Banda aandika historia Zambia ikiitandika Misri mabao 6-0 WAFCON
Muktasari:
- Banda alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kufunga mabao manne peke yake, alianza kwa bao la dakika ya 61 akifunga kwa mkwaju wa penati kabla ya kuongeza la pili dakika tatu baadae.
NAHODHA wa Zambia, Barbra Banda ameendelea kuandika historia kwenye soka la wanawake Afrika baada ya kuiongoza timu hiyo kuondoka na ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Misri katika mchezo wa Kundi C wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 mechi iliyopigwa Uwanja wa Stade Olympique de Rabat.
Banda alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kufunga mabao manne peke yake, alianza kwa bao la dakika ya 61 akifunga kwa mkwaju wa penati kabla ya kuongeza la pili dakika tatu baadae.
Alifunga bao la tatu dakika ya 87 na lile la nne dakika ya 90 huku mabao mengine mawili yakiwekwa kambani na Racheal Nachula dakika ya 25 na Eneless Phiri dakika ya 90.
Zambia imeanza vizuri kwenye harakati zao za kuandika historia nyingine kwenye mashindano hayo.
Banda ambaye pia ni mmoja wa wachezaji wanaotajwa kuwa na uwezo mkubwa zaidi Afrika, mabao hayo manne yameongeza rekodi yake katika mashindano makubwa ya kimataifa.
Huu ni muendelezo tu kwenye mashindano ya WAFCON kwani si mara ya kwanza mshambuliaji huyo kufunga idadi ya mabao hayo aliwahi kufanya hivyo kwenye mashindano ya Olimpiki baada ya kufunga hat-trick mbili mfululizo mwaka 2021, jambo lililomfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kufanya hivyo kwenye historia ya soka la Olimpiki.
Idadi hiyo inamfanya Banda kuingia kwenye orodha ya wachezaji waliowahi kufunga mabao mengi kwenye mechi moja mshambuliaji wa zamani wa Nigeria, Perpetua Nkwocha alifanya hivyo mwaka 2004 dhidi ya Cameroon na Asisat Oshoala alifunga mabao manne dhidi ya Mali mwaka 2016.