Frank Lampard aeleza furaha kuirejesha Coventry EPL
Muktasari:
- Coventry yenye pointi 86 katika Championship, ilijihakikishia kupanda daraja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Blackburn Rovers, ambapo bao la dakika za mwisho la Bobby Thomas liliwasaidia kupata pointi muhimu iliyowatosha kufanikisha ndoto hiyo.
COVENTRY, ENGLAND: KOCHA wa Coventry City, Frank Lampard, ameeleza kwa hisia furaha yake baada ya kuiongoza klabu hiyo kurejea kwenye Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 25.
Coventry yenye pointi 86 katika Championship, ilijihakikishia kupanda daraja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Blackburn Rovers, ambapo bao la dakika za mwisho la Bobby Thomas liliwasaidia kupata pointi muhimu iliyowatosha kufanikisha ndoto hiyo.
Lampard ambaye aliwahi kuichezea Chelsea na Manchester City kabla ya kuingia kwenye ukocha, alisema mafanikio hayo ni miongoni mwa makubwa zaidi katika maisha yake ya soka.
“Ninajivunia sana,” alisema Lampard. “Mara nyingi makocha huzungumzia wachezaji tu lakini mimi ninajivunia mimi mwenyewe, benchi la ufundi na wachezaji.”
Alikumbuka safari yao ilipoanza, akisema walifika Coventry wakiwa na matarajio madogo, lakini walikumbana na changamoto kubwa.
“Tulipokuja hapa miezi 15 iliyopita tulikuwa tunaanzia mahali pasipojulikana. Lakini tumefanya kazi kwa pamoja na kujenga kitu maalum,” alisema.
Lampard alisema mafanikio hayo yanalingana na baadhi ya mafanikio yake makubwa kama mchezaji, ikiwemo kushinda Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa akiwa na Chelsea.
“Hii ni moja ya mafanikio makubwa zaidi kwangu. Nimebahatika kushinda mataji makubwa kama mchezaji, lakini kufanya hivi kama kocha na klabu hii katika mazingira haya ni jambo la kipekee sana,” aliongeza.
Coventry, ambao walikuwa wamekumbana na changamoto kubwa ikiwemo kushuka hadi League Two mwaka 2017, wameonyesha ubora mkubwa na kurejea katika ngazi ya juu zaidi ya soka la England.
Klabu hiyo pia ilikosa nafasi ya kupanda kupitia mchujo ‘play-offs’ katika misimu iliyopita lakini msimu huu wamefanikisha lengo lao mapema wakiwa na michezo michache iliyosalia.