Prime
FOREMAN: Bondia aliyetajirika baada ya ngumi

Muktasari:
- Foreman alijulikana si tu kwa ustadi wake katika ulingo wa ngumi, bali pia kwa mafanikio yake makubwa katika biashara, hasa kupitia bidhaa maarufu kama George Foreman Grill, ambayo ilimpa utajiri mkubwa.
TEXAS, MAREKANI: DUNIA imepoteza mmoja wa mabingwa wa ngumi waliokuwa na umaarufu mkubwa zaidi, George Foreman, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.
Foreman alijulikana si tu kwa ustadi wake katika ulingo wa ngumi, bali pia kwa mafanikio yake makubwa katika biashara, hasa kupitia bidhaa maarufu kama George Foreman Grill, ambayo ilimpa utajiri mkubwa.
Foreman ambaye alifariki Machi 21, 2025, katika enzi za uhai wake alipigana mapambano 81, akishinda 76 na 68 kati hayo ilikuwa ni kwa knockout.
Leo tunaangalia utajiri aliouacha na aliokuwa anamiliki kabla ya kupatwa na umauti.

KAPIGAJE PESA
Hadi anapoteza maisha, alikuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola 300 milioni. Alipata pesa kupitia ngumi kwa wakati huo ingawa haikuwa ni kiasi kikubwa kwani ripoti kutoka tovuti ya Celebrity Net Wort, bondia huyu alipata Dola 5 milioni tu, kuanzia mwaka 1969 hadi mwaka 1977 alipostaafu masumbwi.
Kiasi kikubwa cha utajiri wake alikipata nje ya ngumi kupitia biashara alizokuwa anazifanya ambapo mojawapo iliyokuwa maarufu sana ni ile ya George Foreman Grill ambayo ilikuwa inatengeneza jiko maalumu la kuchomea nyama, kutengenezea pizza na burger.
Kupitia biashara hii alifanikiwa kutengeneza zaidi ya Dola 200 milioni na kila mwezi taarifa zinaeleza alikuwa akiingiza hadi Dola 4.5 milioni.
Grill zake zilipata umaarufu mkubwa kutokana na matangazo aliyokuwa akiyafanya akitumia jina lake hali iliyozaa matunda na kufanya biashara hiyo ipate umaarufu wa kutosha.

NDINGA
Alikuwa akimiliki magari mengi ya kifahari lakini aliripotiwa kuyaweka mnadani ya kuyauza mwaka 2023. Kati ya magari hayo ni pamoja na: 2005 Ford GT -Dola 330,000.
1963 Chevrolet Corvette-Dola 25,000.
1987 Ferrari Testarossa-Dola 143,000.
1959 Chevrolet Impala Tri-Power Convertible- Dola 153,000.
1999 Prevost Vantare H3-45 VIP-Dola 115,000.
MSAADA KWA JAMII
Alikuwa na taasisi mbili ambazo zimejikita katika kusaidia jamii. Ya kwanza ni George Foreman Youth and Community Development Center na nyingine ni The Foreman Foundation.
Bondia huyu pia alikuwa akihudumu kama mchungaji katika kanisa lake alilojenga huko Houston, Texas tangu mwaka 1980.

MJENGO
Foreman alianza kukaa na familia yake maeneo ya Kingwood, kitongoji cha kifahari cha Houston, Texas, ambapo alikuwa akiishi katika nyumba kubwa yenye bwawa la kuogelea nyuma, pia aliwahi kununua shamba lenye ukubwa wa ekari 300 huko Marshall, Texas, mji wake wa kuzaliwa.
Katika shamba hilo alilolifanya kama sehemu yake ya mapumziko alikuwa akifuga farasi, ng’ombe, na wanyama mbalimbali.
Mwaka 2002, alimiliki nyumba ya kifahari kando ya pwani huko Malibu, California, aliyonunua kwa Dola 2.3 milioni, ambayo aliitumia kama nyumba ya kuishi wakati wa likizo alipokuwa akienda Los Angeles. Nyumba yake ya kifahari zaidi ipo Huffman, Texas, aliyoinunua kwa Dola 9.5 milioni.

MAISHA NA BATA
Katika maisha yake alioa na kuacha mara tano, wakwanza ni Adrienne Calhoun aliyefunga naye ndoa kuanzia mwaka 1971 hadi 1974, wa pili ni Cynthia Lewi waliyedumu kuanzia mwaka 1977 hadi 1979, wa tatu ni Sharon Goodson (1981 hadi 1982), wanne Andrea Skeete (1982 hadi 1985) na wa mwisho ni Mary Joan Martelly ambaye alifunga naye ndoa kuanzia mwaka 1985 hadi umauti ulipomkuta. Kupitia wake zake hao watano, bondia huyu alipata watoto 12, watano wa kiume na saba wa kike.
Mtoto wake George III, ndio alifuata nyayo zake kwa kuwa bondia lakini hakufanikiwa kupata umaarufu kama ilivyokuwa baba yake.