuasua wakiwa na pointi moja tu katika mechi nne za kwanza, ambayo waliipata katika sare ya 0-0 ugenini dhidi ya Hull iliyopanda daraja.
Vipigo dhidi ya Brighton, Arsenal na Forest vimewaacha katika eneo la kushuka daraja, wakiwa na pointi moja pungufu kuliko walizokuwa nazo kipindi kama hiki msimu uliopita. Ni mara ya nne kwa Villa kuanza msimu wa Ligi Kuu bila kushinda katika mechi nne za kwanza baada ya misimu ya 1992-93, 1997-98 na 2025-26.
Huku nyuma mwanzo wa Fulham uliokuwa wa kusuasua ulipata msukumo Jumamosi iliyopita baada ya kupata sare iliyostahili dhidi ya Liverpool, ikiwa pointi ya kwanza msimu huu.