Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FIFA yazindua sherehe za ‘digrii 360’

FIFA Pict

Muktasari:

  • Hatua hiyo inamaanisha kuwa wachezaji wote waliopo kwenye kikosi cha mechi, wakiwemo wale wa akiba ambao huenda wasicheze hata dakika moja, watasimama uwanjani pamoja na wenzao wakati nyimbo za taifa zikisikika.

GUADALAJARA, MEXICO: KOMBE la Dunia 2026 linatarajiwa kuwa mashindano makubwa zaidi kuwahi kufanyika katika historia ya soka, lakini kabla hata mpira haujaanza kuchezwa, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limekuja na jambo jipya kunogesha mashindano hayo.

Katika moja ya uamuzi makubwa yaliyozua mjadala, FIFA imetangaza mabadiliko kwenye utaratibu wa kabla ya mechi, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, si wachezaji 11 wanaoanza mechi pekee watakaoshiriki wakati wa nyimbo za taifa, bali kikosi kizima cha siku ya mchezo.

Hatua hiyo inamaanisha kuwa wachezaji wote waliopo kwenye kikosi cha mechi, wakiwemo wale wa akiba ambao huenda wasicheze hata dakika moja, watasimama uwanjani pamoja na wenzao wakati nyimbo za taifa zikisikika.

Ni mabadiliko ambayo FIFA inaamini yataongeza mshikamano ndani ya timu, kuimarisha hisia za uzalendo na kuwapa mashabiki tukio la kipekee kabla ya pambano kuanza.

Kwa kawaida, tangu kuanzishwa kwa Kombe la Dunia mwaka 1930, nyimbo za taifa zimekuwa zikiimbwa na wachezaji 11 wa mwanzo pekee huku wachezaji wa akiba wakibaki kwenye benchi la ufundi.

Lakini kuanzia Kombe la Dunia la mwaka 2026 litakalofanyika katika mataifa ya Marekani, Canada na Mexico, desturi hiyo ya karibu karne moja sasa itabadilika rasmi.

FIF 03

KILA MCHEZAJI AJIHISI SEHEMU YA TIMU

Kwa mujibu wa FIFA, lengo kubwa la mabadiliko hayo ni kuhakikisha kila mchezaji anajihisi kuwa sehemu ya timu bila kujali kama anaanza kikosini au la.

Katika soka la kisasa, mchango wa mchezaji hauishii kwa wale wanaoanza mechi pekee. Wachezaji wa akiba mara nyingi huamua matokeo ya michezo mikubwa kupitia mabadiliko ya dakika za mwisho, jambo ambalo FIFA inaamini linastahili kutambuliwa hata kabla ya mechi kuanza.

Badala ya kupanga mstari mbele ya benchi kama ilivyozoeleka, wachezaji wote pamoja na waamuzi watakusanyika kuzunguka duara la katikati ya uwanja wakati wa kupigwa kwa nyimbo za taifa.

Taswira hiyo mpya inatarajiwa kuwa moja ya picha zitakazotambulisha Kombe la Dunia 2026 kwa mabilioni ya watazamaji duniani.

FIF 02

INFANTINO ATOA SABABU ZA MABADILIKO

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, amesema mabadiliko hayo ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Kombe la Dunia kuwa tukio la kipekee zaidi kwa mashabiki.

“Kadri Kombe la Dunia linavyoendelea kukua, nasi tunaendelea kuboresha namna mchezo unavyoshuhudiwa na mashabiki. Sherehe za kabla ya mechi katika Kombe la Dunia 2026 zitakuwa tofauti kabisa,” anasema Infantino.

Kwa mujibu wa Infantino, soka limebadilika kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni na FIFA inaamini uzoefu wa mashabiki nao unapaswa kubadilika.

Amesema kuwa kuona wachezaji wote wa timu mbili pamoja na waamuzi wakisimama katikati ya uwanja wakati wa nyimbo za taifa kutaleta hisia za umoja, heshima, fahari ya taifa na mshikamano ambao haujawahi kuonekana hapo awali.

Kwa mtazamo wa FIFA, nyimbo za taifa si tukio la kawaida tu kabla ya mechi, bali ni sehemu ya utambulisho wa taifa na hisia za mashindano makubwa zaidi duniani.

FIF 06

SHEREHE MPYA ZA DIGRII 360

Mbali na mabadiliko ya namna wachezaji watakavyopangwa, FIFA pia imezindua mfumo mpya wa burudani uitwao “360-Degree Ceremony”.

Huu ni mfumo ambao utahakikisha kila shabiki ndani ya uwanja anapata uzoefu sawa bila kujali amekaa upande gani.

Katika mfumo huo, bendera kubwa za mataifa zitafunguliwa kwa wakati mmoja pande mbalimbali za uwanja huku skrini kubwa, muziki, taa maalumu na maonesho ya kisasa yakitumika kuongeza msisimko.

FIFA inaamini kuwa mashabiki wanaokuja viwanjani wanapaswa kupata thamani zaidi ya tiketi wanazonunua na ndiyo maana imeamua kuwekeza nguvu kubwa katika sherehe za kabla ya mechi.

Kwa mara ya kwanza, kabla hata mpira haujaanza kuchezwa, uwanja mzima utakuwa sehemu ya tamasha la burudani.

FIF 01

KILA MECHI KUWA KAMA FAINALI

Wachambuzi wa masuala ya michezo wanaamini FIFA inalenga kuifanya kila mechi ya Kombe la Dunia ihisi kama fainali.

Katika miaka ya nyuma, maonesho makubwa yalikuwa yakionekana zaidi katika mechi za ufunguzi au fainali pekee.

Safari hii, FIFA inataka hata mechi za hatua ya makundi ziwe na mvuto wa kiwango cha juu. Mabadiliko hayo yanaonekana kufuata mwenendo wa michezo mingine mikubwa duniani kama NFL ya Marekani, ambayo huweka mkazo mkubwa kwenye burudani ya mashabiki kabla ya mchezo kuanza.

FIF 04

FATAKI NA MOSHI WA RANGI

Habari njema zaidi kwa mashabiki ni kwamba FIFA haijaishia kwenye nyimbo za taifa na mabango makubwa pekee.

Shirikisho hilo limethibitisha kuwa kadri mashindano yatakavyoendelea kuelekea hatua za mtoano, vipengele vingine vya burudani vitaongezwa.

Miongoni mwa vitu vinavyotarajiwa kuonekana ni moshi wa rangi mbalimbali, fataki, maonesho ya taa za kisasa na teknolojia nyingine za kisasa zitakazoongeza hadhi ya mashindano. Lengo ni kuhakikisha kila mechi kubwa inakuwa tukio la kukumbukwa hata kabla ya dakika ya kwanza ya mchezo.

FIF 05

MEXICO KUANDIKA HISTORIA YA KWANZA

Mashabiki wa soka duniani hawatasubiri muda mrefu kuona mabadiliko hayo yakianza kutumika. Mfumo huo mpya utaanza rasmi katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia ambapo Mexico itavaana na Afrika Kusini mbele ya maelfu ya mashabiki watakaofurika katika Uwanja wa Azteca jijini Mexico City, Juni 11.

Mchezo huo hautakuwa wa kihistoria kwa sababu ya kuanza kwa Kombe la Dunia pekee, bali pia utakuwa mwanzo wa enzi mpya ya namna dunia itakavyoshuhudia soka.

FIF 07

REKODI MPYA KILA KONA

Kombe la Dunia 2026 tayari limeandika historia kwa kuwa na timu 48 badala ya 32 zilizokuwa zikishiriki hapo awali.

Litakuwa na mechi 104, idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika mashindano hayo, huku mataifa matatu yakishirikiana kuandaa kwa mara ya kwanza.

Sasa FIFA imeongeza sura nyingine ya historia kwa kubadilisha kabisa namna mechi zinavyoanza.

Ikiwa mabadiliko hayo yatapokelewa vizuri na mashabiki pamoja na timu, huenda yakawa sehemu ya kudumu ya Kombe la Dunia kwa miaka mingi ijayo.

Kwa sasa dunia inasubiri kuona kama ubunifu huo mpya utaongeza mvuto wa mashindano au kama utabaki kuwa moja ya majaribio makubwa zaidi kuwahi kufanywa na FIFA katika historia ya soka.